"Si kwamba watu wanabadilika, isipokuwa tuliowajua wakati wakiwa katika subra, sio wale halisi tunaokuja kuwajua baada ya kupata kile walichokuwa wakikisubiri. Subra hunyenyekeza!" -Togolani Mavura.
"Maisha ya mwanaume yamejaa masumbuko na mitihani, mwanaume hajui 'baadaye' yake, lolote linaweza kutokea kati ya mlo mmoja na mwingine,heri likutokee likute umeshashiba. Ukikutana na chakula hata kama huna njaa kula tu maana huwezi jua kama utapata fursa ya kukutana nacho tena."
"Utajiri kama ilivyo uongozi ni dhima ambayo inaambatana na wajibu wa kugusa maisha ya wasionacho, wenye uhitaji, na wale ambao rizki zao zinapitishiwa mikononi mwa aliyebarikiwa utajiri. Tajiri ni wakala wa Mwenyezi Mungu wa kusimamia na kusambaza rizki kwa waja wake."
"Aliye juu, mpandie juu,usimngoje chini. Hata akirudi chini, haikufanyi wewe kuhamia juu. Utakuwa umebaki hapo hapo chini ulipoachwa na haitabadilisha ukweli kuwa mwenzako alishapandaga juu. Mwenzako akiwa juu,hamasika,usikasirike. Hasira yako iwe ya kumpandia juu si kumshusha!"
"Hata kama ni mtu mbaya machoni kwako au mwenu, mtu mwenye uwezo wa kifedha ambaye anatabia ya kusaidia wengine si mwenzako. Kadri mnavyomlaani ndivyo wengine wanavyomuombea baraka." ~Togolani Mavura.
"Hata pilipili zikipangwa vizuri huvutia lakini kuvutia kwake hakuondoi muwasho wake. Vivyo hivyo, uongo ukipangwa vizuri huvutia ingawa kuvutia kwake hakuugeuzi uongo kuwa ukweli. Kuwa makini sana na vitu vilivyo katika mpangilio mzuri. Katika mpangilio pia kuna vimeo na vilio."
"Mambo unayoyaona madogo madogo katika maisha ndio mambo yote katika maisha. Ukisema usubirie makubwa yaje, hatujui yatafika lini, na wakati unayasubiria, maisha hayasimami kukusubiria. Furaha ya maisha iko kwenye hayo madogo madogo." ~Togolani Mavura.
"Lile tatizo unaloliahirisha kulitatua leo halikai likakusubiri pale pale. Hukulia denge na kukutangulia mbele ya pale ulipoliacha jana. Ahirisha tu kama unaamini kuwa kesho utakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kulitatua kuliko leo." ~Togolani Mavura.
"Katika umri uliofika,kuna tusi gani jipya kabisa ambalo hujawahi kutukanwa? Kwa nini basi uhamaki? Mwenye nafsi dhaifu hutukana, mwenye kujibu tusi ni dhaifu zaidi. Kuna njia nyingi za kushughulika na mwenye matusi zaidi ya kumjibu." ~Togolani Mavura.
"Wakati mwingine janga linalokufika ndio nusu shari na nusura yako, kabla hujanung'unika na kukufuru hebu jiulize, je isingewezekana kukutokea janga baya au kubwa zaidi ya lililokufika?" ~Togolani Mavura.
"Usitumie nguvu na muda wako kugombana na mtu ambaye huna safari ndefu nae katika maisha yako. Atakupotezea nguvu na muda wa kushughulika na makubwa yajayo mbeleni mwako. Kupuuzia pia ni silaha ya ushindi." ~Togolani Mavura.
"Katika maisha yako kuyaelekea mafanikio, watakaokuwekea vizuizi njiani ni wa kizazi chako na watu wa karibu yako ambao watatafsiri kufanikiwa kwako kama tishio kwao au kielelezo cha kufeli kwao. Ukifanikiwa, usiwakoge. Kuwa mnyenyekevu." ~Togolani Mavura.
"Fanya uwezavyo katika maisha yako na haswa katika watu wako wa karibu uwe na walau mtu mmoja anayeweza kukuuliza maswali magumu, machungu na usiyoyapenda." ~Togolani Mavura.