Ukiaminiwa kuzijua aibu za mtu umebebeshwa mzigo mzito.Kuaminiwa ni kula kiapo cha utii.
Hata mkigombana na mtu aliyekuamini, unawajibika kumsitiri na kuheshimu faragha yake.
Ikiwa unajua huna kifua cha kumstahi mtu na aibu zake epuka kufahamu mambo yake ya ndani.
Kama kuna kiashiria kimoja kizuri cha ukomavu wako kihisia ni uwezo wa kumsikiliza mtu hasa yule usiyejua hulazimiki kumsikiliza. Ukomavu huo unakuchochea kutamani kuelewa ‘ulimwengu’ wa mwenzako—anafikiri nini, anaona nini, anaamini nini, anataka kufanya nini—bila kuteka uzoefu wake wala simulizi lake na kulipima kwa mizania ya misimamo na matarajio yako.
Usikivu wako unapimika vizuri kwa namna unavyoweza kusikia kisichoweza kusemwa kwa maneno. Unasikiliza sauti inayobeba hisia zilizo nyuma ya maneno anayochagua mwenzako. Unasikiliza ujumbe unaobebwa na uso wa mtu. Unasikiliza kuelewa maana ya kimya cha mtu bila kumhukumu na kumshinikiza kukuamini. Unasikiliza kuelewa kinachomgusa zaidi, kinachobeba matumaini yake, kinachomtia ujasiri, kinachobeba fahari yake na kumfanya ajione muhimu miongoni mwa binadamu wenzake.
Kadhalika, usikivu wako huambatana na ule upendo wa dhati unaojaribu kuuelewa woga wa mwenzako, kuelewa ilikojificha aibu yake, ukurasa upi wa maisha yake asingependa kuusoma kwa sauti na kubaini swali lipi asingependa uulize maana linaweza kutibua unyonge na hisia za kushindwa. Unasikiliza kinachomkera, kinachotishia heshima yake, kinachotishia kesho yake na hata kuchochochea hasira yake.
Unapokuwa na ukomavu wa kihisia, kwa hakika humsikilizi mwenzako kama mtu anayemsoma mwenzake ili kubaini mapungufu yake, wala humsikilizi ili umshauri, umrekebishe, umkosoe na kumfundisha cha kufanya bali kumuelewa yeye kama binadamu timamu, mwenye uhuru mwenye na utashi anayeishi kwenye dunia yake bila kuiingilia. Usikivu, kwa ufupi, ni kumsikiliza mwenzako kwa lengo la kujifunza maana, kwa hakika, unaheshimu uelewa wake hata kama huuelewi.
Kabla hujajua thamani yake isiyoonekana, hujagundua hana unachokitafuta, hujafahamu tabia zake za siri na mapambano asiyopenda kuyazungumzia, hujamwambia jambo gumu lakini muhimu alipokee ikibidi kwa maumivu, huenda unapita fungate ya hisia za upendo zinazopita.
Siku utakapoweza kusikia asichokisema, ukatofautiana naye na bado akamsikiliza, unaelewa kwa nini amekunyamazia, akikukosea unajikagua uone wapi umekosea, ukazijua tabia zake mbaya na bado ukaendelea kumwamini, hapo upendo wako kwake utakuwa umethibitika.
Empathy ni ule upendo wa kina kwa mtu unaokusukuma kuielewa ‘dunia’ yake, kumsikiliza bila kutumia mizani ya misimamo na uelewa wako kumwelewa.
Empathy inakunyenyekeza, inakuondolea haki ya kujiona bora, mjuaji, mzoefu anayeweza kumkosoa, kumhukumu mtu bila kustahi utu wake.
“Hivi ndivyo nilivyo. This’s who I am. Nipende nilivyo au niache.”
Hiki ni kiburi. Unampendaje mtu na unaogopa kubadilika?
Ukimpenda mtu kuna namna unavutwa kumfanania. Upendo hujenga ukaribu unaotengeneza fursa ya kubadilika. Upendo huchochea msukumo wa kulipa gharama fulani.
“Nyumbani panaweza kuwa pa kawaida, lakini daima panaweza kuwa mahali ambapo maneno mazuri yananenwa na matendo mazuri yanafanywa, mahali ambapo adabu na upendo ni wageni wa kudumu.”
– The Adventist Home, uk. 18.
Upendo, kwa hakika, ni kiwango cha juu cha kumwamini mtu, kumkaribisha awe sehemu ya maisha yako, kumruhusu aione sura yako bila maigizo, aujue ukweli wako, aijue hofu yako, ayajue maumivu na majeraha uliyowahi kupitia, ayaone makovu yako na bado uamini hatokugeuka.
Upendo hukufanya ujisikie huru kuwa wewe bila hofu ya kukataliwa, unamruhusu mtu kuukabili upande wa pili wa maisha yako, huogopi akiujua ‘ujinga’ wako, utoto wako unaowanyima wengine kuujua, huogopi akijua unachowaza na kukiamini na bado unaamini ataendelea kuwa rafiki yako na hatotumia anayoyajua kuhusu wewe kinyume na wewe. Kina hiki cha upendo kinazidi raha ya chochote kinachofanyikia mwilini.
Usimuulize mtu maswali yanayoonesha unalazimisha kuambiwa vitu ambavyo mtu mwenyewe hajawa tayari kukuambia.
Kuna vitu mtu anahitaji muda kidogo kujiridhisha na kiwango chako cha kuaminika. Mpe nafasi. Ukifaulu mtihani huo wa imani atakuambia. Ukifeli heshimu faragha ya mtu.
Uhusiano wa kudumu haujengwi na mvuto wa mapenzi na tamaa ya ngono. Mvuto wa mapenzi, pamoja na utamu wake, haudumu. Ukitegemea mvuto wa mapenzi kushikilia uhusiano, hutofika mbali na mtu —maana nguzo kuu ya uhusiano ni ile imani kuwa unamfahamu vizuri uliyenaye, unamuamini, na kwamba uko tayari kuwekeza kwenye uhusiano huo. Hivi viwili vina gharama na vinahitaji muda.
Ukiweza kudhibiti kidogo ‘hisia’ za pale mwanzo mapenzi yanapoanza, ukajipa kidogo muda wa kumfahamu mtu (intimacy), kujua anaamini nini, anayatazamaje maisha, unapunguza uwezekano maumivu mengi ya kushtukiza na kwa kufanya hivyo, unaongeza uwezekano wa uhusiano wenu kudumu (commitment).
Ukiangalia mchoro huu wa nadharia ya mapenzi ya mshunuzi Steinberg unaona hatari ya kuwekeza kwenye mvuto wa mapenzi usioenda sambamba na kufahamiana. Ghafla, Steinberg anasema, haidumu. Utajifunza staili zote za ngono lakini bila kuwekeza kwenye kuunganisha fikra na mtazamo wenu, ni suala la muda tu ‘grafu’ itawarudusha panapostahili.
Ukiweza kutofautisha hisia za ngono na mapenzi uwezekano wa mahusiano unayoyaanzisha kudumu unakuwa mkubwa. Hisia za ngono, tamaa, ni msukumo wa kimwili unaowachochea wanyama kuzaliana. Nzi, pamoja na udogo wake anazo hisia hizi—sexual instincts—ingawa hana mapenzi.
Hisia za ngono (tamaa) zikiwa kipaumbele chako, vigumu kuwekeza kwenye mahusiano yanayokutanisha fikra na kuruhusu mikinzano ya mawazo kujenga utambulisho wa pamoja—intimacy. Ukaribu wako na mtu, aghalabu, utalenga kukutanisha miili kuliko fikra, imani na mambo yanayowatambulisha (identities). Utavutiwa na mwonekano, utamtamani, ukifanikiwa kukidhi tamaa za mwili hisia hizo zitapoa. Usipozimudu hisia hizi, kama ilivyo kwa nzi, unaweza kucheza na wengi kwa mpigo—maana huwapendi.
Mapenzi, tofauti na hisia za ngono, ndizo zinatutofautisha na wanyama wengine. Ukimpenda mtu unahamia kwenye fikra, imani na misimamo yenu. Upendo unakuchochea kuweka mazingira ya kumwamini, kumfanya kuwa sehemu ya faragha yako, na hivyo unampandisha ngazi ya kumruhusu kukufahamu, kuyafahamu matumaini yako, kuzijua aibu zako. Upendo unakuchochea kujitoa ili kumheshimu, kumstahi na kumfanya kuwa sehemu ya maisha yako.
Ukaribu wa kiwango hiki ndio unaochochea muunganiko wa utambulisho wenu (identity) ili kuufanya kuwa mmoja. Huo ndio upendo unaodumu, kwa mujibu wa mshunuzi Sternberg. Ingawa uwezo huu anao mwanadamu, ukishakosa upendo wa mzazi utotoni, inaweza kukuwia vigumu mno kumpenda mtu mwingine au hata kumruhusu mtu mwingine akupende kwa kiwango hiki. Katika mazingira kama haya, watu wengi huishia kwenye hisia za ngono, na uwezekano wa ajali nyingi za mahusiano unakuwa mkubwa zaidi.
Hisia za ngono ni hulka ya maumbile inayowawezesha wanyama kuzaliana. Hata nzi, huwezi amini, ana sexual instincts. Ingawa hana mapenzi, nzi ana hisia za ngono. Usipojidhibiti, ukamudu tamaa za mwili, kama ilivyo kwa nzi, unaweza kuwa nazo kwa watu wengi usiowapenda.
Hisia za mapenzi ndizo zinatutofautisha na wanyama wengine wote. Ukimpenda mtu unamwamini, unamfanya kuwa sehemu ya faragha yako, unamruhusu akufahamu, ajue matumaini yako, aibu zako, akustahi na nyote mnaunganisha utambulisho wenu kuwa mmoja. Nzi huko hawezi kufika.
Huwezi kuwapenda watu wawili kwa wakati mmoja isipokuwa kama kinachowaunganisha [na mmoja wao] ni ngono na labda mwenzetu unayatazama mapenzi kama mahusiano yasiyokuleta karibu na mtu na kukulazimisha kupoteza kwa kiwango hicho.
Kuna ‘mahusiano’ yanakunyanyasa na kukuumiza na huondoki. Ukishalalamika kwa kila mtu unarudi kule kule. Kuna kazi inakutesa na huiachi. Huishi kulalamika na kazi huachi.
Ubongo una tabia ya kututafutia utulivu. Ukiteseka sana ubongo unamaliza kesi kwa kutuchagulia ‘zimwi tulijualo.’ Unajisikia salama kwenye maumivu uliyoyazoea. Unaona bora kichaa unayemfahamu. Unaona bora ajira mbaya uliyonayo tayari.
Ndio maana unaweza kumshauri mtu aondoke unashangaa anarudi kule kule. Kumbe wakati wewe unaitazama hali yake kwa jicho la ‘akiondoka atakuwa salama,’ mwenyewe anauona usalama kwenye mateso unayotaka ayakimbie. Malalamiko unayoyasikilia ni kilio kinachotafuta kusikia ‘endelea kumvumilia.’