Kwa wale wenye kuamini ni muhimu sana kusoma maisha na visa vya wale waliokuwa kabla yetu. Kwa sababu wengi wao walikuwa wameneemeshwa vitu vingi lakini wamebaki historia katika ulimwengu.
Ukimaliza kusoma visa vyao, geukia familia na ukoo wako. Wakumbuke mababu zako walivyokuwa na neema ya mali nyingi (baadhi sio wote), nguvu za miili yao (miamba ilikuwa na wake hadi 9 mtu mmoja).
Watizame wazazi wako, njoo kwako na waangalie vizuri watoto wako utagundua hayakuwa maisha ya Dunia ni chochote zaidi ya starehe ya muda mfupi tu. Hivyo hatuna haja ya kufanyiana ubaya kwa namna yoyote ile kwa sababu kila akifanyacho mwanadamu kina malipo yake.
Kiasi kidogo cha halali chenye amani na uhuru wa kuishi na kuabudu ni bora zaidi kuliko haramu inayokuondolea uhuru huo. Vijana, tuendelee kupambana kwa njia halali; kilichoandikwa, kimeandikwa. Mwisho wa siku, kaburi halina VIP, na maisha ya dunia hayakuwa ila ni pambo la muda mfupi tu.
Mtume Muhammad (SAW) alimwambia mtu:
"Yatumie vizuri mambo matano kabla hayajakupata matano mengine:"
1. Ujana wako kabla ya uzee wako
2. Afya yako kabla ya maradhi yako
3. Utajiri wako kabla ya ufukara wako
4. Wakati wako wa faragha kabla ya shuguli zako
5. Uhai wako kabla ya mauti yako