VIDEO:
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja, Idrisa, amenusurika kifo baada ya kuungua moto ndani ya chumba alichohifadhiwa kufuatia tuhuma za kuiba mafuta ya petrol yanayotumika kwenye vyombo vya uvuvi katika soko la samaki Sahare, eneo la Kasera mkoani Tanga, huku chanzo cha moto kikidaiwa kuwa ni mabaki ya mafuta yaliyokuwepo ndani ya chumba hicho.
Wakizungumza na vyombo vya habari leo, mashuhuda wa tukio hilo wamesema mtu huyo anafahamika katika eneo hilo na amekuwa akijihusisha na shughuli za uvuvi, hali iliyowashangaza wengi kumuona akituhumiwa kuhusika na tukio hilo.
Kwa upande wake, Afisa Habari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji jijini Tanga, Alfani Mhina, akithibitisha kutokea kwa tukio hilo amesema walipokea taarifa kwa wakati na kufika eneo la tukio ambapo walifanikiwa kufanya uokoaji.
Hata hivyo, Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Halidi Rashidi, amesema soko hilo limekuwa na mchango mkubwa katika kukuza mapato ya Halmashauri, huku akiahidi kuwa watajipanga kulirejesha katika hali ya kawaida baada ya athari za tukio hilo.