Official Video Twitter page for @millardayo | We tell the best news and stories from East Africa | from the Most Subscribed to Journalist on YouTube in Africa.
Wafanyabiashara katika Stendi ya Kaloleni, iliyopo Kata ya Mji Mpya, Manispaa ya Morogoro, wamelazimika kufunga baadhi ya Maduka yao wakilalamikia kupungua kwa Wateja, hali inayotokana na daladala kushindwa kuingia ndani ya Stendi hiyo kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria.
Tatizo hilo limebainika kufuatia ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, aliyefika Stendi hapo na kufanya mazungumzo na Wafanyabiashara hao, katika mazungumzo hayo, Kilakala ametoa agizo kwa Madereva wote wa vyombo vya usafiri vinavyotakiwa kutumia Stendi hiyo kuhakikisha wanaacha mara moja tabia ya kushusha na kupakia abiria nje ya eneo rasmi.
Aidha amesema kitendo cha magari kushusha na kupakia abiria nje ya kituo kinasababisha upotevu wa mapato ya Serikali, huku pia kikiwaathiri Wafanyabiashara wanaotegemea Wateja wanaotumia Stendi hiyo.
“Katika Manispaa ya Morogoro kumekuwa na ongezeko la Stendi bubu, hali inayosababisha baadhi ya Madereva kukatisha ruti zao, hii si sahihi; ni lazima magari yote yafuate utaratibu wa kupakia na kushusha abiria ndani ya vituo vilivyopangwa rasmi,” amesema Kilakala.
#MillardAyoUPDATES.
Rais wa Cuba, Miguel Díaz-Canel, amesema Taifa lake liko tayari kupambana endapo Marekani itachukua hatua za Kijeshi, licha ya kusisitiza kuwa hawatamani vita.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa kuadhimisha miaka 65 ya Mapinduzi ya Kisoshalisti, Díaz-Canel amesema hali ya sasa ni ngumu na inahitaji taifa kuwa tayari kukabiliana na vitisho vikubwa, ikiwemo mashambulizi ya kijeshi.
“Hatutaki hali hiyo, lakini ni wajibu wetu kujiandaa ili kuizuia, na ikiwa haitakwepeka, basi tuishinde,” alisema.
Kauli hiyo inakuja wakati mvutano kati ya Cuba na Marekani ukiendelea kuwa juu, huku mgogoro wa nishati ukizidi kuathiri maisha ya kila siku kufuatia vikwazo vya Marekani.
Wakati huo huo, Donald Trump amesema huenda akaivamia Cuba baada ya kumaliza mzozo unaohusisha Iran, akiitaja nchi hiyo kuwa imekuwa ikikumbwa na matatizo kwa muda mrefu.
#MillardAyoUPDATES
Katibu wa Halmashauri Kuu ya NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo Kenani Kihongosi amesema kuwa chama hicho kinaendelea kufanya kazi na Watu wa makundi yote pamoja na Vyama mbalimbali kwa lengo la kuangalia maslahi mapana ya taifa badala ya kujikita katika tofauti za kisiasa
Amesema bado kuna baadhi ya Watu wanaojihusisha na kuomba michango na kuitumia bila kuwekeza katika miradi yenye tija hali ambayo inakwamisha maendeleo na kwamba ni wakati sasa kwao kujifunza umuhimu wa uwekezaji ili kuchangia ukuaji wa uchumi
Kihongosi ametoa kauli hiyo leo Aprili 17 2026 Mkoani Geita alipotembelea mradi wa Kitega uchumi wa chama unaoendelea kujengwa katika eneo la Sabasaba kata ya Kalangalala ambapo amesisitiza kuwa miradi hiyo inalenga kuimarisha uchumi wa chama na kutoa manufaa kwa jamii kwa ujumla
#MillardAyoUPDATES
Mtoto mdogo ameibua hisia na kuvutia maelfu ya Watu baada ya kuonyesha ujasiri wa kipekee kwa kumkimbilia Papa Leo XIV mara baada ya ibada ya Misa nchini Cameroon.
Katika tukio hilo, mtoto huyo ameonekana kuvuka eneo la usalama bila woga na kumfikia Papa, hatua iliyowashangaza walinzi pamoja na waumini waliokuwepo.
Badala ya taharuki, Papa alionekana kumkaribisha kwa utulivu na upendo, akionesha ishara ya ukarimu na kujali, jambo lililowagusa wengi waliokuwa wakishuhudia tukio hilo.
Wengi mitandaoni wamesifu ujasiri wa mtoto huyo, wakieleza kuwa kitendo chake kinaonyesha imani ya dhati na moyo wa kumwamini kiongozi huyo wa dini, huku wengine wakivutiwa na namna Papa alivyolipokea tukio hilo kwa upole na busara.
Tukio hilo sasa limegeuka kuwa gumzo, likitafsiriwa kama picha ya uhusiano wa karibu kati ya viongozi wa dini na waumini wao, hasa watoto.
#MillardAyoUPDATES
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema hana mpango wa kukutana na Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, kufuatia tofauti zao za wazi kuhusu suala la Iran na umiliki wa silaha za Nyuklia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Trump amesisitiza msimamo wake kuwa Iran haipaswi kuruhusiwa kumiliki silaha za Nyuklia, akidai taifa hilo limehusika katika matukio mbalimbali ya vurugu yaliyosababisha vifo vya raia wasio na hatia.
Alipoulizwa kama yuko tayari kukutana na Papa ili kupunguza mvutano huo, Trump alijibu kwa kifupi kuwa haoni umuhimu wa kufanya hivyo kwa sasa.
Hata hivyo, Trump ameeleza kuwa hana uadui binafsi na Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, akibainisha kuwa tofauti yao ni ya kimtazamo kuhusu masuala ya kimataifa, huku akigusia pia kuwa ndugu wa Papa anaunga mkono vuguvugu lake la kisiasa la MAGA (Make America Great Again)
#MillardAyoUDPATES.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Albert Msando amefika katika eneo la Stendi ya Mawasiliano, Ubungo Jijini Dar es salaam ambapo vibanda katika eneo hilo vimeteketea kwa moto hii leo Aprili 4, 2026 ambapo amewapa pole Wahanga waliounguliwa na vibanda vyao na amewaahidi ulinzi wale wote ambao wamefanikiwa kuokoa mali zao.
Akizungumza baada ya kufika katika eneo hilo Msando amesema "Kwa hiyo mimi niwape pole sana kwa niaba ya Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa nimefika hapa kuwapa pole lakini pia kuwashukuru kwa sababu wakati sisi Zimamoto tunafika mzimaji wa moto wa Kwanza ni Mwananchi mwenyewe hii kazi kweli mmeifanya kwa kweli sio ndogo"
"Sasa kwa wale ambao imebidi wahamishe mali zao cha kwanza uzuri Kamanda wa Polisi yuko hapa tutaweka Askari hapa mpaka kukuche asijidanganye mtu kwamba atatokea Mtu adokoe mali ya Mtu, kwa sababu tunawapa Watu wengine kazi na ukishatoa mali yote kwenye duka alafu hukuwa na mahali pakuipeleka mwingine anaweza kupata hasara lakini Jeshi la Polisi litakuwepo hapa mpaka kukuche kulinda mali za watu"
#MillardAyoUPDATES
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amekanusha vikali taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu madai ya Watu kupoteza sehemu zao za siri, akizitaja kuwa ni uzushi usio na msingi wowote wa ukweli.
Akizungumza hii leo, April 04, 2026, Msando amesema hakuna tukio hata moja lililothibitishwa la Mtu kupoteza kiungo chake, na kusisitiza kuwa taarifa hizo zimekuwa zikizua taharuki isiyo ya lazima kwa Wananchi.
Aidha, Msando ameeleza kuwa haiwezekani mtu kupoteza kiungo chake kwa njia zinazodaiwa, kama kushikwa bega au kuguswa tu, akibainisha kuwa madai hayo hayana uhalisia wowote wa kisayansi wala kiusalama, na kuonya kuwa kuendelea kusambaza taarifa hizo kunachochea hofu na kuvuruga utulivu wa jamii, hali ambayo inaweza kuathiri amani na mshikamano wa Wananchi.
Pamoja na hayo, ametoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha linawachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuhusika katika kusambaza au kuzusha taarifa hizo za uongo, iwe ni mitaani au kupitia mitandao ya kijamii, huku akiwataka Wananchi kupuuza taarifa hizo na badala yake kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa utulivu, huku wakizingatia kupokea taarifa sahihi kutoka vyanzo rasmi.
#MillardAyoUPDATES.
Historia imeandikwa timu ya mpira wa kikapu ya Dar City kutokea Tanzania imefuzu kucheza robo fainali ya BAL 2026 kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania.
Dar City licha kufungwa leo kwa vikapu 104-92 dhidi ya Tigers ya Rwanda, Dar City inafuzu kwa kumaliza nafasi ya nne ambayo hata Nairobi City akishinda mechi yake ya mwisho haiwezi kuishusha kutokana na head to head.
Dar City itakuwa Kigali Rwanda kuanzia Mei 22, 2026 hadi Mei 31, 2026 kwa ajili ya robo fainali.
#MillardaAyoUPDATES
Zaidi ya vibanda 500 vya Wafanyabiashara katika soko la Simu 2000 vimeteketea leo kwa moto ambao bado chanzo chake bado hakijajulikana.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto ja Uokoaji Mkoa wa Kinondoni, Jacob Chacha amesema Uchunguzi wa kujua chanzo cha moto huo umeanza.
Pia Mkuu wa Wilaya ya Ubunvo, Albert Msando ametoa maagizo kwa Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua Wafanyabiashara wanaoziba maeneo ya njia katika masoko katika Wilaya ya Ubungo
#MillardAyoUPDATES
Hali ya majonzi, simanzi na vilio imeendelea kutaka kwa Wafanyabiashara wa Soko la Simu 2000 Ubungo, Jijini Dar es Salaam baada ya moto kuteketeza zaidi ya vibanda 500.
@AyoTV_ inakupitisha kujionea hali ilivyo nyakati hii ya usiku baada ya moto huo uliozuka tangu majira ya jioni kudhibitiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambapo tumezungumza na baadhi ya watu walionguliwa Vibanda kupata tathmini ya mali walizofanikiwa kuziokoa.
#MillardAyoUPDATES
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kufuatia ajali ya moto ulioteketeza Soko la Mawasiliano maarufu kama Simu 2000, lililopo katika Kata ya Sinza, Wilaya ya Ubungo, Mkoani Dar es Salaam, jana Aprili 4, 2026. Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko taarifa ya tukio hilo lililosababisha hasara kubwa kwa Wafanyabiashara na Wananchi waliokuwa wakitegemea soko hilo kwa shughuli zao za kila siku.
Katika salamu zake, Rais Samia ametoa pole kwa Wafanyabiashara wote waliopoteza mali zao pamoja na Wananchi wote walioathirika kwa namna mbalimbali kutokana na ajali hiyo. Amesema Serikali iko pamoja na waathirika katika kipindi hiki kigumu, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano na faraja kwa wale waliokumbwa na madhara ya tukio hilo.
Aidha, Rais Samia amesema tayari amezielekeza mamlaka husika kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini chanzo cha moto huo, pamoja na kufanya tathmini ya kina ya madhara na hasara iliyotokea. Pia amesisitiza hatua stahiki zichukuliwe mapema ili kuwasaidia waathirika na kuhakikisha mazingira ya biashara yanarejea katika hali ya kawaida haraka iwezekanavyo.
#MIllardAyoUPDATES.
#PICHA Kutokea Kanisa la ZICC Kariako Visiwani Zanzibar mamia ya Waumini wa Dini ya Kikiristo wamejitokeza kwa wingi kwenye Ibada ya Sikuku ya Pasaka ,Ibada ambayo imeongozwa na Askofu Dickson D. Kaganga.
#MillardAyoUPDATES.
Askofu wa Kanisa la ZICC Karikao Zanzibar, Askofu Dickson D. Kaganga, amewataka Waumini kuacha kuamini imani za kishirikina na badala yake kumwamini Mungu kwa dhati, akisisitiza kuwa imani ya kweli haiendani na hofu ya matukio yanayosambaa mitandaoni kuhusu watu kudai kuibiwa viungo vyao vya siri.
Akizungumza leo April 05, 2026, Visiwani Zanzibar wakati wa maadhimisho ya Pasaka, Askofu Kaganga amesema Mtu anayemwamini Mungu na kumuabudu kwa moyo wa kweli hawezi kukumbwa na matukio hayo, huku akionya kuwa taarifa hizo zimekuwa zikienezwa bila uthibitisho na kuleta hofu isiyo ya lazima kwa jamii.
Aidha, amewasihi Wakristo kusherehekea Pasaka kwa utulivu na maadili mema, na kuongeza kuwa matumizi ya pombe kupita kiasi na anasa, vinaweza kusababisha ajali na matatizo yanayoweza kuepukika.
Katika hatua nyingine, Askofu Kaganga amewataka Waumini kuendelea kulinda amani na mshikamano, ambapo pia ameiomba Serikali kushughulikia changamoto za maadili katika jamii, akibainisha kuwa amesikitishwa na tabia ya baadhi ya watu kusherehekea vifo na kuombeana mabaya mitandaoni.
#MillardAyoUPDATES.
Mwalimu mmoja ametajwa kuuawa kikatili katika Kijiji cha Kilyamatundu, Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, kufuatia tuhuma za imani potofu.
Marehemu, Henry Shubati Myuwanga (50), ambaye alikuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Wema Mkoani Songwe, ameuawa usiku wa kuamkia Aprili 4, 2026 majira ya saa 2:30, baada ya kuvamiwa na Wananchi wenye hasira kali wakimtuhumu kwa imani za kishirikina.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limethibitisha kuwakamata watuhumiwa 25 kuhusiana na tukio hilo, huku msako mkali ukiendelea dhidi ya Kijana mmoja aitwaye Cleuben Simchimba ambaye amekuwa akitafutwa kwa tuhuma za kuanzisha vurugu hizo.
Taarifa zimeeleza kuwa tukio hilo limetokana na kutokuelewana juu ya bei ya sabuni kati ya marehemu na Kijana huyo, ambapo Kijana huyo alipiga kelele akimtuhumu Mwalimu huyo kuwa amemshika na kusababisha kupotea kwa viungo vyake vya siri. Kutokana na madai hayo, Wananchi walikusanyika na kuanza kumshambulia kwa mawe kabla ya kuuchoma moto mwili wake.
#MillardAyoUPDATES.
Wafanyabiashara katika Soko la Mawasiliano maarufu kama Simu 2000, Wilaya ya Ubungo, Jijini Dar es salaam wameiomba Mamlaka ya Wilaya hiyo kuwaruhusu kuanza kufanya usafi pamoja na kurejea kwenye shughuli zao za biashara kufuatia ajali ya moto iliyoteketeza vibanda vyao.
Ombi hilo linakuja siku moja baada ya moto mkubwa kuzuka na kuharibu zaidi ya vibanda 500, tukio lililosababisha hasara kubwa kwa Wafanyabiasha hao na kuwaacha wengi wao wakiwa katika sintofahamu kuhusu hatma ya maisha yao.
Baadhi ya Wafanya waliozungumza na @AyoTV_ wamesema bado wanakabiliwa na maumivu makubwa kutokana na tukio hilo, wakisisitiza kuwa kuchelewa kwa ruhusa ya kuanza usafi na biashara kunaweza kuongeza ugumu wa maisha yao kwa sasa.
#MillardAyoUPDATES
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia Ramadhan Joseph (35) Mkazi wa Misegese Malinyi kwa tuhuma kuhusika na mauji ya mpenzi wake Messe Ngayumgwa baada ya kudaiwa kumkaba koo na kupoteza maisha.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro ACP. Andrew Kantimbo amesema tukio hilo limetokea usiku April 4 mwaka huu 2026 wakati wakiwa baa.
Aidha, amesema Mtuhumiwa alimfuata mpenzi wake ambaye kwa sasa marehemu katika moja ya baa iliyopo Kitongoji cha Kilolelo Kijiji cha Misegese Wilaya ya Malinyi alikokuwa anafanyia kazi kisha kumkaba koo jambo lililopelekea kukosa hewa na kufariki.
#MillardAyoUPDATES.
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe na Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Jokate Mwegelo ( @JokateMwegelo ) ametunukiwa Tuzo ya Heshima ya Uongozi “Honorary Award – Excellent Leadership Icon” katika hafla ya Tuzo za East Africa Youth Awards iliyofanyika Aprili 4, 2026 Jijini Arusha.
Tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Vijana na jamii, ikiwa ni matokeo ya utendaji wake uliotukuka katika nafasi mbalimbali za Uongozi Serikalini.
Jokate ni miongoni mwa Viongozi Vijana waliopitia nyanja tofauti zikiwemo Siasa, Uongozi wa umma na harakati za kijamii, akijijengea taswira ya Kiongozi mwenye maono na anayejali matokeo, hali iliyomfanya kuibuka kinara katika tuzo hizo za East Africa Youth Awards.
#MillardAyoUPDATES.
Jeshi la Polisi nchini limesema mpaka sasa Watu saba wamefariki na wengine kadhaa wamejeruhiwa na wanaendela na matibabu kutokana na kupigwa baada ya kusingiziwa wameondoka na sehemu za siri za Watu hii ni kutoka na uzushi wa imani potofu unaoendelea wa kwamba mtu akiguswa bega sehemu za siri zinatoweka.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa hii leo Aprili 5, 2026 na Msemaji wa Jeshi la Polisi DCP, David Misime imeeleza kwa siku ya jana Aprili 4, 2026 katika mikoa ya Dodoma, Rukwa, Songwe, pamoja na Visiwani Zanzibar Watu kadhaa wamesingiziwa kuondoka na sehemu za Siri za watu na kisha kushambuliwa na silaha za jadi
"Kibaya zaidi pamoja na madhara ambayo yameshashuhudiwa wapo baadhi ya watu wanaoendelea kushabikia pamoja na kusambaza upotoshaji huo katika mitandao ya kijamii na wengine wameamua kuutumia kutengeneza vichekesho na kusambaza kwenye mitandao yao na mingine kwa lengo la kutafuta wafuasi (followers) au kwa malengo mengine wanayo fahamu wao."
"Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa kila mmoja wetu tuendelee kuelimishana kuanzia ngazi ya familia ili kuachana na tabia hizi potofu za kishirikina zinazotuletea madhara makubwa yakiwepo mauaji na fedheha kubwa katika karne hii ya sayansi na teknolojia." imeeleza taarifa ya Polisi.
#MillardAyoUPDATES