NI WAKATI GANI ASKARI ANAWEZA KUNGÓA ALAMA ZA UTAMBULISHO (mf. Number Plate) KWENYE GARI? NA NI ASKARI YUPI NA KATIKA MAZINGIRA GANI?
Kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani yaani The ROAD TRAFFIC ACT, askari aliyepewa mamlaka ya moja kwa moja ya kuondoa alama za utambulisho wa gari, katika mazingira ya kawaida ni Askari Mkaguzi wa Magari (Vehicle Inspector-VI)
Nasema mazingira ya kawaida, ukiacha mazingira maalumu kwa mfano pale ambapo gari limetelekezwa, haliwezi kuvutwa mara moja na askari wanataka mwenye gari ajitokeze.
Vehicle Inspector amepewa mamlaka haya kwa mujibu wa kifungu cha 97(2) cha sheria baada ya kujiridhisha kuwa gari hilo halifai kwa matumizi yaliyokusudiwa barabarani au ni hatari kwa matumizi jinsi lilivyo. Madhara ya kisheria (legal effect) ya kuondoa namba za utambulisho, ndio kusema gari lako au chombo husika hakifai kwa matumizi.
Hii ndio tafsiri hasa. Sheria haitaji mazingira mengine ya kuondoa namba kama vile kudaiwa faini, wrong parking, kubishana na askari, au sijui kutokuwa na bima.
Kwani kumbuka sheria hiyo hiyo RTA inataka kila gari litembee na namba za utambulisho. Kutembea bila namba za utambulisho ni kosa kisheria.
Hivyo hata wewe mwenye gari huruhusiwi kuondoa alama za utambulisho kwenye gari lako.
Alama za utambulisho ni pamoja na namba, rangi na aina ya gari.
Mamlaka ya Vehicle Inspector Kukagua magari
Mamlaka ya mkaguzi wa magari (VI) kukagua magari yapo kwa mujibu wa kifungu cha 97 cha sheria ya usalama barabarani.
Kwa mujibu wa kifungu hiki, Mkaguzi wa magari baada ya kulikagua gari au tela anaweza:
(a) Kuthibitisha kuwa gari hilo linafaa kwa matumizi kwa jinsi linavyotumika na atatoa cheti cha uthibitisho (certificate of fitness)
(b) anaweza kutoa kibali gari liendeshwe au kuvutwa kwenda karakana ili litengenezwe na baadae lirudishwe kwake kwaajili ya ukaguzi baada ya matengenezo kukamilika_
(c) anaweza kutamka kwa kuhitimisha kuwa gari hilo halifai kwa matumizi ambayo lilisajiliwa nayo
Mamlaka ya kuondoa alama za utambulisho
Kwa mujibu wa kifungu cha 97(2) ikiwa gari litatamkwa kuwa halifai kwa matumizi au ni hatari kwa matumizi hadi lirekebishwe, basi mkaguzi wa magari ataondoa alama za utambulisho na kuzirudisha kwa msajili, ambaye ataamua au alifutie usajili au kusimamisha usajili hadi pale atakapothibitishiwa na mkaguzi wa magari kwamba gari hilo sasa linafaa kwa matumizi.
Askari Mwingine asiye VI baada ya kukagua gari anatakiwa kuchukua hatua gani?
Iwapo askari atakuwa amekagua gari alilolishuku barabarani kwa mujibu wa kif.95(d), iwapo ukaguzi wake utadhihirisha kwamba gari au tela hilo halifai au ni hatari kwa mtu yeyote au lina mzigo mkubwa zaidi ya unaotakiwa kubebwa, anaweza kufanya mojawapo ya yafuatayo:
(i) Iwapo ataona ni salama, na kwa kuzingatia uwezo wa gari kutembelea lenyewe, ataamuru liende katika kituo cha polisi cha karibu au mahali alipo mkaguzi wa magari, kutegemea na lipi ni rahisi zaidi
(ii) Iwapo ataona gari limezidisha mzigo au mzigo haujafungwa kwa usalama, anaweza kuamuru gari liende katika kituo cha mzani kilicho karibu ili lipimwe au akaamuru mzigo ufungwe vizuri kwa usalama kabla gari halijaondoka
(iii) Iwapo ataona sio salama kwa gari hilo kutembea kwa nguvu zake lenyewe, ataamuru gari hilo livutwe hadi kituo cha karibu cha polisi au mahali alipo mkaguzi wa magari, kulingana na lipi ni rahisi kati ya hayo mawili
RSAadmin1
RSA TANZANIA
Usalama Barabarani ni Jukumu Letu Sote.