Uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Tanzania imejaaliwa utajiri wa maliasili na wingi wa bioanuai zilizopo katika mifumo mbalimbali ya ikolojia, kama vile misitu, uoto wa savana, mito na fukwe za bahari, hivyo kuifanya nchi kuwa eneo muhimu sana la bioanuai duniani.
Kwa Mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania ina ardhi yenye rutuba, rasilimali za baharini na fukwe, mito na maziwa, ambayo huchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Usimamizi madhubuti wa maliasili huwezesha uhifadhi endelevu wa mazingira, ambao ni muhimu katika kuendeleza huduma na manufaa kwa rasilimali zenyewe na watu.
Katika kufikia lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati ngazi ya juu ifikapo 2050, matumizi endelevu ya rasilimali hizi na usimamizi wake madhubuti ni muhimu. Uhifadhi wa mazingira unahusisha ulinzi wa bioanuai, usimamizi endelevu wa rasilimali maji, ardhioevu, matumizi sahihi ya ardhi na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira. Mabadiliko ya tabianchi yanayodhihirishwa na ongezeko la joto, hali ya hewa isiyotabirika, na majanga yanayotokea mara kwa mara, yanatishia maendeleo endelevu ya nchi.
Dira inabainisha kuwa madhara ya mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na vipindi virefu vya ukame, mafuriko, na kupotea kwa bioanuai, ambayo moja kwa moja yanaathiri sekta zinazotegemea hali ya hewa katika uzalishaji, kama vile kilimo, uvuvi, maji na misitu. Kukabiliana na changamoto hizi kunahitaji juhudi za pamoja katika kujenga ustahimilivu wa jamii ili ziweze kuendana na mabadiliko ya tabianchi na mazingira.
Hatua muhimu zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ni pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, kuhamasisha matumizi bora ya rasilimali, na kuimarisha mikakati ya uhifadhi wa mazingira. Kwa kufanya hivyo, Tanzania italinda mazingira, kuendeleza uchumi na kuhakikisha ustawi wa wananchi wake kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Nguzo hii inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi inayothamini, kulinda na kutumia rasimali zake za asili kwa uendelevu, kuhifadhi mazingira na kuwa na ustahimilivu wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Kwa kuwa na mikakati madhuburi ya kulinda mifumo ya ikolojia na kukuza ustahimilivu, Tanzania itakuwa ni nchi yenye maisha bora, usawa, na ustawi kwa watu wake na urithi wake wa asili.
Serikali imemuagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa Kituo cha Maendeleo ya Uzalishaji wa Samaki cha Rubambagwe wilayani Chato, mkoani Geita, kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Machi 30, 2026, ikisisitiza kuwa hakuna kisingizio chochote hasa baada ya fedha za mradi huo kutengwa na kutolewa tayari.
Agizo hilo limetolewa Januari 5, 2026, na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo, ambapo alionesha kutoridhishwa na kucheleweshwa kwa utekelezaji wake pamoja na kukosekana kwa shughuli zozote za ujenzi katika eneo la mradi.
Dkt. Bashiru alisema hali aliyoikuta haiendani na ratiba ya utekelezaji iliyowasilishwa na mkandarasi, akibainisha kuwa licha ya fedha kutolewa kwa wakati, hakuna nyenzo za ujenzi wala kazi inayoendelea katika eneo hilo.
“Kwa mradi wa aina hii, ambao tayari umewezeshwa kifedha, kunapaswa kuwepo dalili za wazi za utekelezaji. Hata hivyo, hakuna saruji, hakuna kokoto, wala hakuna kazi yoyote ya ujenzi inayoendelea,” alisema Dkt. Bashiru.
Kutokana na hali hiyo, Waziri alimwagiza Mhandisi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. George Kwandu, kuwasilisha nakala za mpango wa utekelezaji wa awamu ya pili kwa ofisi yake pamoja na kwa mamlaka muhimu ikiwemo Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mbunge wa Jimbo husika, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kamanda wa Polisi Mkoa pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Aidha, wadau hao wameelekezwa kufanya ufuatiliaji wa kila wiki wa utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha kazi zinaendelea kwa mujibu wa mpango, viwango vilivyokubaliwa na ndani ya muda uliopangwa.
Mradi wa Kituo cha Maendeleo ya Uzalishaji wa Samaki Rubambagwe unatarajiwa, mara baada ya kukamilika, kuwa kitovu cha uzalishaji wa vifaranga vya samaki, tafiti za kisayansi na uendelezaji wa ufugaji wa samaki wa kisasa, hatua itakayochangia ongezeko la uzalishaji wa samaki, kuboresha kipato cha wafugaji na kuimarisha sekta ya uvuvi katika Ukanda wa Ziwa na Taifa kwa ujumla.
Mimi sio mtabiri lakini kwa takwimu hizi na ushahidi huu, Dkt. Samia Suluhu Hassan akimaliza uongozi wake huu wa awamu ya pili, watanzania wenyewe tutampa Tuzo ya uongozi bora, achana na ile aliyopewa na Baraza la Wanawake la Chadema Mwaka 2023 au ile ya Gates Foundation, anastahili zaidi.
Namba hazidanganyi kila nikitathimini uwezo wake alioonyesha katika miaka minne iliyopita katika huduma za jamii, uwezeshaji wa wananchi, miradi ya kimkakati, utekelezaji wa sera za uchumi naiona historia ikimkumbuka kama kiongozi kinara ndani na nje ya mipaka yetu.
Kulingana na ripoti za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) ulikuwa 4.7% mwaka 2022, ukapanda 5.2% mwaka 2023, na kufikia 6.1% mwaka 2024 nainatajiwa huenda ikafika 7.0%. Ongezeko kubwa la GDP kufikia TZS trilioni 156.6 mwaka 2024. Hii imetokana na maendeleo katika sekta za kilimo, utalii, na uwekezaji wa kigeni, hii inaonyesha jinsi Dkt. Samia alivyofungua milango kwa wawekezaji wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bomba la mafuta na kuifanya Tanzania kuwa lango la biashara Afrika Mashariki kupitia Bandari ya DSM.
Utekelezaji wa miradi ya kimakakati. Tayari mradi wa Daraja la Kigongo–Busisi, refu zaidi Afrika Mashariki, likiunganisha Tanzania na masoko ya kikanda kupitia Ziwa Victoria umekamilika. Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere(JNHPP), ambao umechangia ukuaji wa uchumi kwa 5.5% mwaka 2024, na reli ya Kisasa(SGR) tayari Tanzania ndiye kinara Afrika Mashariki. Kila sekta ya uzalishaji mali imeguswa na matokeo yako dhahiri. Mfano mzuri katika sekta ya mifugo mauzo ya nyama yamepanda hadi tani 14,701 yenye thamani ya dola milioni 61.4 mwaka 2025.
Katika huduma za jamii, Dkt. Samia ameonyesha kujali maisha ya kila mwananchi. Mnamo Mei 2025, alitangaza ongezeko la mishahara ya wafanyikazi wa umma kwa 35.1%, kutoka TZS na hivyo kuimarisha uwezeshaji wa familia nyingi. Sekta ya elimu na jinsia imefaidika pia, kwa kutoa elimu bure katika shule za serikali na kuondoa vizuizi kwa wanafunzi wajawazito, na hivyo kuwapa fursa zaidi wanawake na vijana. Hii imechangia kuunganishwa kwa vijiji 3,731 ( 30%) na gridi ya umeme kutoka 8,587 mwaka 2021 hadi 12,318 Julai 2025. Aidha, madini madogo yamechangia 20% ya mapato ya sekta ya madini mwaka 2021/22, kutoka TZS bilioni 124.6 nje ya TZS bilioni 623.
katika sera za kisiasa na kimataifa, Dkt. Samia amefuata falsafa ya "4R” (Reconciliation, Resilience, Reforms, Rebuilding), akirudisha uhuru wa mikutano ya kisiasa na kurejesha leseni za vyombo vya habari vilivyozuiliwa. Namba hizi na maendeleo haya, ni wazi kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan anaandika historia kwa wino wa dhahabu bila kelele wa majivuno.
Serikali kupitia Wizara ya Madini imetangaza rasmi orodha ya huduma na bidhaa 20 zinazopaswa kutolewa Migodini kupitia kampuni zinazomilikiwa na watanzania kwa asilimia 100 ikilenga kuongeza wigo wa ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzimawa sekta ya madini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde Januari 5, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari na kueleza kuwa, hatua hiyo imefanyika baada ya kufanywa marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini za Mwaka 2018.
Akizungumzia manunuzi ya huduma na bidhaa kwa kampuni za kitanzania amesema yameongezeka kutoka kiasi cha Shilingi trilioni 1.85 kati ya manunuzi ya huduma na bidhaa za jumla ya kiasi cha Shilingi trilioni 3.01 sawa na asilimia 62 kwa mwaka 2018 hadi kufikia Shilingi trilioni 4.41 ambayo ni sawa na asilimia 88 ya kiasi cha Shilingi trilioni 5.00 ya manunuzi yote yaliyofanyika mwaka 2024.
Kwa upande wa ajira kwenye miradi ya madini, amesema kumeshuhudiwa ongezeko la ajira kwa watanzania kutoka ajira 6,668 kati ya ajira 7,003 sawa na asilimia 95 kwa mwaka 2018 hadi kufikia ajira 18,853 kati ya ajira 19,356 sawa na asilimia 97 kufikia Desemba 2024.
Waziri Mavunde ameitaka sekta binafsi nchini Tanzania kuchangamkia fursa ya usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma migodini ili kuhakikisha fedha kiasi kikubwa inabaki nchini Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Jana Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, alifanya ziara katika Mradi wa Kituo cha Maendeleo ya Uzalishaji wa Samaki cha Rubambagwe wilayani Chato, mkoani Geita,
Katika ziara hiyo Waziri Kakurwa alibaini ucheleweshaji wa kuanza kwa utekelezaji wa Mradi huo huku kukiwa hakuna dalili zozote za kuonyesha kuna shughuli za ujenzi hali iliyoibua mjadala mpana unaovuka mipaka ya mradi mmoja.
Swali kubwa linalojitokeza si tu ucheleweshaji wa mradi, bali uwajibikaji wa viongozi waliokabidhiwa jukumu la kusimamia maendeleo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ni jambo la kushangaza na la kuumiza kwamba mradi uliotengewa na kupewa fedha tayari, unaonekana kusimama bila shughuli zozote, huku viongozi wa ngazi ya Mkoa, Wilaya, Mbunge wa Jimbo, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na vyombo vya ulinzi wa maadili ya matumizi ya fedha za umma kama TAKUKURU wakiwa kimya, hadi pale Waziri wa Serikali Kuu alipofika kwa ziara ya kushtukiza.
Je, hawa si viongozi wanaoishi karibu na wananchi? Na je, hawakupaswa kuona, kusikia na kuchukua hatua mapema ili hata Waziri anapopita akute kuna shughuli za ujenzi zinazoendelea eneo la Mradi?
Kwa mantiki ya kiutawala, viongozi hawa ndiyo nguzo ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa, ndiyo macho na masikio ya Rais katika maeneo yao. Ndiyo wanaopaswa kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati, kwa viwango vinavyotakiwa na kwa thamani halisi ya fedha za umma.
Kushindwa kufanya hivyo si tu uzembe wa kiutendaji, bali ni kuiangusha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa vitendo.
Katika kipindi hiki ambacho wananchi wanataka kuona, mabadiliko ya kweli ya kiutendaji, miradi inayokamilika kwa wakati, zinapatikana ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, na fursa za kiuchumi zikifunguliwa,
Ni aibu kubwa kushuhudia miradi ikisimama kimya huku viongozi wakisubiri ziara za mawaziri ndipo “madudu” yaibuliwe hadharani.
Kinachotokea Geita kinapaswa kuwa kengele ya tahadhari kwa Taifa zima. Swali la kujiuliza ni moja tu, kama hili limeonekana Geita, ni miradi mingapi nchi nzima inakabiliwa na changamoto kama hii kutokana na uzembe wa viongozi wachache wasiotaka kuwajibika?
Serikali ya Rais Samia imeonyesha dhamira ya dhati ya uwajibikaji, uwazi na kusimamia maendeleo. Kinachohitajika sasa ni viongozi wa kati kuacha tabia ya “kusubiri maagizo kutoka juu” na badala yake watimize wajibu wao kwa weledi, uadilifu na ujasiri wa kuchukua hatua kwa wakati.
TAKUKURU, kwa nafasi yake ya kikatiba, haina budi kuwa mstari wa mbele si kusubiri maagizo au ziara za viongozi wakuu, bali kufanya kazi ya kuzuia, kuchunguza na kuchukua hatua mapema pale dalili za uzembe au matumizi mabaya ya fedha za umma zinapoonekana.
Kadri Taifa letu linavyoendelea, Utafiti na Maendeleo ni nyenzo muhimu katika kuongeza ubunifu, kutatua changamoto za ndani, na kuongeza tija katika uzalishaji.
Vilevile, utafiti na maendeleo huimarisha ukuzaji wa ustadi, husaidia kutoa mwongozo wa uundaji wa Sera, na kukuza mbinu endelevu za maendeleo, hivyo kuimarisha ushindani wa nchi katika soko la kimataifa.
Kwa kutambua umuhimu huu, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaeleza kuwa, Serikali imechukua hatua madhubuti za kuongeza kasi ya utafiti, ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya utafiti, kuimarisha ushirikiano baina ya vyuo vikuu, taasisi za utafiti na sekta za uzalishaji na huduma, sambamba na kuongeza juhudi za kuhamasisha maendeleo na matumizi ya teknolojia bunifu.
Hatua hizi zimechochea ongezeko la kiwango cha ubunifu, ambalo linadhihirishwa na kuongezeka kwa kampuni zinazochipukia, vituo vya ubunifu, vituo vya kulea na kustawisha mawazo ya biashara na programu za ukuzaji wa biashara.
Aidha, Dira inaonesha kuwa taasisi za elimu nchini zimeongeza mkazo kwenye Utafiti na Maendeleo, sambamba na kuimarisha mifumo ya kulinda hakimiliki, jambo linalosaidia kuhifadhi haki za wabunifu na kukuza utamaduni wa ubunifu na uvumbuzi.
Kwa upande wa Elimu, katika miaka mitano ijayo Serikali itaanza utekelezaji kamili wa maboresho ya Sera ya Elimu inayosisitiza elimu ujuzi. Tutaendelea kuweka mkazo zaidi kwenye masomo ya sayansi na hisabati (STEM).
Azma ya Serikali ni kuongeza wanasayansi wabobezi katika eneo la sayansi ya data, akili unde, sayansi ya kompyuta na teknolojia za viwanda. Tutatumia Mfuko wa Samia Scholarship kusomesha wanasayansi hawa ndani na nje ya nchi. Jambo hili litakwenda sambamba na kukamilisha shule maalum za Sekondari za Wasichana za Sayansi na zile za vipaji za Wavulana katika kila mkoa. Ili kuhakikisha mitaala na silabasi zetu zinatekelezwa kikamilifu, tutaunganisha kwa njia ya kidijiti shule za vijijini na mijini ili kubadilishana uzoefu na taarifa.
JIJI la Arusha, ambalo ni kitovu cha utalii nchini Tanzania, limepata shavu jingine la kimataifa baada ya Kituo cha Habari cha CNN (CNN Travel) kuliainisha kama moja ya maeneo bora zaidi duniani ya kutembelea kwa mwaka 2026.
Katika ripoti yake maalum iliyochapishwa Desemba 31, 2025, CNN imeiweka Arusha kwenye rada za wasafiri wa kimataifa, ikivutiwa na mchanganyiko wa urembo wa asili, utajiri wa kitamaduni, na uzoefu wa kipekee wa safari (safari experience) ambao haupatikani kwingineko duniani.
CNN Travel imeielezea Arusha kama "lango la dhahabu" la kuelekea kwenye vivutio vikubwa zaidi Afrika. Ripoti hiyo imebainisha kuwa Arusha imezungukwa na maajabu kama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kreta ya Ngorongoro, Tarangire, na Ziwa Manyara, huku ikiwa ni kambi kuu kuelekea kilele cha Mlima Kilimanjaro.
"Chini ya Mlima Meru unaovutia sana kuna Jiji la Arusha... mara nyingi ni lango la matukio mengine makubwa, lakini lenyewe lina urembo wa kipekee unaostahili kuonekana," ilieleza sehemu ya makala hiyo ya CNN.
Uchambuzi wa CNN umekwenda mbali zaidi na kuangazia Hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA) kama kivutio adhimu. Wasafiri wameshauriwa kutembelea hifadhi hiyo ili kujionea twiga na tembo wakizurura kwenye miteremko ya Mlima Meru, pamoja na maelfu ya ndege aina ya korongo wanaopamba Maziwa ya Momella.
Mandhari ya misitu mirefu na mazingira ya milimani yamefanya hifadhi hiyo kuanza kushindana kwa karibu na mbuga nyingine maarufu katika mzunguko wa Kaskazini.
Tanzania Yatikisa Mataifa Makubwa
Katika orodha hiyo ya maeneo bora ya kutembelea mwaka 2026, Arusha imekaa meza moja na maeneo mengine maarufu duniani kama:
Santa Monica (California, Marekani)
Kanazawa (Japan)
Adelaide (Australia)
Aragon (Hispania)
Devon (Uingereza)
Hatua hii imetafsiriwa na wachambuzi wa utalii nchini kama matunda ya kampeni endelevu za kuitangaza Tanzania kimataifa, zilizochochewa na filamu ya The Royal Tour na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha miundombinu ya usafiri , huduma kwa wageni na amani.
Kutajwa huku kwa Arusha kunategemewa kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa (International arrivals) mwaka huu, jambo litakalochochea biashara za hoteli, miongozo ya watalii (Tour Guides), na soko la bidhaa za asili, hivyo kuimarisha kipato cha wananchi mkoani hapa na nchi kwa ujumla.
SERIKALI ya Awamu ya Sita imetangaza mkakati mpya wa kuimarisha haki na amani nchini kwa kuipanua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia hadi ngazi ya wilaya nchi nzima. Hatua hiyo iliyotangazwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera, inalenga kuondoa kero na migogoro inayowakabili wananchi katika maeneo yao, hususan wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za kisheria.
Akiwa mkoani Morogoro, Dk. Homera amebainisha kuwa wizara imejipanga kuwafuata wananchi walipo ili kuwasogezea huduma hizo muhimu. Kampeni hii imejikita katika kutoa elimu na utatuzi wa changamoto za kisheria kwenye masuala mtambuka yakiwemo ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, na usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala. Lengo kuu ni kuhakikisha misingi ya haki za binadamu na utawala bora inaimarika kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa.
Uamuzi wa kupeleka huduma hizi wilayani unakuja baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikana mwaka jana, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya wananchi milioni 40 walifikiwa na kunufaika na kampeni hiyo. Kupitia usikilizaji wa mamilioni ya kero za kisheria, serikali imeweza kurejesha utulivu na mshikamano katika jamii nyingi zilizokuwa zimegubikwa na migogoro ya muda mrefu ya ndoa na ardhi.
Amani na Uchumi.
Uamuzi wa kumfuata mwananchi alipo unatajwa kuwa ni "Habari Njema" kwani msaada wa kisheria una uhusiano wa moja kwa moja na amani ya nchi. Wananchi wanapopata haki zao, migogoro hupungua, jambo linalopelekea,Kuimarika kwa utulivu na mshikamano wa kitaifa.
"Jukumu letu ni kuwafuata wananchi ili wanufaike na serikali yao. Tunataka kuondoa changamoto zinazowakabili ili kila mmoja ashiriki katika ujenzi wa taifa akiwa na amani moyoni," amesisitiza Dk. Homera.
Ufikishaji wa huduma hizi ngazi ya chini una tija kubwa katika kuimarisha amani na utulivu wa taifa. Wananchi wanapopata haki zao, hupata utulivu wa moyo unaowawezesha kujikita katika shughuli za uzalishaji mali na kuongeza kipato chao. Hivyo, Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia si tu chombo cha kutoa haki, bali ni injini ya kuleta utengamano wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi kwa watu wasiojiweza, hususan wanawake na watoto.
Mwaka 2026 umeanza kwa kishindo, huku sauti za Watanzania wa kada mbalimbali zikijielekeza katika jambo moja kuu, Amani kama mhimili wa maendeleo.
Aidha katika kipindi hiki ambacho Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza maridhiano, wananchi wameibuka na kutoa mwongozo wa jinsi wanavyotaka taifa liongozwe.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji, ameweka wazi kuwa bila amani, sekta nyeti kama utalii haziwezi kustawi. Kauli hii inaungwa mkono na Hussein Hassan (Mkufunzi MUM), anayekumbusha kuwa amani ndiyo inayotoa uhuru wa kuabudu na kusoma. Kwa upande wake, Athumani Saidi kutoka Mwanga, anabainisha kuwa uzalendo wa kweli unazaliwa pale tu nchi inapokuwa na utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Hofu ya vurugu imetajwa kuwa tishio kwa makundi yenye uhitaji. Husna Tauka wa Mikumi na Victoria Mkwizu wa Iringa, kwa nyakati tofauti, wameonya kuwa machafuko huwaumiza zaidi wanawake, watoto, wazee, na watu wenye ulemavu. Hali hii inamfanya Mary Makoa wa Morogoro kutoa wito kwa vijana kutoruhusu kuchochewa kuasi na kufanya vurugu, ili warithi taifa lenye amani ambalo waasisi walilijenga kwa miaka mingi.
Pamoja na sauti hizo za wananchi, mwaka 2026 unatajwa kuwa mwaka wa "Siasa za Busara" huku kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana kukiwa ni kiashiria tosha kuwa sauti za vijana sasa zinapaswa kuwa sehemu ya maamuzi na si kelele za pembezoni.
Uchambuzi wa mwelekeo wa sasa unaonyesha kuwa Taifa linahitaji kuachana na siasa za kejeli na matusi ambazo huwafanya vijana kuamini kuwa siasa ni uwanja wa visasi. Maridhiano ya Rais Samia yanapaswa kuwa sera na utamaduni, si hotuba pekee ili amani inayozungumzwa na akina Victoria Mkwizu na Mary Makoa iwe ya kudumu.
KATIKA kile kinachoonekana kama mtihani mzito kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) na uhuru wa mataifa madogo duniani, mtaalamu wa masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa, Christopher Makwaia, amechambua kwa kina anguko la Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro.
Makwaia anabainisha kuwa kukamatwa kwa Maduro na mkewe, Cilia Flores, Januari 3, 2026, kufuatia shambulio la anga la Marekani jijini Caracas, kumeibua maswali magumu kuhusu mustakabali wa sheria za kimataifa dhidi ya mataifa yenye nguvu.
Katika uchambuzi wake, Makwaia anahoji: "Je, sheria za kimataifa ni kinga ya wote, au ni lugha inayozungumzwa tu pale wenye nguvu wanaporuhusu?" Anabainisha kuwa kitendo cha Marekani kuingia katika ardhi ya nchi huru na kumkamata kiongozi aliyeko madarakani ni ukiukwaji wa wazi wa Ibara ya 2(4) ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Licha ya Marekani kudai kuwa ilikuwa ni operesheni ya "kusimamia sheria" kutokana na tuhuma mbalimbali, Makwaia anaonya kuwa hatua hii inatengeneza mfano mbaya ambapo mataifa makubwa yanaweza kuvamia nchi yoyote kwa kisingizio cha kujifanya polisi.
Sehemu muhimu katika makala ya Makwaia ni uhusiano kati ya operesheni hiyo na utajiri wa mafuta wa Venezuela. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, tamko la Rais Donald Trump kuwa Marekani itasimamia sekta ya mafuta ya nchi hiyo, linathibitisha kuwa rasilimali ndizo kiini cha mgogoro.
"Je, rasilimali za nchi ni mali ya wananchi kwa haki ya uhuru wao, au zinakuwa mali ya yule mwenye nguvu za kijeshi? Mataifa madogo yanaweza kujikuta yakichaguliwa washirika wa kibiashara na mataifa makubwa, na ushirika huo ukageuka kuwa liability (mzigo) pindi maslahi ya wenye nguvu yanapoguswa."
Makwaia katika maandiko yake anaonya kuwa hakuna cha kushangilia kwa tukio hilo kwani dunia inaingia katika zama ambapo "Mwenye Nguvu ndiye Mwenye Haki."
Anabainisha kuwa ikiwa Umoja wa Mataifa utashindwa kuzuia vitendo hivi, mataifa madogo yataacha kuamini diplomasia na badala yake kuanza kujiimarisha kijeshi ili kulinda uhuru wao, jambo ambalo litaifanya dunia kuwa mahali hatari zaidi.
Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amewatahadharisha Watanzania kuacha kutumiwa na watu wenye nia ovu kuhujumu uchumi wa nchi kwa kuharibu miundombinu, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni "kupiga ngumi kwenye ukuta na kuumiza mikono yako mwenyewe."
Akirejea matukio ya vurugu yaliyotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Dk. Mwigulu amebainisha kuwa uharibifu wa zahanati, barabara na mifumo ya mawasiliano hauikomoi Serikali, bali unamuumiza mwananchi wa kawaida ambaye kodi yake ndiyo iliyojenga miradi hiyo.
Hujuma za Kiuchumi Dk. Mwigulu amefafanua kuwa vurugu hizo hazikuwa maandamano ya kidemokrasia, bali ni mbinu ya mabeberu wanaotaka kuifanya Tanzania ishindwe kuzalisha ili wao waje kuchota rasilimali kama gesi asilia ya Lindi, makaa ya mawe na madini wakati Watanzania wakimwagiana damu.
"Wanaotaka kutuvuruga wanajua kuwa tukiingia kwenye giza la vurugu, hatutakuwa na muda wa kuzalisha. Matokeo yake tutaanza kuuziwa silaha na bidhaa kwa bei wanayotaka wao huku wakijifanya wanatupa misaada," alisema Dk. Mwigulu.
Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amenukuliwa akisema kuwa mafanikio ya Tanzania yanawanyima usingizi wale wanaotaka kuiona Afrika ikiendelea kuwa maskini. Amesema mabeberu hawafurahii kuona Tanzania inajitegemea kwa fedha zake yenyewe kujenga miundombinu ya kisasa.
"Tanzania haitaendeshwa kwa rimoti (remote control). Miundombinu tuliyonayo si mali ya Serikali, bali ni mali ya kila Mtanzania. Hata unaponunua shati la mtoto mchanga, unachangia ujenzi wa barabara na zahanati hizi," alisisitiza Dk. Mwigulu.
SERIKALI ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha rasilimali za madini nchini zinawanufaisha Watanzania moja kwa moja kwa kugeuza maeneo ya migodi kuwa vitovu vya viwanda na biashara.
Akizungumza katika ziara yake kwenye Eneo Maalumu la Kiuchumi la Buzwagi (BSEZ) wilayani Kahama hivi karibuni, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amebainisha kuwa serikali imedhamiria kukomesha utaratibu wa migodi kuagiza huduma na bidhaa kutoka nje ya nchi, jambo linalopoteza takribani Sh bilioni 5.1 kila mwaka.
Mkakati huo wa serikali unahusisha kugeuza eneo la Mgodi wa Barrick Buzwagi, lenye ukubwa wa hekta 1,333, kuwa eneo maalumu la viwanda baada ya shughuli za uchimbaji kusitishwa. Badala ya eneo hilo kubaki gofu, serikali imeweka miundombinu ya kisasa kuvutia wawekezaji.
"Malengo yetu ni kuifanya Kahama kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa migodi ya ndani na hata nje ya nchi. Tunataka fedha zinazotoka nje ya nchi zibaki nchini Tanzania," alisema Mavunde.
Waziri Mavunde amesisitiza kuwa serikali imeweka mazingira rafiki na kipaumbele kwa wawekezaji wazawa. Alibainisha kuwa kisheria, kuna huduma na bidhaa zaidi ya 20 ambazo wageni hawaruhusiwi kuwekeza, hivyo kuwapa uwanja mpana Watanzania kuchangamkia fursa hizo.
Uwekezaji huu unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 5,000 zilizokuwepo awali wakati wa uchimbaji, huku kampuni ya Nickel ikiwa tayari imeweka mtambo wa uchenjuaji wa dhahabu utakaosaidia wachimbaji wadogo wa eneo hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amethibitisha kuwa tayari wawekezaji 15 wameonyesha nia ya kuwekeza katika eneo hilo. Alitaja vivutio kama uwepo wa barabara bora, hoteli za kisasa, kiwanja cha ndege, na reli ya kisasa (SGR) itakayounganishwa kutoka Bandari Kavu ya Isaka hadi ndani ya eneo la uwekezaji.
"Mikakati imewekwa kuunganisha reli kutoka Isaka hadi ndani ya eneo hili ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa hadi asilimia 50," alisema Mhita, huku akiongeza kuwa kampuni kubwa kama Dangote (GSM) na TRC tayari zimeanza ujenzi wa vituo vya mizigo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA), Gilead Teri, ameeleza kuwa eneo la Buzwagi lina faida ya kijiografia kutokana na ukaribu wake na masoko ya nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, DRC, na Sudan Kusini.
Mbunge wa Kahama, Benjamin Ngayiwa, na mwenzake wa Msalala, William Magangila, wamepongeza hatua hiyo wakisema italeta neema kwa vijana na wachimbaji wadogo ambao sasa watapata vifaa vya utambuzi wa madini na zana za kazi kwa bei nafuu kutokana na kuzalishwa ndani ya nchi.
Nao wakazi wa Kahama, Hamza Hassan na Salome Gabriel, wameonyesha matumaini makubwa, wakisema uwekezaji huo utachochea biashara ndogondogo kama za 'mama lishe' na kuwawezesha kumudu gharama za maisha na masomo kwa watoto wao.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na wimbi la upotoshaji likiongozwa na mwanaharakati wa mitandao ya kijamii, Mange Kimambi, ambaye kwa mara nyingine ameonekana kukosa ukomavu wa kifikra kwa kuliombea Taifa la Tanzania livamiwe na Marekani. Hoja yake dhaifu ni kwamba uvamizi huo utakuwa "njia ya kuikomoa" serikali.
Hata hivyo, uchambuzi wa kina wa siasa za dunia unaonyesha kuwa Mange hajui maana ya uvamizi, hajui gharama ya damu ya Watanzania, na anaonekana kufurahia mateso ya binadamu wenzake kama inavyotokea sasa nchini Venezuela.
Venezuela: Shamba la Mawe, Sio Bustani ya Edeni
Mange amekuwa akishangilia kuanguka kwa Venezuela na uvamizi wa Marekani nchini humo, akidhani ni msaada wa kiungwana. Ukweli ni kwamba Venezuela haijaanguka ili kuwasaidia raia, bali imekuwa uwanja wa vita wa mataifa makubwa (Superpowers) yanayowania utajiri wa mafuta.
Kama ilivyo Ukraine kwa Urusi, au Taiwan kwa China, Venezuela ni muhimu kwa Marekani kwa sababu ya Jiografia na Rasilimali. Matokeo ya shinikizo hilo ni mfumuko wa bei uliokithiri, vifo, na mamilioni ya raia kukimbia nchi zao. Je, hili ndilo Mange analoliombea Tanzania?
Sera ya "Amani kupitia Nguvu" (Peace Through Strength)
Kauli ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu "amani kupitia nguvu" haina chembe ya sheria za kimataifa. Ni sera ya kulazimisha mataifa madogo kufuata matakwa ya taifa kubwa kwa shinikizo la kijeshi na kiuchumi.
Kudhani kuwa Marekani au taifa lolote la nje litakuja Tanzania kumlinda mwananchi wa kawaida ni ndoto ya mchana. Katika ulimwengu wa sasa, kila nchi inalinda maslahi yake (National Interests). Hakuna taifa linalomwaga damu ya askari wake ili "kumkomoa" kiongozi fulani kwa faida ya wananchi wa nchi nyingine bila kuchukua rasilimali kama malipo.
Uhaini au Harakati?
Kukosoa serikali ni haki ya kidemokrasia na ni jambo la afya kwa taifa. Lakini, kutamani nchi yako ivamiwe, raia wako wauawe, na miundombinu yako ibomolewe na mataifa ya kigeni, huo siyo uanaharakati—ni uzalendo uliokufa au balehe ya akili inayochelewa.
Kama kuna jambo la kujifunza kutoka kwa Venezuela na migogoro mingine, ni hili: Nguvu ya ndani, umoja wa kitaifa, na uchumi imara ndivyo pekee vinavyoweza kuleta heshima na uhuru wa kweli.
Sauti ya Busara: Tukatae Uchochezi
Watanzania wanapaswa kupuuza kelele hizi zinazotafuta "kiki" kupitia maafa. Uhuru wa bendera tuliopewa na waasisi wetu, kama alivyokumbusha Mama Maria Nyerere , unapaswa kulindwa kwa wivu mkubwa.
Mataifa ya nje yakija, hayaji na mikate; yanakuja na mabomu na mikataba ya uporaji wa rasilimali. Akili kumkichwa! Tanzania ni yetu sote, na matatizo yetu tutayamaliza wenyewe mezani kupitia mazungumzo na maridhiano, si kwa kuleta majeshi ya wageni yatakayotugeuza wakimbizi ndani ya ardhi yetu.
Tuukumbuke mambo 3:
Hakuna "Msaada" wa Bure: Mataifa makubwa yanafuata rasilimali (Mafuta, Madini, Bandari), siyo kuwakomboa wananchi.
Gharama ya Vita: Uvamizi wowote huacha makovu ya vizazi na vizazi; vifo, njaa, na uharibifu.
Uzalendo Kwanza: Harakati za kweli ni zile zinazojenga nchi, siyo zinazoombea nchi ibomolewe.
MAMA wa Taifa, Maria Nyerere, ametoa wito mzito kwa Watanzania kudumisha mshikamano na kutumia mazungumzo kama njia pekee ya kuvuka changamoto zinazolikabili taifa kwa sasa.
Akizungumza kwa busara na falsafa ya hali ya juu Januari 5, 2026, nyumbani kwake Msasani, Mama Maria amewataka Watanzania kutoishi kwa kukata tamaa, bali kutambua hatua ambazo nchi imepitia tangu enzi za Mwalimu Nyerere.
Makundi Matatu ya Ujenzi wa Taifa
Mama Maria amechambua historia ya nchi kupitia makundi matatu, akisisitiza kuwa kila kizazi kina deni kwa taifa lake:
Kundi la Kwanza: Ambalo lilipigania na kuleta Uhuru wa Bendera, likiongozwa na waasisi wa taifa hili.
Kundi la Pili: Ambalo lilijenga Misingi ya nchi, kuweka mifumo ya utawala na huduma za kijamii.
Kundi la Tatu: Ambalo ni kizazi cha sasa, ambacho alikielezea kuwa kina jukumu la Kuendeleza na Kuona Mwanga Mkubwa Zaidi wa maendeleo.
"Msikate tamaa. Kundi la kwanza lilitupa uhuru wa bendera, la pili likajenga misingi. Hili la tatu sasa linaona mwanga mkubwa zaidi. Tunachohitaji ni kukubaliana wote, tukae chini na kuzungumza ili kuelewana namna ya kuifikisha nchi mbele," alisema Mama Maria.
Mazungumzo na Maelewano
Kauli ya Mama Maria imekuja wakati ambapo taifa limekuwa likishuhudia vuta nikuvute katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiroho. Amesisitiza kuwa ujenzi wa taifa si kazi ya mtu mmoja au kiongozi pekee, bali ni matokeo ya maelewano ya pamoja.
Amewasihi vijana kutokata tamaa kutokana na changamoto za sasa, bali watumie mawazo yao kuleta mabadiliko chanya bila kusubiri kulaumu wengine.
Tuzo ya Heshima kutoka Angola
Kauli hiyo ameitoa wakati akipokea nishani ya heshima iliyotolewa na Serikali ya Angola kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kama ishara ya kuthamini mchango wake katika ukombozi.
Nishani hiyo ilikabidhiwa kwake na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, akiwa na Balozi wa Angola nchini, Domingos De Almeida Da Silva Coelho. Tukio hilo limeonekana kuwa kielelezo kuwa misingi iliyowekwa na kundi la kwanza na la pili bado inaheshimika kimataifa.
MATUNDA ya uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha elimu ya ufundi na vyuo vya kati yameanza kuonekana dhahiri, baada ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mkoani Mbeya kuzindua mtambo wa kisasa wa kusafisha dhahabu uliotengenezwa na wataalamu wa ndani.
Mtambo huo, ambao ni wa kwanza wa aina yake mkoani hapa, umetajwa kuwa ni mkombozi kwa wachimbaji wadogo wa kati kwani utaondoa matumizi ya zebaki—kemikali hatarishi kwa afya na mazingira ambayo imekuwa ikitumiwa kwa miaka mingi kutokana na ukosefu wa teknolojia mbadala.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, uongozi wa SIDO Mbeya umebainisha kuwa mtambo huo ni matokeo ya maboresho makubwa yaliyofanywa katika karakana za Kituo cha Uendelezaji wa Teknolojia (TDC). Wataalamu waliohitimu katika vyuo vya ufundi na kati nchini wametumia ujuzi wao kubuni mashine hiyo kulingana na mahitaji halisi ya wachimbaji wa Kitanzania.
"Lengo ni kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi. Mtambo huu utawasaidia wachimbaji kusafisha dhahabu kwa haraka, usalama na kwa tija zaidi, tofauti na mbinu duni za zamani," ilieleza taarifa ya SIDO.
Mageuzi ya Mashirika ya Umma
Uvumbuzi huu wa SIDO unaendana na mkakati mpana wa Serikali wa kufanya mageuzi makubwa ndani ya Mashirika ya Umma kuelekea mwaka 2030. Serikali imedhamiria kuongeza ufanisi na uwazi ili mashirika haya yachangie angalau asilimia 10 ya mapato yote yasiyo ya kodi.
Taarifa rasmi za Serikali zinaonyesha kuwa nia ni kuyajengea uwezo mashirika kama SIDO, STAMICO na mengineyo yaweze kushindana kimataifa na hata kuwekeza nje ya mipaka ya Tanzania, kama yanavyofanya mashirika ya kigeni yaliyopo nchini.
Uwajibikaji na Huduma kwa Wananchi
Mbali na mapinduzi ya viwanda, Serikali imesisitiza kuendelea kupambana na rushwa, ubadhirifu na uzembe maofisini ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi. Hatua za kuimarisha nidhamu na mifumo ya upimaji wa utendaji kazi (OPRAS) zimeendelea kuchukuliwa ili kuleta matokeo ya vitendo kama haya yanayoonekana SIDO Mbeya.
Kwa upande wao, baadhi ya wachimbaji wadogo mkoani Mbeya wameipongeza hatua hiyo wakisema kuwa teknolojia hiyo itapunguza gharama za uchenjuaji na kulinda afya zao, jambo ambalo ni kielelezo cha uongozi unaojali utu na maendeleo ya watu wa hali ya chini.
KATIKA hali inayozidi kuonyesha tofauti za kimtazamo kati ya wazalendo wa kweli na wale wanaoendeshwa na mihemko ya mitandaoni, mchambuzi wa siasa Alvin Habibu ametoa tamko zito linalowataka Watanzania kupuuza kelele za watu wanaodhani uongozi wa nchi ni sawa na kuposti picha au video kwenye mitandao ya kijamii.
Habibu, ambaye ana uzoefu wa uongozi tangu ngazi ya serikali za wanafunzi, amesema kuwa watu wanaopiga kelele kutaka mataifa ya nje yaingilie kati au wanaodhihaki juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, wakipewa nchi hata kwa nusu saa, watajikuta wakikimbia ofisi kutokana na ukubwa wa majukumu.
Urais Si "Kuposti" Instagram wala TikTok
Habibu amewashukia wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kuchochea vurugu na dharau kwa Taifa, akibainisha kuwa kuongoza nchi yenye watu milioni 60 kunahitaji akili iliyokomaa na uvumilivu ambao wakosoaji wengi hawana.
Alieleza kuwa tofauti ya mkosoaji na kiongozi ni kubwa kama mbingu na ardhi.
Mkosoaji wa mitandaoni mara nyingi husema chochote bila ushahidi ili kutafuta "Likes" na umaarufu, wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya maamuzi yenye athari za moja kwa moja kwa maisha ya mamilioni ya watu. Wakati mkosoaji hupoteza utulivu na kuanza matusi, Rais amekuwa akibeba ukosoaji huo kwa hekima, utulivu na kifua cha chuma huku akitekeleza miradi ya afya, maji na elimu.
"Kuna watu kazi yao ni kupiga kelele tu, wanadhani kuongoza ni mchezo. Mimi nimekuwa Rais wa chuo, tena chenye watu wachache, lakini nilijua maana ya kutolala. Leo hivi Rais Samia anaamka na ripoti za nchi nzima, matatizo ya mipakani, uchumi, na kero za watu milioni 60. Hawa wanaopiga kelele nusu saa tu hawawezi huo mzigo; wangepata shinikizo la damu (BP) mapema sana," alisema Habibu.
Uzalendo vs. Uhaini wa Kifikra
Akizungumzia kauli za hivi karibuni za Mange Kimambi zinazohimiza uvamizi wa kijeshi au shinikizo la mataifa makubwa kama Marekani dhidi ya Tanzania, Habibu amezitafsiri kama "uasi wa kifikra." Alieleza kuwa kutamani nchi yako ipitie machafuko kama ya Venezuela au nchi nyingine zilizovamiwa ni ishara ya kutokujua historia na kukosa utu.
Amesisitiza kuwa hata wale wanaojifanya wana majibu ya kila kitu, wakipewa dhamana, hawawezi kutatua hata robo ya kero wanazozipigia kelele. Hii ni kwa sababu ulimwengu wa siasa za kimataifa na uongozi wa ndani ni mgumu na unahitaji diplomasia ya hali ya juu, siyo kelele za kutafuta wafuasi (followers).
Kumuombea Rais na Kulinda Amani
Habibu amewataka vijana na Watanzania kwa ujumla kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Amesema kuwa uongozi wenye dhamira ya dhati kama anaoonyesha Rais kwa sasa unapaswa kulindwa na kupewa ushirikiano badala ya kupigwa vita kwa ajenda za watu binafsi waliojificha nje ya nchi.
"Kukosoa ni haki, lakini kukosoa kwa nia ya kubomoa na kuleta maadui wa nje ni usaliti. Tuache maneno, tufanye kazi. Rais anafanya kazi kubwa, na sisi wajibu wetu ni kumpa nguvu ili hili kundi la sasa la ujenzi wa taifa lione mwanga zaidi," alisisitiza Habibu.
Katika nchi ambayo vijana wanachukua zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi, Rais Samia Suluhu Hassan ameweka uwezeshaji kiuchumi wa vijana kuwa msingi wa maendeleo ya Taifa. Tangu alipoingia madarakani mwaka 2021 na kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ameanzisha sera na mikakati inayolenga kuwapatia vijana stadi za maisha, mitaji na fursa mbalimbali, ili kugeuza wingi wa vijana kuwa nguzo imara ya uchumi wa Taifa.
Moja ya mafanikio makubwa ni uwezeshaji wa elimu ya ufundi stadi (VETA). Idadi ya wanafunzi waliojiandikisha katika vyuo vya ufundi imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 29, kutoka wanafunzi 344,815 mwaka 2021 hadi kufikia 446,252 mwaka 2025. Hali hii imechangiwa na ujenzi wa vyuo vipya pamoja na kuongezeka kwa ufadhili. Hatua hii imewawezesha maelfu ya vijana kupata stadi zinazohitajika sokoni na kupunguza utegemezi.
Uwezeshaji wa kifedha nao umeimarishwa kwa kiwango kikubwa. Rais Samia ameahidi kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya biashara zinazomilikiwa na vijana. Aidha, ameendelea kuthibitisha dhamira yake ya kutoa mikopo ya asilimia 10 bila riba kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, fedha hizi zimewezesha wajasiriamali vijana kupata mitaji, kuanzisha biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.
Hatua nyingine ya kihistoria ni kuanzishwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Vijana. Rais Samia ameanzisha Wizara ya Maendeleo ya Vijana chini ya Ofisi ya Rais, ikiwa ni wizara ya kwanza maalumu kwa ajili ya vijana, inayoongozwa na Waziri Joel Nanauka. Wizara hii inaratibu programu za kitaifa zinazohusiana na stadi, uvumbuzi, utatuzi wa changamoto, utafutaji wa fursa, ufadhili, ushauri na uundaji wa sera rafiki kwa ajili ya vijana. Wizara inalenga kuwezesha zaidi ya kampuni 100,000 zinazoongozwa na vijana katika miaka ijayo, ikiwemo kampuni 20,000 zitakazofanya kazi katika Maeneo Maalumu ya Kiuchumi, kwa lengo la kukuza viwanda, mauzo ya nje na ujasiriamali.
Mikakati hii inaendana kikamilifu na Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, ambayo Rais Samia aliitumia kuomba ridhaa ya wananchi wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu uliopita. Ilani hiyo inalenga kuunda ajira mpya milioni nane ifikapo mwaka 2030, kupanua wigo wa mikopo bila riba kwa vijana, kujenga vituo vya maendeleo ya stadi, pamoja na kuimarisha uwezeshaji wa wajasiriamali vijana katika kuongeza thamani ya bidhaa na mauzo ya nje. Aidha, inasisitiza ukuaji wa uchumi jumuishi, kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka na kuinua makundi maalumu, hususan vijana.
Mwaka huu wa 2026, uongozi wa Rais Samia unaendelea kuweka msingi wa uchumi unaoongozwa na vijana. Kupitia uwekezaji katika elimu, mitaji na mifumo rafiki, serikali inashughulikia changamoto za ukosefu wa ajira huku ikifungua fursa mpya za kiuchumi. Dhamira hii inatoa taswira ya Tanzania yenye ustawi, ambako vijana si watafuta fursa pekee, bali ni waasisi wa fursa na wajenzi wa Taifa imara kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza orodha ya bidhaa na huduma 20 za uchimbaji madini ambazo kuanzia sasa zitatolewa na kampuni zinazomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wazawa, kukuza uchumi wa ndani na kufungua fursa zaidi za ajira kwa wananchi.
Hatua ya kutenga bidhaa na huduma hizo kwa Watanzania inatarajiwa kuimarisha kipato cha wananchi, kuongeza mzunguko wa fedha ndani ya nchi na kuifanya sekta ya madini kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Uamuzi huo unafanywa kupitia Wizara ya Madini, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini.
Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema uamuzi huo pia unafuatia marekebisho ya Kanuni za Local Content za mwaka 2018 na kwamba Sekta ya madini imeendelea kuonesha mchango chanya kwa Watanzania.
Amebainisha kuwa thamani ya manunuzi ya bidhaa na huduma za uchimbaji imefikia shilingi trilioni 5 mwaka 2024, ambapo asilimia 88 ya manunuzi hayo yalifanywa ndani ya nchi.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ajira kwa Watanzania katika sekta ya madini, ambapo kwa sasa asilimia 97 ya wafanyakazi katika migodi ni Watanzania, hatua inayodhihirisha mafanikio ya sera za kuwajengea uwezo wazawa na kuimarisha ushiriki wao kiuchumi.
Waziri Mavunde ametoa wito kwa sekta binafsi, hususan wafanyabiashara na wajasiriamali wa Kitanzania, kuchangamkia fursa hizo kwa kuwekeza katika utoaji wa bidhaa na huduma za madini, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayosaidia wananchi kunufaika moja kwa moja na rasilimali za madini.
Serikali imeahidi kuendelea kuchukua hatua madhubuti za kukuza na kuimarisha sekta ya sanaa nchini kwa kusikiliza sauti za wadau na kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ukuaji wa sekta hiyo na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa Januari 5, 2026 na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, alipokutana na wadau wa sekta ya sanaa katika Ofisi za Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo zilizopo Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, wadau wa sanaa walipata fursa ya kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, kutoa mapendekezo na kueleza matarajio yao kwa Serikali kuhusu namna ya kuimarisha mazingira ya kazi, kulinda maslahi ya wasanii na kukuza mchango wa sanaa katika uchumi wa taifa.
Mhe. Mwinjuma amesema Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa sanaa kwa kusikiliza kero zao na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sera, sheria na miongozo iliyopo ili kuhakikisha sekta hiyo inakua na kunufaisha wasanii pamoja na Taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa kupitia sekta ya sanaa, Serikali inalenga kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana, kukuza uchumi wa ubunifu na kuhakikisha sanaa inatambuliwa kama sekta muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi Afrika Mashariki (EACOP) unaendelea kudhihirisha mchango wake mkubwa katika kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Tanzania, hususan katika kukuza uchumi wa viwanda, kuongeza ajira zaidi ya 12,000, kuimarisha mapato ya Taifa na kuendeleza ushirikiano wa kikanda.
Hayo yameelezwa wakati wa ziara rasmi ya Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa, aliyeko nchini kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bomba hilo la kimkakati linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.
Ziara hiyo imefanyika kwa ushirikiano na mwenyeji wake, Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, aliyesema utekelezaji wa mradi wa EACOP umeendelea kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa Tanzania na Uganda, hususan kupitia ajira, uhamishaji wa ujuzi na fursa za kiuchumi zinazochochea ustawi wa jamii.
Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, hadi sasa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi Afrika Mashariki umefikia asilimia 79 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai 2026.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha Tanzania kuongeza mapato ya Taifa, kuimarisha mchango wa sekta ya nishati katika Pato la Taifa, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa muda mrefu.
Bomba hilo litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 246,000 ya mafuta ghafi kwa siku, hali itakayoongeza ushindani wa kikanda na kuiimarisha Tanzania kama kitovu cha miundombinu ya nishati Afrika Mashariki, sambamba na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu yenye uchumi shindani.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira thabiti, uongozi na ushirikiano mkubwa unaooneshwa katika utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati kwa maendeleo ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema mradi wa EACOP umeleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania na Uganda, na kusisitiza umuhimu wa kuweka utaratibu mahsusi wa kuwatambua, kuwalinda na kuwathamini watumishi pamoja na wataalamu wanaoshiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati.
Mradi huo una urefu wa kilomita 1,443, na kati ya hizo kilomita 296 zipo nchini Uganda na kilomita 1,147 zipo nchini Tanzania ambapo kwa upande wa Tanzania, kutakuwa na jumla ya vituo vinne vya kusukuma mafuta, huku Uganda ikiwa na vituo viwili, na kufanya jumla ya vituo hivyo kuwa sita.