Hapa duniani, umiza watu, chafua watu, wafitinishe, watoe machozi, vunja familia za watu, waondolee watu furaha utakavyo, ila Kuna siku kabla hujafumba macho kuiaga dunia. Allah atakuletea matukio si moyo wako tu Bali mpaka maini, figo, bandama vitatikisika. KARMA✍️
Uko hapo ulipo, pazuri au pabaya sababu ama kuna mtu alikuwahi huko nyuma akakuambia ukweli uliokusaidia, ama hakukuambia ukweli kwa wakati sahihi, au alikuambia ukweli ambao ungekusaidia lakini ukaupuuza. Kesho yetu inaumbwa na ukweli au uongo tuliouamini na kuaminishwa jana.
Nimejifunza kuwa ipo tofauti ya upendo na mapenzi na mapenzi na ndoa. Ana heri ambaye vitatu hivi vimekutana pamoja. Ikitokea vimegoma kukaa pamoja, basi chagua upendo. Upendo ndio gundi ya kugandisha hivyo vingine viwili pamoja au na kimojawapo. Bila upendo ni bure.
Aliye juu, mpandie juu,usimngoje chini. Hata akirudi chini, haikufanyi wewe kuhamia juu. Utakuwa umebaki hapo hapo chini ulipoachwa na haitabadilisha ukweli kuwa mwenzako alishapandaga juu. Mwenzako akiwa juu,hamasika,usikasirike. Hasira yako iwe ya kumpandia juu si kumshusha!
Mahangaiko ndio maisha ya mwanadamu tofauti ni tunachohangaikia na kuhangaishwa nacho. Kila mtu ana mahangaiko yake.Madogo yake, makubwa kwako.Makubwa yake, madogo kwako.Ukitaka kuishi vizuri na watu, usiyadogoshe mahangaiko yao.Heshimu mahangaiko ya kila mtu.
Mambo unayoyaona madogo madogo katika maisha ndio mambo yote katika maisha. Ukisema usubirie makubwa yaje, hatujui yatafika lini, na wakati unayasubiria, maisha hayasimami kukusubiria. Furaha ya maisha iko kwenye hayo madogo madogo.
Lile tatizo unaloliahirisha kulitatua leo halikai likakusubiri pale pale. Hukulia denge na kukutangulia mbele ya pale ulipoliacha jana. Ahirisha tu kama unaamini kuwa kesho utakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kulitatua kuliko leo.
Katika umri uliofika,kuna tusi gani jipya kabisa ambalo hujawahi kutukanwa? Kwa nini basi uhamaki? Mwenye nafsi dhaifu hutukana, mwenye kujibu tusi ni dhaifu zaidi. Kuna njia nyingi za kushughulika na mwenye matusi zaidi ya kumjibu.
Katika safari kuna wanaosafiri, wanaosafirisha wasafiri, wasindikizaji na wapagazi. Ndivyo ilivyo katika safari ya maisha. Tambua nafasi yako na nafasi za watu wengine katika safari ya maisha yako.Tambua pia nafasi yako katika safari za maisha ya watu wengine.
Hata kama unamjua Mkubwa mahala, usiwadharau wale wadogo chini yake, maana hao waweza kuwepo muda mrefu kushinda huyo mkubwa, na pia, katika udogo wao, wana nafasi kubwa ya kukwamisha jambo lako kukuonyesha tu nafasi yao.