“Hakikisha unaweka utaratibu wa watoto wakiamka asubuhi wanaanza siku kwa kujuliana hali kabla hawajaendelea na michezo au kwenda shule. Wewe pia mzazi walazimike kukusalimia kujua umeamkaje ndio mambo yao mengine yaendelee.”
“Ukifanikiwa hilo, familia kusalimiana inakuwa sehemu ya shughuli za msingi kukamilisha siku. Ukubwani, mambo mengine yakiwa sawa, watoto wasiposalimiana kuna kitu muhimu watahisi kinapungua—familia kusalimiana inakuwa tabia isiyohitaji kukumbushana.”
Kujipendekeza sio ‘networking.’ Watu hufuata thamani. Ikiwa huna ufumbuzi fulani unaorahisisha kazi za watu, unaweza kufahamiana na watu wengi na isikusaidie.
Ufumbuzi ni matokeo ya kutumia muda mwingi kujifunza, kujitafuta na kujenga umahiri unaoambatana na ukiwa kwa muda. Thamani yako ikianza kuonekana, ‘network’ zitakuja zenyewe wala hutotumia nguvu.
Ukifanikiwa kupata saa 5 tu kwa wiki (sawa na wastani wa dakika 43 kwa siku) utulie na mwanao, usikilize story zake, ucheze michezo yake, ujibu maswali yake, umpongeze kwa aliyoyafanya, umrekebishe alikokosea, useme jambo atakalolikumbuka, hizo ni takribani siku 10 za mawasiliano ya mzazi na mwanae kwa mwaka. Siku 10 za ‘quality time’ na mtoto kwa mwaka.
Sasa fikiria wastani wa umri wa mtoto kwenda kidato cha kwanza, aghalabu shule ya bweni kwa wengi wetu, ni miaka 12. Huo ndio umri anakutana na watoto wa familia nyingine, walimu wanaowaza mitihani na ufaulu na watu wazima wengine ambao wakati mwingine hatuna hakika wanapanda nini kwa watoto, na wewe mzazi wake kipindi hicho utakuwa umewekeza miezi minne (au pungufu) ya kumjengea sauti atakayoisikia anapofanya maamuzi huko aliko.
Kwa umri wake huo wa miaka 12, ukiondoa takribani miaka 5 ya kulala, wataalamu wanasema kinachochukua muda wake mwingi ndicho kinachoamua anachokiamini, anachokifikiri, anachokiamua na kubeba utambulisho wake. Je, nani huyo ametumia muda mwingi na mtoto kumfundisha, kumtazamisha, kuwekeza kwenye ufahamu wake? Unadhani ni kwa kiasi gani mzazi utakuwa na ushawishi kwa mtoto huyu uliyewekeza miezi minne kwa miaka 12—tena pengine ukiadhibu zaidi na kuonya kuliko kuhusiana? Tafakari hili kabla hujasema, ‘watoto wa siku hizi hawasikii.’ Silengi kukufanya ujisikie hatia. Nakukumbusha Juni hii hapa na watoto wanarudi nyumbani.
Waovu wana ‘kipaji’ cha kujilinda na kujihami. Kwanza, hujijengea uhalali kwa kujisogeza karibu na waovu wenzao (coalition of the evil) ili kujipatia uhakika wa kinga dhidi ya maovu yao. Ukaribu na chama cha waovu unawasaidia kuwa na kundi kubwa linaloweza kuwatetea—maana kila mwanachama ana siri ya mwenzake.
Lakini pia, ukimsoma Albert Bandura unaona waovu husambaza na kufubaza hatia zao kwa kuimarisha mtandao na watu wanaojua adui yao anawaogopa. Unapokuwa karibu na adui wa adui yako, ni kama unamchanganya adui yako asiwe na haraka ya kukushughulikia. Kukushughulikia wewe inamaanisha kumshughulikia mwovu mwenzako.
Kinachoimarisha umoja wa waovu kuteteana, ni ukweli kuwa waovu wanaijua siri kuwa watu wema, shauri za dhamira zao, hupata shida kuwakemea waovu maana kuna saa ni kama hawaamini mtu anaweza kuwa mwovu kwa kiwango hicho.
Watu wema, aghalabu, huishia kugombana wao kwa wao maana wana dhamira inayowashtaki wanapotaka kumuwajibisha mtu mwovu. Inakuwa kama kumwuumiza mwovu ni sawa na kumtendea uovu hii ndio sababu waovu wengi huponyoka kuwajibikia uovu wao. Waovu, tofauti na binadamu wema, hawanaga “dhamiri” hiyo — hivyo wanaungana kwa urahisi zaidi na kuwachezea wema kirahisi sana.
@bwaya Nipo hapa kudhibitisha moja ya mambo umesema hapo, Watanzania wenzangu hakuna mtu anaekufatilia isipo kuwa mwizi anae taka kukuibia, wengine wote tunazoshida zetu tunazifatilia tuzimalize.
Ungekuwa huogopi kushindwa, ungekuwa huogopi watu watakavyosema ukikosea, ungekuwa hulindi sura fulani ya ‘mafanikio’ usiyokuwanayo, ungekuwa huogopi kufanya kazi zisizoendana na jina lako kubwa, zisizoendana na ‘brand’, elimu yako isiyotatua chochote, na heshima kubwa usiyonayo unadhani ungeshafanya nini tangu mwaka uanze? Juni hii hapa.
Ukweli ni kwamba watu wala hawakufikirii kivile kama unavyodhania. Ungejua kila mtu anateseka na mambo yake kimya kimya wala usingejitwisha mzigo wa kufikiria namna watu wanavyokufikiria. Ungejua watu wala hawakupi umuhimu mpaka utakapofanikiwa, ungepambana kufanya hicho unachoogopa kufanya. Tunaelekea nusu mwaka. Mwaka ukiisha utajuta zaidi kwa kile ulichoogopa na kushindwa kukifanya kuliko kile ulichokifanya na kukosea.