"Binadamu tuna uhuru na mawazo yetu, tuna uhuru na maoni yetu, lakini hatuna uhuru na ndimi zetu. Fikiria unavyoweza, waza unavyopenda lakini sema kwa mahesabu." ~Togolani Mavura.
"Wengi hujua kwa uhakika wasichokitaka, lakini hawana uhakika na wanachokitaka. Ndio hujikuta unavunja chungu kwa madhumuni ya kumtoa nzi aliye ndani yake. Kabla hujahangaika kuondokana na usichokitaka, jiulize kama kwa kuondokana na usichokitaka kunakufanya upate unachokitaka."
"Usifanye kosa la kuruhusu shida ziungane dhidi yako, hakikisha shida haziwi na umoja, zifitinishe, zigonganishe na zichanganye kiasi kwamba badala ya kuhangaika na wewe zihangaishane zenyewe kwa zenyewe ili wewe upate muda wa kufurahia maisha katikati ya shida moja na ingine."
"Iko hatua ya mafanikio katika maisha ambayo inataka uwe mnyenyekevu ili uweze kuiishi. Ikitokea umeifikia kabla hujafaulu mtihani wa unyenyekevu, maisha yatatafuta namna ya kukunyenyekeza yenyewe. Na njia moja ya maisha kukunyenyekeza ni kwa kukupokonya hicho ulichonacho."
"Matarajio yako uliyoweka juu ya watu ndio mtego wa furaha yako na sababu ya kukosa kwako furaha. Usilolitarajia huwezi kulikosa wala haliwezi kukukosesha furaha. Usipokuwa na matarajio juu ya watu huangushwi wala huumizwi." ~Togolani Mavura.
"Ikatokea hamkubaliani jambo na mtu, hakikisha japo muelewane. Kuelewana juu ya msichokubaliana hutoa fursa ya kukubaliana mbeleni kuliko kutoelewana kabisa, au kukubaliana shingo upande. Kuelewana ndio muhimu zaidi kuliko kukubaliana." ~Togolani Mavura.
"Ukitumwa upeleke ujumbe mbaya kwa mtu usiufikishe kama ulivyoupokea. Uchuje uondoe mihemko na hisia ubakishe hoja tu. Binadamu ana hulka ya kutuma ujumbe mkali sana akipitia kwa mtu kuliko akiufikisha mwenyewe usoni kwa mhusika. Ukiufikisha kavukavu utageukwa na aliyekutuma."
"Usitumie nguvu na muda wako kugombana na mtu ambaye huna safari ndefu nae katika maisha yako. Atakupotezea nguvu na muda wa kushughulika na makubwa yajayo mbeleni mwako. Kupuuzia pia ni silaha ya ushindi." ~Togolani Mavura.