Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inafikiria kuja na mkakati maalum utakaowezesha Vijana kutumia vyeti vyao vya uhitimu wa elimu kama dhamana ya kuombea mikopo ili waweze kupata mitaji ya biashara na kukuza uchumi wao.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo April 09,2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha Vijana, Timida Mpoki aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuwainua Vijana kiuchumi na kuwawezesha kuwekeza na kuwaunganisha na fursa mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Waziri Mkuu amesema “Mimi nilipomaliza Chuo Kikuu nilifanya kazi za kubeba zege na kufyatua tofali na Mke wangu akifanya kazi ya Mama lishe kwahiyo najua adha ya Kijana kukosa ajira na Mh. Spika tumeshaanza hata kuongea kwamba Vijana wanapata mikopo wakiwa kwenye masomo, wakimaliza wakapata vyeti vyao vile wanahangaika kupata mikopo kwasababu hawana dhamana”
“Tumeanza kuwaza kupitia maelekezo yale ambayo Mh. Rais aliyaelekeza kutafuta namna ya kuwakwamua Vijana hawa, tumeanza kuwaza kwamba Kijana aweze kutumia cheti chake kile alichohitimu kuweza kukopa, kama kamaliza Famasia aweze kutumia cheti chake kile kukopa aanzishe Pharmacy, kama amemaliza Uhandisi na ana cheti na anahitaji vifaa vya umeme aweze kutumia cheti chake kama dhamana apate mikopo hiyo, jambo hili tutalileta hapa Bungeni tutakapokuwa tumemaliza hiyo sheria ambayo tunataka itengeneze kampuni ya kutoa dhamana lakini pia ya kuweka dhamana mali ambazo zinaweza kuhamishika”
#MillardAyoUPDATES
Baada ya miaka 35, tumelazimika kufanya tena tathmini ya mfumo wa kodi nchini ambapo leo nimepokea ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi Nchini niliyoiunda Julai 2024. Tume imewasilisha mapendekezo 284 yanayolenga kuboresha mfumo wa kodi ili uendane na mabadiliko ya kiuchumi, kiuwekezaji na kibiashara duniani.
Maboresho ndiyo maendeleo. Kwa muktadha huo, tumechukua hatua hii kwa malengo makuu mawili; kwanza, kupanua wigo wa walipakodi, ili kila mwananchi ashiriki kujenga uchumi wa nchi yetu, na pili, kutambua kuwa mfumo bora wa kodi ni muhimu katika kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani, sawa na malengo ya Dira 2050.
Ninawashukuru wananchi wote kwa kutoa maoni kwani mmeshiriki kuamua hatma ya leo na kesho yetu na Taifa letu. Aidha, katika utekelezaji wa mapendekezo hayo, tutashirikiana kikamilifu na sekta binafsi, wananchi na wadau wengine ili tufanikishe lengo la ukusanyaji rasilimali zinazohitajika kwa ustawi wa watu na maendeleo ya nchi yetu.
Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa Watanzania watapewa nafasi kubwa kushiriki katika mradi mkubwa wa gesi asilia iliyosindikwa (LNG) unaotarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa Juni.
Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi amesema Serikali inataka wadau wa ndani kushiriki kikamilifu katika mradi huo ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali za gesi badala ya kuachia nafasi kubwa kwa kampuni za kigeni.
Kwa mujibu wa Serikali, mradi wa LNG wenye thamani ya takribani dola bilioni 42 unatarajiwa kuwa uwekezaji mkubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini na unaweza kuzalisha zaidi ya ajira 100,000.
Naye Prof.Kitila Alexander Mkumbo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji amesema Serikali inaendelea kukamilisha mfumo wa kisheria kwa ajili ya kusaini makubaliano ya mradi huo, huku ikilenga kuhakikisha unatekelezwa kwa manufaa ya taifa.
Aidha, Petroleum Upstream Regulatory Authority (PURA) imehimizwa kuongeza juhudi za utafiti na utafutaji wa maeneo mapya ya mafuta na gesi ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuendeleza sekta ya nishati nchini.
Uwekezaji wa kihistoria wa Shilingi bilioni 700 katika upanuzi wa kiwanda cha Kilombero Sugar siyo tu habari ya takwimu za serikali, bali ni mlango mpya wa fursa kwa vijana wa Kitanzania. Huu ni ubia wa kimkakati kati ya Serikali na mwekezaji unaolenga kuifanya Tanzania ijitosheleze kwa sukari, lakini nyuma yake kuna "mchongo" mkubwa kwa vijana wenye maono.
Akizungumza hivi Februari 24, 2026 mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, amebainisha kuwa uwekezaji huu unakwenda kuwa mwarobaini wa kilio cha muda mrefu cha wakulima wa miwa.
Kwa miaka mingi, wakulima wa miwa Kilombero walikabiliwa na changamoto ya miwa yao "kukaa shambani" na kupoteza ubora kutokana na uwezo mdogo wa kiwanda wa kuchakata mazao hayo.Hivyo uwekezaji huu unamaanisha kiwanda sasa kina "tumbo" kubwa la kutosha kupokea kila bua la muwa linalozalishwa. Hii inahakikisha fedha za mkulima hazipotei na inabadilisha kilimo kutoka cha "kujikimu" kwenda cha "biashara yenye faida".
Wakati Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, ameweka wazi kuwa uwekezaji huu unakwenda kufuta changamoto za muda mrefu za wakulima, Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari, Prof. Kennedy Bengesi, amesisitiza kuwa uwekezaji huoni muhimu kwa sababu unaleta utulivu wa bei ya sukari mtaani na kukuza uchumi wa ndani, jambo linaloongeza mzunguko wa fedha katika eneo husika.
Faida nyingine ya uwekezaji huo unaokuja na mitambo ya kisasa ya uzalishaji ni kwa kijana aliyesomea ufundi (VETA au Vyuo Vikuu), kuingia kwenye mfumo wa uchumi wa viwanda. Kiwanda kitahitaji wahandisi, wataalamu wa mitambo (automation), na wataalamu wa maabara. Hii siyo tu ajira, bali ni nafasi ya kupata utaalamu wa kimataifa (Technical Expertise).
Aidha kama kijana, hana haja ya kuajiriwa kiwandani moja kwa moja anaweza kuingia mkataba kama mkulima mdogo (Outgrower) ukiwa na uhakika wa soko la miwa yake huku akitumia utaalamu wa washauri wa kilimo wa kampuni kuongeza tija ili miwa yake ikubalike kiwandani.
Pia uwekezaji huo unafanya maajabu katika mnyororo mzima wa soko na usafirishaji Kiwanda kikizalisha sukari nyingi, inahitaji kusambazwa nchi nzima na hivyo kutengeneza fursa ya kutoa huduma za malori ya kusafirisha miwa kutoka shambani au kusambaza bidhaa ya mwisho sokoni.
Uwakala na Usambazaji: Vijana wanaweza kuchangamkia fursa za kuwa miongoni mwa wasambazaji wa sukari na bidhaa nyingine zitokanazo na miwa.
Faida nyingine ni ujasiriamali na huduma saidizi kama chakula na malazi yaani kuwapo kwa fursa ya kutoa huduma za kutoa chakula (Catering) kwa wafanyakazi wa kiwandani na ujenzi wa nyumba bora za kupanga;huduma za ufundi kama gereji za matengenezo ya magari hadi huduma za tehama.