Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mama yetu, Mama Fatma Karume, mjane wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kilichotokeo leo tarehe 21 Septemba, 2026.
Kifo chake ni pengo kwa familia na Taifa kwa ujumla, kwani alikuwa sehemu muhimu ya historia adhimu ya Zanzibar kuanzia wakati wa harakati za kupigania uhuru, Mapinduzi Matufuku ya Zanzibar na kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Daima tutaendelea kukumbuka, kuenzi na kuheshimu mchango wake katika kuhifadhi kumbukumbu na urithi wetu, pamoja na kuchochea maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya Taifa letu.
Ninatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Amani Abeid Karume, familia ya Hayati Sheikh Karume, ndugu, jamaa, marafiki, wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote. Ninawaombea Mwenyezi Mungu awajalie subra, faraja na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un.
Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 12 (mahabusu saba na Askari Polisi watano), vilivyotokea leo katika Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida, kufuatia ajali iliyohusisha gari la Jeshi la Polisi na lori.
Ninatoa pole kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Halima Omary Dendego, familia za marehemu, ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa msiba huu.
Ninaendelea kuwasisitiza madereva wote kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani na kuhakikisha vyombo vya moto vinakuwa katika hali nzuri na salama kabla ya kutumika, ili kulinda maisha ya wananchi na watumiaji wengine wa barabara.
Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahala pema peponi. Amina.
Naitakia kila la kheri Timu yetu ya Taifa ya Wanawake chini ya Miaka 20 (Tanzanite Queens) inapoanza safari ya kulitumikia na kuliheshimisha Taifa letu katika mashindano ya Kombe la Dunia la 2026 yanayoanza leo nchini Poland.
Ushiriki wenu katika mashindano hayo makubwa duniani ni heshima na fahari kubwa kwa nchi yetu. Aidha, ni uthibitisho wa uwezo, vipaji na juhudi za mabinti zenu, na pia ni chachu ya kuhamasisha na kukuza ushiriki wa wanawake katika michezo.
Tunawatakia kila la kheri. Taifa lenu lipo pamoja nanyi.
Lusaka, Zambia
Leo nimeshiriki sherehe za uapisho wa Mheshimiwa Hakainde Hichilema kuwa Rais wa Jamhuri ya Zambia.
Kwa mara nyingine, ninampongeza Mheshimiwa Hichilema kwa kuaminiwa tena na wananchi wa Zambia.
Ninawahakikishia ndugu zetu wa Zambia kuwa Tanzania itaendelea kuthamini na kuimarisha uhusiano wetu wa kidugu, wa kihistoria na kimkakati, kwa manufaa ya nchi zetu mbili.
Ikulu, jijini Dar es Salaam, baada ya kazi nimepata wasaa wa kukutana, kuzungumza na kuwaaga wanafunzi 44 wanaonufaika na Ufadhili wa Samia Scholarship Extended katika Sayansi ya Data, Akili Unde (Artificial Intelligence) na Sayansi Shirikishi, wanaokwenda masomoni nchini Ireland na Urusi.
Katika nasaha zangu kwao, nimewakumbusha ujumbe wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kuwa wale wenye bahati ya kupata elimu wana wajibu wa kulipa jasho ambalo wengine wamejitolea ili wao wasome. Ni sawa na mtu aliyepewa chakula chote cha kijiji ili apate nguvu za kwenda mbali kuwaletea nduguze chakula.
Ninawatakia kila la kheri.
Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), Rufiji, Pwani
Shukrani kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwezesha kushuhudia tukio hili la kihistoria kwa Taifa letu. Hii ni hatua ya kujivunia katika safari yetu ya kuendelea kufanya kazi ya kujikomboa kiuchumi, ili kuiishi maana halisi ya Uhuru wetu, pamoja na malengo na ndoto za waasisi wetu.
Hongera kwa kila Mtanzania.
@SuluhuSamia@kwamekivaisi Hongera sana Mh. Rais, Mungu aendelee kukupa afya njema uendelee kututumikia. Hakika uongozi wako unaweka alama chanya sana kwa ustawi na maendeleo ya Taifa letu
Leo ni siku kubwa na ya kihistoria kwa nchi yetu ambapo nimezindua Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), hatua inayotimiza maono ya zaidi ya miaka 50 ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ya kuzalisha umeme katika Mto Rufiji ili kuchochea maendeleo yetu. Ninawashukuru watangulizi wangu, viongozi na watendaji wa Wizara na taasisi mbalimbali, pamoja na wananchi, kwa mchango wao mkubwa katika kukamilisha safari hii.
JNHPP ni kielelezo cha uwezo wetu wa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, pia ni ushahidi kuwa nchi za Afrika zikishirikiana zinaweza kufanikisha mambo makubwa yenye maslahi kwa watu wetu. Pamoja na manufaa mengine, mradi huu umeongeza uwezo wetu wa kuzalisha umeme hadi megawati 4,646, hivyo kutuhakikishia umeme wa uhakika nchini na ziada ambayo tutaiuza kwa nchi jirani, pia umetoa ajira kwa maelfu ya vijana wetu na kuwapa ujuzi na uzoefu.
Ninawasihi Watanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na mradi huu, kutunza mazingira, hasa vyanzo vya maji, pamoja na kulinda miundombinu yake ili udumu na kuhudumia vizazi vijavyo. Aidha, nimeielekeza Wizara ya Nishati kuongeza kasi katika ujenzi wa njia za kusafirisha na kusambaza umeme, ili wananchi waone tija ya uwekezaji huu kwenye maisha yao na maendeleo ya Taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania.
Ninampongeza Hawa Wanyeche, mchezaji wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, kwa kutwaa ubingwa wa Uganda Ladies Open, mashindano yaliyokutanisha wachezaji kutoka Ghana, Japan, Kenya, Nigeria, Rwanda, Tanzania na Uganda.
Ushindi huu ni fahari kubwa kwa Taifa letu na unaonesha uwezo wa wachezaji wetu kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Serikali itaendelea kuimarisha na kuendeleza michezo nchini kwa kuweka mazingira bora kwa wanamichezo wote, pamoja na kuwawezesha kushiriki na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Kusini Unguja, Zanzibar
Leo nimehitimisha Tamasha la Kizimkazi 2026, baada ya siku tatu za shangwe, fursa na shughuli mbalimbali zilizolenga kujenga umoja, kukuza fursa za biashara na uwekezaji, kutangaza utamaduni na utalii wetu, pamoja na kufungua miradi ya maendeleo kwa wananchi. Tunatarajia matokeo ya shughuli hizi kuendelea kuonekana hata baada ya tamasha kumalizika.
Ninawashukuru wote walioshiriki na kufanikisha tamasha hili. Ninawasihi tuendelee kushikamana, tudumishe amani, utulivu na usalama wa nchi yetu, kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wetu.
Mapema leo nimeungana na wakazi wa mkoa wa Kusini Unguja, ambapo nimeweka jiwe la msingi la ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Amali, kuzindua mradi wa maji na kukagua maboresho ya Kituo cha Afya Kizimkazi, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra kuelekea kilele cha Tamasha la Kizimkazi mwaka 2026.
Uwekezaji huu unalenga kuchochea ustawi na maendeleo ya jamii kwa kuhakikisha huduma za msingi zinakuwa bora, nafuu na za uhakika wakati wote. Uwekezaji huu ambao unaendelea kufanyika katika kila kona ya nchi yetu, unatutaka sote kutimiza wajibu wa kuitunza na kuilinda miundombinu hii ili iendelee kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.
Kuelekea Tamasha la Kizimkazi 2026, leo nimezindua Viwanja vya Kufurahishia Watoto vya Kizimkazi, vyenye uwezo wa kuhudumia watoto 500 kwa wakati mmoja. Nawashukuru wote walioshiriki kukamilisha mradi huu unaoweka mazingira salama kwa watoto kujifunza, kucheza na kukua.
Michezo ni sehemu muhimu ya malezi na makuzi ya watoto, kwani huwajengea uwezo wa kushirikiana, nidhamu, ubunifu na tabia njema, huku wakikuza vipaji na uwezo wao wa kiakili.
Wahenga walisema, “Watoto ni Taifa la Kesho.” Kadiri tunavyowekeza kwa watoto, ndivyo tunavyojenga Taifa lenye usalama, ustawi na maendeleo endelevu. Nimeelekeza viwanja hivi vitunzwe na vitumike kwa ajili ya watoto pekee. Aidha, ni muhimu tufahamu kuwa urithi mkubwa zaidi tunaoweza kuwaachia watoto wetu ni Taifa salama, lenye amani na umoja, litakalowawezesha kustawi na kutimiza ndoto zao.
Ninawapongeza Klabu ya Simba kwa tamasha lililofana la Simba Day 2026, lililoambatana na maadhimisho ya kutimiza miaka 90. Ninawatakia kila la kheri katika msimu ujao wa Ligi Kuu.
Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2025 inaielekeza Serikali kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) ili kuwezesha wananchi kufika kwa urahisi na kwa haraka kwenye makazi, biashara na huduma muhimu. Nina furaha kuona tunatekeleza ahadi hiyo ambapo leo nimezindua Awamu ya Pili ya BRT katika barabara za Kilwa, Chang’ombe, Sokoine na Kawawa jijini Dar es Salaam.
Mradi huu umeanza kuleta matokeo chanya kwa kupunguza muda wa safari kutoka zaidi ya saa moja hadi takribani dakika 30, kupunguza msongamano wa abiria na magari, pamoja na kuongeza fursa za ajira, hususan kwa vijana. Azma yetu ni kukamilisha awamu zilizobaki ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hii.
Ili kuhakikisha miradi hii inakuwa na manufaa ya kudumu, nimetoa maelekezo yafuatayo:
1. Wizara Ujenzi, TAMISEMI na mamlaka zinazohusika ziimarishe usimamizi wa miradi yote ili ikamilike kwa wakati na itoe huduma kwa wananchi.
2. Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) uongeze mabasi kulingana na mahitaji halisi ya abiria.
3. Wananchi watunze miundombinu inayojengwa ili idumu.
4. Wizara ya Ardhi na mamlaka za serikali za mitaa zitenge mapema na kulinda maeneo yatakayojengwa miundombinu.