Award winning TV/Radio Personality | Hosting Amplifaya on CloudsFM |Journalist from Tanzania covering East Africa and beyond | Bookings [email protected]
Simba SC imeibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaochezwa leo, Oktoba 29, 2026.
Bao la Simba limefungwa na Rushine De Reuck dakika ya 42 na kuipa timu hiyo ushindi katika mchezo huo.
#MillardAyoUPDATES
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, ameagiza kukamatwa kwa baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Lukonde, Kata ya Tomondo, Halmashauri ya Morogoro, wanaodaiwa kumtishia usalama Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Ismail Mkimbu, kwa kutoridhishwa na maamuzi yake kuhusu masuala mbalimbali.
Agizo hilo limetolewa wakati wa mkutano wa Mkuu wa Mkoa na Wananchi wa Kijiji hicho, ambacho kina mgogoro wa ardhi kati ya Wananchi na Mwekezaji, baadhi ya waliokamatwa wanadaiwa kutoridhishwa na maamuzi ya Serikali yaliyotolewa awali kuhusu eneo linalogombaniwa.
Mkutano huo ni sehemu ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ya kusikiliza kero za Wananchi na kutafuta suluhisho, Sendiga anatarajiwa kuzunguka Mkoa mzima kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.#MillardAyoUPDATES
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza mchakato wa kuangalia uwezekano wa kuingia ubia katika mradi wa Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Lobito (Lobito Refinery) nchini Angola.
Akizungumza leo, Oktoba 29, 2026, Ikulu ya Magogoni Jijini Dar es salaam, baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Angola, João Lourenço, Rais Samia amesema Tanzania imekaribishwa kushirikiana na Angola katika Sekta ya Mafuta, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Mataifa hayo mawili.
Rais Samia amesema kwa muda mrefu Angola imekuwa ikisafirisha mafuta ghafi nje ya Nchi, lakini tangu Rais Lourenço alipoingia madarakani, Serikali ya Angola imechukua hatua za kuanzisha viwanda vya kusafisha mafuta ndani ya Nchi hiyo.
#MillardAyoUPDATES
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC, Murtaza Mangungu amesema Klabu hiyo haina nia ya kumfukuza Mwekezaji, huku akidai kuna baadhi ya Watu wanaotanguliza maslahi yao binafsi badala ya kusimamia maendeleo ya michezo na ustawi wa klabu, hali ambayo amesema imekuwa ikisababisha migogoro ndani ya Simba.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam, Mangungu amesema baadhi ya Watu hao wamekuwa wakitumia fedha kwa ajili ya kumshambulia, kumtukana na kumdhalilisha, huku akidai kuwa fedha zinazotumika katika shughuli hizo zinaingia kwenye deni la mwekezaji wa klabu hiyo.
“Kuna Kikundi cha Watu ambacho badala ya kusimamia maslahi yanayohusu ustawi wa michezo Nchini na maendeleo ya vilabu, wao wanaangalia maslahi wanayopata katika mifuko yao na matumbo yao, pesa hizo wanazozipata ndizo zinazotuletea shida,” amesema Mangungu.
#MillardAyoUPDATES
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itafungua tena Ubalozi wake Nchini Angola ili kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kibiashara kati ya Mataifa hayo mawili.
Akizungumza leo, Oktoba 29, 2026, Ikulu ya Magogoni Jijini Dar es salaam, baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, Rais Samia amesema uamuzi huo unalenga kuendeleza ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola.
“Kwenye mazungumzo yetu nimemuarifu Mheshimiwa Rais kwamba Tanzania imeamua kufungua tena Ubalozi wake Nchini Angola, ambapo hivi karibuni nitateua Balozi ili tuweze kufanya kazi kwa karibu zaidi,” amesema Rais Samia.
#MillardAyoUPDATES
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamsaka Mwanamke anayedaiwa kumuiba Mtoto wa Kiume mwenye umri wa miezi mitatu ndani ya Kanisa la Living Water, lililopo Mtaa wa Kiseke “A”, Kata ya Kiseke, Wilaya ya Ilemela, Jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa leo Oktoba 29, 2026, tukio hilo lilitokea Oktoba 25, 2026, majira ya saa 7 mchana , wakati Mama wa Mtoto huyo, Godliver Bahati Zilahenda (23) alipokuwa Kanisani pamoja na mumewe, Galuma Kawekamo.
Inadaiwa kuwa wakati wa kutoa sadaka, Mwanamke huyo alimwomba Mama wa Mtoto amshikie Mtoto wake, hata hivyo, Mama huyo aliporejea kutoka kutoa sadaka, alibaini kuwa Mwanamke huyo ametoweka pamoja na Mtoto.
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoani humo linafanya uchunguzi baada ya miili ya Watoto wawili wa kiume, inayokadiriwa kuwa na umri wa miezi mitano hadi sita, kukutwa imetelekezwa kando ya Barabara katika Mtaa wa Chamwenda, Kata ya Nyasaka, Wilaya ya Ilemela, miili hiyo ilikutwa Oktoba 27, 2026, majira ya saa 12 jioni, baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa Wananchi.
#MillardAyoUPDATES
Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando, ameitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza kiwango cha miamala ya fedha kupitia simu za mkononi kutoka Shilingi milioni 10 hadi milioni 50 au hata milioni 100, ili kurahisisha malipo na kuendeleza juhudi za kupunguza matumizi ya fedha taslimu Nchini.
Akizungumza leo Oktoba 29, 2026 Bungeni Jijini Dodoma, Chipando amesema Wananchi na Wafanyabiashara wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kufikia ukomo wa miamala ya simu, hali inayowazuia kuendelea kutuma au kupokea fedha wanapofikia viwango vilivyowekwa na watoa huduma.
Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri Mhandisi Mshamu Ali Munde, amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza viwango vya miamala ya fedha kwa njia ya simu ili kurahisisha malipo, kuchochea biashara na kupunguza matumizi ya fedha taslimu, hata hivyo, amesema mifumo ya malipo ina taratibu tofauti za usimamizi, utambuzi wa Wateja na usalama wa miamala.
“Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza viwango vya miamala ya fedha kwa njia ya simu ili kurahisisha malipo, kuchochea biashara na kupunguza matumizi ya fedha taslimu.” Amesema Naibu Waziri. #MillardAyoUPDATES
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC, Murtaza Mangungu amewataka Wanachama na Mashabiki wa Klabu hiyo kuwa watulivu na kuepuka maandamano au vitendo vinavyoweza kusababisha migogoro, kufuatia mvutano unaohusu mchakato wa uchaguzi wa Viongozi wa klabu hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Oktoba 29, 2026, Jijini Dar es salaam, Mangungu amesema Serikali na Mamlaka zinazosimamia soka Nchini zinaendelea kutekeleza majukumu yake, hivyo hakuna sababu ya Wanasimba kuchukua hatua zinazoweza kuvuruga amani na mshikamano.
“Nawaomba tutulie, Serikali inafanya kazi yake na Mamlaka za Soka Nchini zinafanya kazi zilizopo chini ya dhamana yao, hatuna haja ya kuingia katika misukosuko ya aina yoyote,” amesema Mangungu.
#MillardAyoUPDATES
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba Murtaza Mangungu, amesema klabu hiyo haina Mtendaji Mkuu, akieleza kuwa nafasi hiyo ipo katika kampuni ya Simba Sports Club Company, ambayo ina Mtendaji Mkuu wake.
Akizungumza leo na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam, Mangungu amesema kuna Mtu mmoja aliyesajiliwa na Bodi ya Michezo ya Tanzania (BMT), huku mwingine akiwa amesajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), akisisitiza kuwa usajili huo unatokana na sheria tofauti.
“Simba Sports Club haina Mtendaji Mkuu, labda kama yupo basi ni kwenye Simba Sports Club Company ndiyo ina Mtendaji Mkuu, kuna mmoja amesajiliwa na BMT na mwingine amesajiliwa BRELA ni kutoka sheria tofauti, Katiba inasema Simba Sports Club inatakiwa kuwa na Mtendaji wake na tutamtangaza kwa Taifa” #MillardAyoUPDATES
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC, Murtaza Mangungu amesema mchakato wa uchaguzi, Tume ya Uchaguzi pamoja na Mkutano Mkuu wa klabu hiyo uliotangazwa kufanyika Januari 3, 2027, ni batili na haramu.
Mangungu ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 29, 2026, wakati akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, akieleza kuwa amepokea barua kutoka Serikalini yenye mwongozo kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusiana na mchakato huo.
Kwa mujibu wa Mangungu, taratibu zinazohusu uchaguzi na Mkutano Mkuu wa Simba zinapaswa kufuata mwongozo uliotolewa na Serikali.
#MillardAyoUPDATES
Klabu ya Azam FC imeibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa leo, Oktoba 28, 2026, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Jijini Dar es salaam.
Mabao ya Azam FC yamefungwa na Kipre Zunon, Hassan Mubiru, Feisal Salum Abdallah maarufu kama Fei Toto na Iddy Seleman Nado, huku Mbeya City ikishindwa kupata bao lolote katika mchezo huo.
#MillardAyoUPDATES
Watu wasiopungua 68 wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa baada ya treni mbili za mwendo kasi kugongana katika eneo la Urda, Mkoani Toledo, Nchini Hispania, Oktoba 28, 2026.
Ajali hiyo imehusisha treni ya AVE inayomilikiwa na Kampuni ya Renfe na treni ya Kampuni ya Iryo, iliyokuwa imesimama kwenye reli kabla ya kugongwa kwa nyuma.
Mgongano huo umesababisha baadhi ya mabehewa kutoka kwenye reli na kutumbukia kwenye mteremko, huku Vikosi vya Uokoaji vikiendelea na operesheni katika eneo la tukio.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, treni hizo zilikuwa zimebeba jumla ya Abiria takribani 544, huku njia za treni za mwendo kasi katika baadhi ya njia zimesitishwa wakati uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo.
#MillardAyoUPDATES
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa Viongozi watatu, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Oktoba 28, 2026, na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Shaaban Kissu, Rais Samia amemteua Angeline Lubala Mabula kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, akichukua nafasi ya Beno Morris Malisa ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Aidha, Rais Samia amemteua Dunford George Mpelumbe kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambapo kabla ya uteuzi huo, Mpelumbe alikuwa Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akichukua nafasi ya Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mwaimu aliyemaliza muda wake.
Katika uteuzi mwingine, Rais Samia amemteua Omar Ali Omar kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, akichukua nafasi ya Mohamed Khamis Hamad aliyemaliza muda wake.
Kabla ya uteuzi huo, Omar alikuwa Mkuu wa Idara ya Utawala, Mipango na Fedha katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume, Zanzibar.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uapisho wa Viongozi hao utafanyika katika tarehe itakayopangwa baadaye.
#MillardAyoUPDATES
Klabu za Yanga na Simba zinazoiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) msimu wa 2026/27 zimefahamu Wapinzani wao katika hatua ya Makundi baada ya kufanyika kwa droo ya michuano hiyo.
Kwa mujibu wa droo hiyo, Yanga imepangwa Kundi B pamoja na Zamalek SC ya Misri, MC Alger ya Algeria na Club Africain ya Tunisia.
Kwa upande wake, Simba imepangwa Kundi C pamoja na RS Berkane ya Morocco, Orlando Pirates ya Afrika Kusini na Colombe Sportive ya Cameroon.
Michezo ya hatua ya makundi inatarajiwa kuanza Novemba 27 hadi 29, 2026, huku raundi ya mwisho ikitarajiwa kuchezwa Januari 22 hadi 24, 2027.
#MillardAyoUPDATES
Droo ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) msimu wa 2026/2027 imezipanga timu za Tanzania, Azam FC na Singida Black Stars, katika makundi tofauti.
Azam FC imepangwa Kundi B pamoja na AS FAR ya Morocco, Al Ahly Tripoli ya Libya na Durban City FC ya Afrika Kusini.
Singida Black Stars imepangwa Kundi C pamoja na AS Maniema ya DR Congo, Red Arrows ya Zambia na mshindi wa michezo inayohusisha CRB ya Algeria, AS Douanes ya Mauritania na HFC ya Côte d’Ivoire.
Kwa upande wa Kundi A, timu zilizopangwa ni Al Ahly FC ya Misri, Raja CA ya Morocco, ASKO de Kara ya Togo na CD 1 Agosto ya Angola, Kundi D linaundwa na USMA ya Algeria, CS Sfaxien ya Tunisia, Black Bulls ya Msumbiji na AS Real de Bamako ya Mali.
Mechi za kwanza za hatua ya makundi zimepangwa kuchezwa Novemba 27 hadi 29, 2026, huku hatua hiyo ikitarajiwa kukamilika Januari 24, 2027.
#MillardAyoUPDATES
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema ushindi wa Jihan Dimack katika mashindano ya Miss Grand International 2026 umefungua milango ya fursa kwa Tanzania, huku akieleza kuwa Serikali ipo katika mazungumzo ya kwamba mashindano ya Miss World yafanyike Nchini kwa miaka mitatu mfululizo.
Makonda ameyasema hayo leo, Oktoba 28, 2026, Bungeni Jijini Dodoma, wakati wa utambulisho wa Jihan, huku akimpongeza Mfanyabiashara Jennifer Jovin, maarufu kama Niffer, kwa kuwa miongoni mwa Watu waliojitokeza kumuunga mkono Jihan wakati wa mashindano hayo.
Amesema Vijana wakipewa nafasi wana uwezo wa kuliunganisha Taifa, akieleza kuwa Waafrika waliungana kumuunga mkono Jihan hadi kufanikisha ushindi wake.
Aidha, Makonda amesema kuna matarajio ya Mashindano ya Miss World 2027 kufanyika nchini Tanzania, huku akiwatania Vijana ambao bado hawajaoa au kuolewa kwamba wanaweza kupata fursa ya kupata wenza kupitia mashindano hayo.
#MillardAyoUPDATES