Habari zilizosambaa kuwa Kijana wa aliyekuwa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ni Wakala wake na kwamba alikuja Nchini kukamilisha dili la Baba yake kuondoka Yanga SC sio za kweli ni za uwongo na za kipuuzi.
Hayo yamesemwa na kocha huyo kupitia Insta story akizipinga vikali na kubainisha kuwa Mwanae ni Mwanafunzi na alikuja Nchini kutoa sapoti kwa Mzazi wake na sio wakala kama inavyosemwa.
Aidha Nabi amefichua kuwa uamuzi wa yeye kuondoka Yanga aliuwasilisha baada ya mechi dhidi ya TP Mazembe na kwamba kwa wakati huo hakuwa na ofa ya Klabu yoyote na kubainisha kuwa hakuwahi kukaa mezani na klabu ya Yanga kuhusu kuongeza mkataba mpya.
“Ningependa kufafanua mambo machache. Uamuzi wangu kuhusu mustakabali wangu na Yanga SC ulichukuliwa na kutangazwa klabuni mara baada ya mechi dhidi ya TP Mazembe. Wakati huo, sikuwa na ofa kutoka kwa klabu nyingine yoyote.”
“Taarifa iliyotolewa na kituo cha redio cha ndani kwamba mwanangu alikuwa wakala wangu na alikuja kukamilisha mpango huo ni ya uwongo na ya kipuuzi kabisa. Mwanangu ni mwanafunzi na mfuasi wa klabu, na alikuja kusaidia timu na baba yake.
“Uwepo wake ulikuwa mdogo tu kwa sababu hizi mbili, kusaidia timu na baba yake. Pia ningependa kusema kwamba sikuwahi kukaa na klabu kujadili uwezekano wa kuongeza mkataba, kwa sababu klabu tayari ilijua uamuzi wangu miezi iliyopita.
“Nimehuzunika kama mashabiki wetu wote wapendwa kufikia mwisho wa ushirikiano wangu na klabu.
“Kwa kujiheshimu, ningewaomba muiache familia yangu, haswa mwanangu, ambaye hana uhusiano wowote na maamuzi yangu ya kitaaluma” - Nasreddine Nabi.
#KitengeSports