Na mwisho wa dua yangu, Hapa niloibakisha.
Nakuomba mola wangu, Japo linahuzunisha.
Wahifadhi ndugu zangu, Uwape ya kuridhisha.
Nirahamu ya rahimu, Siku ya kunyoka kwangu.
Wafikapo kaburini, Chini wanaponishusha.
Kwenye wangu mwana ndani, Mwili wakiufikisha.
Ruhuma yako dayani, Nilipo kuiegesha.
Nirahamu ya rahimu, Siku ya kunyoka kwangu.
Wasimamapo kwa safu, Mikono wakifungisha.
Zitakabali Latifu, Dua wakiwasilisha.
Ili nilonao khofu, Uweze kuiepusha.
Nirahamu ya rahimu, Siku ya kunyoka kwangu.
Sitopenda kuwaliza, Ila mda umekwisha.
Likiwasili jeneza, Ndani wakinipitisha.
Wape subira muweza, Nyuma nilowabakisha.
Nirahamu ya rahimu, Siku ya kunyoka kwangu.
Wape moyo ya manani, Sanda wanaponivisha.
Mda wa kunikafini, Chozi wakitiririsha.
Wape imani ya dini, Wajuwe ndio maisha.
Nirahamu ya rahimu, Siku ya kunyoka kwangu.