Roho ni mgeni haidumu duniani.
Maana yake: Roho ya binadamu ni kama mgeni, haidumu mara huondoka/ akafa.
Matumizi: Inatukumbusha binadamu hana wakati mrefu wa kuishi ulimwenguni.
Riziki ya yule si ya huyu.
Maana yake: Riziki au bahati ya mtu mmoja haiwezi kuwa sawa na ya mtu mwingine.
Matumizi: Inatukumbusha kuwa kila binadamu ana riziki anayojaliwa na mungu. Haifai kuona wivu kutokana na riziki ya mtu mwingine.
Riziki kama ajali, huitambui ijapo.
Maana yake: Mtu haitambui riziki imjiapo ghafla kama ajali itokeavyo.
Matumizi: Hutumiwa kupigia mfano bahati nzuri au neema iliyomjia mtu bila kuitarajia.
Mtu ni watu.
Maana yake: Hakuna mtu anayeweza kuishi peke yake pasi na kuingiliana na watu wengine.
Matumizi: Hutumiwa kumzindua mtu anayedhani anajitosheleza/anajiweza kutokana na hali aliyo nayo na hatangamani na wenzake.
Uso wa kufadhiliwa u chini.
Maana yake: Uso wa mtu anayefanyiwa fadhila au hisani huinamia chini, hawezi kumkabili mfadhili wake.
Matumizi: Tunapotendewa fadhila/hisani na mtu fulani huwa tu kama watumwa wake, hatuna uhuru.
Dua mbaya haiombolezewi mwana.
Maana yake: Maneno mabaya hayatumiwi kwa mtoto anayelelewa.
Matumizi:Hutumiwa kumzindua mtu anayeelekea kuwa na tabia ya kutumia lugha chafu mbele ya watoto kumkanya kuwa huenda akawazoeza mabaya.
Mema na maovu ndiyo Ulimwengu.
Maana yake: Mema na mabaya ni sehemu ya maisha Ulimwenguni.
Matumizi: Inatukumbusha kuwa maisha yamejaa mema na mabaya, yanapokuja basi tunapaswa kuyakubali na kupambana nayo.
Mchama ago hanyele huenda akauya hapo.
Mchama ni anayeondoka/anayeacha. Ago ni kambi. Nyele ni kujisaidia na Uya ni kurudi.
Mtu anayeihama kambi hajisaidii hapo huenda akarudi hapo.
Kumnasihi mtu anayetaka kuharibu/kuangamiza kitu kilicho mfaa kwa kuwa huenda akakihitaji.
Zingwizingwi lipe nguo ulione.
Maana yake: Zingwizingwi ni jitu pumbavu au lisilotumia akili. Mjinga ukimpa nguo atatembea kwa maringo/majivuno kuonesha wengine.
Matumizi: Hutumiwa kwa mtu aliyekuwa duni kisha akapata cheo/ madaraka na akaanza kuwa na maringo.
Ogopa ni ngao pia.
Maana yake: Kuogopa ni kama ngao kwa kuwa mtu anajiepusha na taabu.
Matumizi: Inatukumbusha watu kuwa woga huweza kumfaa mtu wakati mwingine aiepuke balaa/taabu.
Maskini wa mali yuko, Maskini wa jambo hakuna.
Maana yake: Wapo maskini wasiokuwa na chochote lakini hakuna mtu asiyekuwa na jambo/kitu akijuacho.
Matumizi: Inatukumbusha inawezekana mtu akawa maskini wa mali lakini analo jambo analolijua ambalo mwenye mali halijui.
Aliyekupa wewe kiti ndiye aliyenipa kumbi.
Maana yake: Kumbi ni ganda la nje la nazi. Mungu aliyekupa kiti ulicho nacho ndiye huyo aliyenipa kumbi.
Matumizi: Waliojaliwa na hali nzuri hawapaswi kuwadharau wadhaifu na wenye hali duni. Mwenye uwezo wa haya yote ni Mungu.
Mke ni nguo, mgomba ni kupalilia.
Maana yake: Mke lazima avishwe vizuri ili avutie kama mgomba unavyopendeza baada ya kupaliliwa.
Matumizi: Hutunasihi kuwa hakuna kitu kinachoweza kuvutia kama hakijashughulikiwa kwa juhudi na mhusika.
Zinguo la mtukutu ni ufito/Ufito funzo la mtukutu.
Maana yake: Zinguo ni kisomo cha kumwombea mtu Mwenyezi Mungu amwepushe na balaa.
Ufito ni kiboko/ mchapo.
Mtukutu ni mtundu au asiyesikia.
Matumizi: Tusichelewe kuwaadhibu au kuwatia adabu wahalifu/watoto watukutu.
Hujafa hujaumbika.
Maana yake: Binadamu anaendelea kuumbika akiwa bado anaishi/hai. Mungu anaweza kumpa kilema au wasifu mwingine.
Matumizi: Inatukanya dhidi ya kuwacheka/ kudharau wengine haswa wenye ulemavu kwa kuwa tunaweza fikwa na ulemavu huo mradi bado tunaishi.
1. Family time is finite—cherish it.
2. Children time is precious—be present.
3. Friend time is limited—prioritize the real friends.
4. Partner time is meaningful—never settle.
5. Coworker time is significant—find energy.
6. Alone time is abundant—love yourself.
Adui aangukapo mnyanyue.
Maana yake: Adui akianguka ni vizuri kumsaidia kunyanyuka/kuamka.
Matumizi: Inatukanya dhidi ya kuwa na uadui au kuwekeana kisasi. Tuwatendee mema watutendeao mabaya.