Leo, nimeungana na mwenyeji wangu, Rais wa Jamhuri ya Angola, Mheshimiwa João Manuel Gonçalves Lourenço, kuzindua Hospitali Kuu ya Rufaa ya Rais Julius Nyerere (Hospital dos Queimados Presidente Julius Nyerere) iliyopo Kilamba, jijini Luanda.
Hospitali hiyo imepewa jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa heshima ya mchango wake mkubwa katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, hususan nchi za Kusini mwa Afrika, ikiwemo Angola.
Heshima hii kubwa kwa Taifa letu ni kielelezo cha uhusiano wa kihistoria na urafiki wa kudumu kati ya Tanzania na Angola, uliojengwa katika mshikamano wa kupigania uhuru, na unaoendelea kuimarishwa kupitia ushirikiano wa kiuchumi kwa maendeleo ya watu wetu.
Pongezi za dhati kwako Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mbunge), kwa dhamana uliyopewa na Taifa letu kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Umekabidhiwa jukumu kubwa na muhimu la kuiongoza Serikali, kusimamia utekelezaji wa ahadi zetu kwa wananchi na kuimarisha ustawi wa Taifa letu. Tunakuahidi ushirikiano katika utekelezaji wa kazi hii.
Mwenyezi Mungu akusimamie, akuongoze na kukufanikisha kwa ajili ya Taifa letu na Watanzania wote.
Mungu Ibariki Tanzania.
Alasiri ya leo jijini Dodoma, ambapo kwa baraka za Mwenyezi Mungu, nimehutubia na kufungua rasmi Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kiungio cha Hotuba
Maandishi: https://t.co/s6vSkJW0JA
Video: https://t.co/kiOjleHS4S
Sambamba na mambo mengine, katika hotuba yangu ya kulifungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimevielekeza vyombo vya sheria hasa Ofisi Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwafutia makosa vijana na watoto wetu ambao kwa kutokujua, walifanya makosa kwa kufuata mkumbo Oktoba 29 mwaka huu.
Nikiwa Mama na Mlezi, ninawasihi vijana wote kuendelea kulinda amani na mshikamano wa nchi yetu, na hata siku moja msikubali kushawishiwa kuichoma nchi yenu wenyewe.
Ninawatakia kila la kheri wanafunzi wote 595,816 wa Kidato cha Nne ambao leo mnaanza mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari katika shule za sekondari 5,868 nchini. Idadi hii ya shule inatokana na nyongeza ya shule 305 mpya, ambazo ni mara yake ya kwanza kufanya Mitihani wa Kidato cha Nne. Shule hizi ni matokeo ya kazi tunayoendelea kufanya kuhakikisha kila mtoto wa Tanzania ana uhakika wa kupata elimu bora.
Mwenyezi Mungu Mtukufu aliyewaongoza tangu elimu ya awali hadi leo awajalie utulivu mwifanye na kukamilisha vyema hatua hii muhimu kwenye maisha yenu.
Ninawaombea pia mwendelee kuwa na nidhamu, upendo na bidii katika hatua zinazofuata kwenye maisha yenu. Serikali itaendelea kufanya kila inachoweza kuhakikisha ndoto zenu njema zinapata fursa na nafasi ya kukua na kustawi kwa manufaa yetu sote.
Leo alasiri nimetangaza uteuzi wa Baraza la Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri. Kwa pamoja, tutafanya kazi ya kutekeleza jukumu la msingi la kuwatumikia wananchi.
Dhamana hii ni wajibu na pia deni ambalo tunapaswa kuwalipa wananchi kwa kuwatumikia kwa ari, bidii na uaminifu mkubwa.
Ninawatakia kila la kheri. Mwenyezi Mungu awasimamie na kuwaongoza.
Hotuba yangu mapema leo Ikulu, Dodoma nilipozindua Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Nina imani na uwezo na weledi wa tume hii. Taarifa yao juu ya kiini cha tatizo itatuongoza kujielekeza kwenye hatua sahihi za kiutendaji na mazungumzo ya kuleta maelewano, kuimarisha usalama, amani na umoja wetu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu awasimamie na kuwaongoza.
Leo nimetunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi 296 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kundi la 06/2022 waliohitimu Shahada ya Sayansi ya Kijeshi (BMS) na Kundi la Kawaida la 72/2024 kwa Cheo cha Luteni Usu katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi, Monduli mkoani Arusha.
Ustawi wetu na maendeleo ya nchi yetu vinategemea sana uwepo wa amani, usalama na utulivu ndani na nje ya nchi, kazi ambayo jeshi letu linaifanya kwa mafanikio makubwa. Nguvu kazi hii mpya ya maafisa itaimarisha zaidi uwezo wetu wa kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazoendelea kubadilika.
Ninawapongeza wahitimu wote kwa kukamilisha safari ya mafunzo. Ni imani yangu kuwa mtaendeleza misingi inayolipambanua jeshi letu ya utii, uchapakazi, uhodari, uaminifu na uzalendo.
Mungu Ibariki Tanzania.
Ahsanteni sana Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kama ilivyokuwa kote nilipopita kwa takribani miezi miwili ya mikutano ya kampeni, nimeona upendo, ukarimu, utu, hamasa, shukrani na kiu yenu ya kuendelea kuona matokeo bora zaidi ya kazi ya kuitumikia nchi yetu. Tuendelee kuhamasishana na kukumbushana, ili ifikapo Oktoba 29 sote tujitokeze kwa wingi, tukapige kura kwa amani na utulivu, na tuchague wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kura yako ni Haki yako. Kura yako ya Ndiyo kwa wagombea wa CCM ni kura ya Ndiyo kwa maendeleo, umoja, amani na mshikamano, na kesho iliyo njema zaidi kwa nchi yetu.
Ahsanteni sana. Mwenyezi Mungu awabariki.
Asubuhi ya baraka na shukrani kwa Mwenyezi Mungu, nilipoungana na wananchi wenzangu wa Chamwino kupiga kura.
Tuendelee kujitokeza, kama ambavyo mamilioni ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu wamefanya, na kupiga kura kwa amani na utulivu.
Shukrani kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu mwingi wa rehema kwa siku hii kubwa na muhimu kwangu, kwa Watanzania na kwa Taifa letu, ambapo nimeapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ahsante kwa Watanzania wote kwa imani kubwa kwangu na kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ridhaa ya kuendelea na kazi ya kulitumikia Taifa letu.
Uchaguzi umekamilika na sasa tunarejea kwenye kazi ya kuijenga nchi yetu. Kama ambavyo sote tunafahamu, nguzo muhimu ya mafanikio ya Taifa letu ni amani. Tutaendelea kuweka mkazo katika kudumisha nguzo hii muhimu, na kamwe hatutokuwa na muhali na yeyote atakayejaribu kuivunja, kwani huyo atakuwa si mwenzetu na huo si Utanzania.
Mungu atubariki sote.
Mungu Ibariki Tanzania.