Jeshi la Polisi limezuia kufanyika kwa mkutano wa hadhara uliopangwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambao ulikuwa unatarajiwa kuhudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Tundu Lissu, tarehe 20 Septemba 2024 kama mgeni rasmi.
Katika barua inayoonekana kusainiwa tarehe 19 Septemba 2024 na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Tanga SP D. I. Mwambigiri, polisi wameeleza kuwa wamezuia mkutano huo kwa mujibu wa Kifungu cha 44 cha Sheria ya Jeshi la Polisi, wakisema kuwa mkutano huo una dalili kubwa za kuvuruga amani ndani ya wilaya na kuhatarisha usalama wa raia pamoja na mali zao.
"Kwa mujibu wa mamlaka niliyonayo kwa Kifungu cha 44 cha Sheria ya Jeshi la Polisi, ninazuia uwepo wa mkutano huo kwani una dalili kubwa za kuleta uvunjifu wa amani ndani ya wilaya na kuhatarisha usalama wa raia na mali zao," ilisomeka sehemu ya barua hiyo iliyotumwa kwa ofisi ya CHADEMA wilayani Tanga.
Polisi pia wameonya kuwa kukiuka maagizo hayo ni kosa la jinai kwa mujibu wa Kifungu cha 45 cha Sheria ya Jeshi la Polisi, ambapo adhabu stahiki itachukuliwa dhidi ya wahusika. "Kukiuka kwa maagizo haya ni kosa la jinai, na mtashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni za adhabu," ilieleza zaidi barua hiyo.
Barua hiyo imeeleza kuwa mkutano huo ungetumika kama maandalizi ya maandamano makubwa yaliyopangwa kufanyika Dar es Salaam tarehe 23 Septemba 2024, yaliyoelezwa kuwa yana nia ovu ya kuvuruga utulivu wa Taifa.
Hata hivyo, taarifa za CHADEMA zinaeleza kuwa mkutano huo ulikuwa uambatane na zoezi la kuhani msiba wa Mzee Ali Mohamed Kibao, aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya CHADEMA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limewakamata Watu watano kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi kwa kuwakamata na kuwaua Watu wawili kisha kuteketeza miili yao kwa moto.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith M. Swebe , leo September 20,2024 imesema “Waliouawa na mili yao kuteketezwa kwa moto ni Ntawa Limbu (32), Mkulima na Mkazi wa Mtaa wa Buzunza na mwenzake aliyejulikana kwa jina moja la Suma”
“Chanzo cha kufanya halifu huo wa kujichukilia sheria mkononi ni kwamba inasemekana Marehemu hao walikuwa wanamiliki mali zinazosadikika kuwa ni za wizi mara baada ya taarifa kumfikia Mhanga aliyewahi kuibiwa aliweza kuhamasisha kundi la Vijana Waendesha pikipiki maarufu bodaboda na kuanza kuwatafuta Watuhumiwa ambao kwa sasa ni Marehemu”
“Uchunguzi unakamilishwa ili taratibu zingine za kisheria zifuate za kuwafikisha Mahakamani Watuhumiwa hao, Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linaendelea kutoa wito kwa baadhi ya Wananchi kuacha tabia za kujichukilia sheria mkononi kwani ni kosa kisheria, Jeshi la Polisi litawakamata na kuwafikisha Mahakamani”
#MillardAyoUPDATES