"Wale ambao wanakusaidiaga hakikisha siku moja moja bila sababu unawapigia tu simu kuwasalimia sio kuwapigia tu ukiwa na shida mpaka wakiona simu yako wanajua ni ombi linakuja. Wataacha kupokea simu zako." ~Togolani Mavura.
"Kwenye maisha watu wengi hujisahau na kudhani kuwa hakuna mbadala wao. Ila ikifika wakati ukajua kuwa unaweza kutokuwepo na maisha yakaendelea ndio hatua muhimu ya kuelekea kwenye unyenyekevu." ~Togolani Mavura.
"Ukiwa kijana unatakiwa kuzingatia haya;Usiwe na pupa,kuwa mnyenyekevu,jinoe katika stadi walau moja uimudu vizuri,jitolee zaidi ili upate kujifunza zaidi,jenga mtandao,zingatia ibada, jifunze nidhamu ya maisha na pesa na heshimu kanuni ya wakati,wakati wako wa kuchanua utafika."
"Watu waliojiuzulu maisha ni wale wanaoamini wakati wote kuwa kuna mtu mwingine ndio mwenye kuwajibika kwa matatizo yao na si wao wenyewe. Matarajio yao kwa wengine ni makubwa, yasiyotimizika na yanaishia na lawama. Waepuke hao." ~Togolani Mavura.
"Kadri mkwezi anavyokwea mnazi ndio inavyokuwa rahisi zaidi kuchunguliwa utupu wake na walio chini. Vivyo hivyo kadri unavyokwea juu kimaisha ndio faragha zako zinavyokua hatarini zaidi. Ukiwa juu usipojisitiri jiandae kudhalilika." ~Togolani Mavura.
"Stadi na mafunzo mengine katika maisha na kazi zinapatikana kupitia kukosea. Kila unapokwepa kukiri kukosea kwa kujificha kwenye visingizio na lawama kwa wengine, unajinyima fursa ya kujifunza na kutorudia kosa lile lile mbeleni." ~Togolani Mavura.
"Tofauti ya wanaume na wavulana ni hii. Wanaume hutawala akili, hisia na matamanio yao wakati wavulana hutawaliwa nayo. Hiyo ndio tofauti kati ya wanaume na wavulana. Haijalishi umri." ~Togolani Mavura.
"Kabla hujalaumu watu kukutenga jiulize na tafakari ikiwa katika maisha ya watu wewe ni kile kisoda ambacho huwekwa kuisimamisha meza sawasawa isiyumbe au wewe ni ule mguu mfupi wa meza unayeifanya meza icheze?" ~Togolani Mavura.
"Kwenye maisha kuwa pia na yule rafiki katika maisha ambaye hakubishii wala hakufanyi ujisikie mjinga, yeye hukuunga tu mkono. Huyo ni muhimu sana unapokuwa umeshakusanya ujasiri na kukata shauri." ~Togolani Mavura.
"Ukiona unapata tabu sana kutetea au kuhalalisha jambo kwa watu ujue kuwa jambo hilo hata wewe mwenyewe nafsi yako haijashawishika nalo. Litafakari upya au liache kabisa." ~Togolani Mavura.
"Hakuna ujinga mtupu wala upumbavu mtupu. Hata wajinga na wapumbavu nao hufikiri isipokuwa mtiririko wa mawazo yao ndio wa tofauti na ule wa wenye akili. Ukifuatilia mtiririko wa mawazo yao kuna mawili matatu ya maana utayapata." ~Togolani Mavura.
"Wepesi au ugumu wa maisha ya watoto wako baadae unautengeneza kwa jinsi unavyoishi na watu leo. Watasaidiwa au watakamolewa kulingana na ulivyoishi na watu. Kama unaumiza watu leo, hakikisha wanao hawatumii jina lako ili watu wasiwahusishe nawe." ~Togolani Mavura.