Mjane mwenye umri wa miaka 83, Evelyn Chiomba, amefungua kesi katika Mahakama Kuu akimpinga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kufuatia hatua ya kutolewa kwenye nyumba anayoidai kuishi tangu mwaka 1978 katika eneo la Regent Estate jijini Dar es Salaam.
Shauri hilo limesikilizwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Anorld Kirekiano ambapo Mahakama imeamua kusimamisha kwa muda utekelezaji wa amri iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ya kumuondoa mjane huyo kwenye nyumba hiyo na kumtaka arudi na kuendelea kuishi hapo hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Akizungumza mara baada ya kutoka mahakamani, Wakili wa mwombaji,Fernand Makore amesema mama huyo aliamua kufungua shauri hilo baada ya Mkuu wa Mkoa kutoa maelekezo ya kuondolewa kwa nguvu kwenye nyumba hiyo kufuatia taarifa ya kamati ya uchunguzi iliyodai kuwa nyumba hiyo si mali yake.
"Baada ya kamati ya uchunguzi kufanya uchunguzi ikapeleka taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa kwamba wamejiridhisha kwamba nyumba hiyo si mali ya Bibi Evelyn Chiomba kwa maana hiyo Mkuu wa Mkoa akatoa maagizo au amri ya kwamba kuanzia Mei 6, 2026 mama huyo anatakiwa aondolewe kwa nguvu na mabavu chini ya usimamizi wa Askari Polisi na mabaunsa na watu wengine wakaenda kutekeleza amri hiyo ya kumuondoa," amesema.
Wakili Makore amedai kuwa mlalamikaji ameomba Mahakama kutoa tafsiri ya kisheria kuhusu iwapo Mkuu wa Mkoa ana mamlaka ya kushughulikia migogoro ya ardhi na kutoa maamuzi kuhusu umiliki wa nyumba inayobishaniwa.
Amesema upande wa mlalamikaji uliomba pia amri ya muda ya kusimamisha utekelezaji wa agizo hilo ili mama huyo aweze kurejea nyumbani kwake wakati akisubiri usikilizwaji wa shauri la msingi.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama imeamua kuiweka pembeni kwa muda amri ya Mkuu wa Mkoa na kuagiza mjane huyo arejee katika nyumba hiyo hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.
"Jaji baada ya kusikiliza pande zote mbili mahakama imeamua yafuatayo kwamba wakati tunasubilia usikilizwaji wa shauri hili ameiweka pembeni amri ya Mkuu wa Mkoa na kumtaka bibi huyu arudi kwenye nyumba yake wakati akisubilia maombi yake kusikilizwa," amesema.
Aidha Mahakama imeielekeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha viapo vya majibu ndani ya siku 14.huku usikilizwaji wa kesi ya msingi ukitarajiwa kuendelea Mei 29, 2026.
Angalia hii video kwa makini uone jinsi Polisi wanavouwa Ndugu zetu.
Kumbe walizima data na umeme ili wafanye huu ukatili gizani walidhan itakuwa siri.