Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 19 Mei, 2025.
Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Mambo ya Ndani na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua za haraka kwa wanaotumia mitandao na teknolojia vibaya, akikemea pia wingi wa Wanaharakati kutoka nje ya nchi wanaojaribu kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania na kutaka kuivuruga amani.
Rais Samia amesema hayo Jijini Dar es salam leo May 19, 2025 wakati akizindua Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 (Toleo la 2024), ambapo amesema hatotoa nafasi kwa watovu wa adabu kutoka nje ya nchi kuja kujaribu kuvuruga amani, utulivu na usalama uliopo nchini Tanzania.
“Tusiwe shamba la Bibi kwamba Mtu anaweza kuja Tanzania akasema analolitaka, lipo Tanzania halipo, Watu wakajisemea tu, tumeanza kuona mwenendo wa Wanaharakati ndani ya Ukanda huu kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku, sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia, tusitoe nafasi walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika ni hapa kwetu, niwaombe Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutotoa nafasi kwa Watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kutovuka hapa kwetu, hapana”
“Nimeona clip kadhaa za kunisema, nipo bias na nini, ninalofanya ni kulinda nchi yangu na ndiyo wajibu wangu niliopewa, kwahiyo hatutotoa nafasi kwa kiumbe yeyote kuja kutuvurugia hapa awe yupo ndani ama anayetoka nje”
Katika maelezo yake, Rais Samia ameitaka Wizara na Maafisa wanaohusika kutoa ufafanuzi kuhusu yale yanayosemwa na Wanaharakati na Watu mbalimbali, kukanusha ama kuchukua hatua za haraka ikiwa yanayosemwa yana ukweli kuhusiana na sekta zao mbalimbali.
RAIS SAMIA AWAKARIBISHA DIASPORA NA RAIA WA KIGENI KUWEKEZA NCHINI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewakaribisha Watanzania wanaoishi Nje ya nchi maarufu kama Diaspora pamoja na Raia wa Kigeni na Sekta zao binafsi kuja kuwekeza nchini Tanzania, akieleza kuwa sasa Sera ya Mambo ya nje inawatambua rasmi kama wabia muhimu wa maendeleo ya Tanzania.
Aidha Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa uhusiano na Diplomasia ya Kimataifa ni suala linalohusu pia ulinzi na usalama wa nchi hivyo ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama nchini Tanzania kuhakikisha kuwa wanajidhatiti katika kudhibiti vitendo vya uhalifu wa kuvuka mipaka pamoja na matendo ya kigaidi yanayoendelea kote duniani kwa kuhakikisha mipaka inakuwa salama na amani inatamalaki nchini.
Rais Samia amebainisha hayo leo Jumatatu Mei 19, 2025 kwenye Hafla ya uzinduzi wa sera ya mambo ya nje ya Mwaka 2001, toleo la mwaka 2024, akiwahamasisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuwa mabalozi wema wa Tanzania kwa kutangaza mazuri na fursa zinazopatikana nchini Tanzania.
Aidha Rais Samia ametoa wito kwa watanzania hususani Vijana pamoja na sekta binafsi nchini, kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii zilizopo nchini, akizitaka Mamlaka zinazosimamia ajira nje ya nchi kuja na sera na sheria rafiki kwa Watanzania ili waweze kufaidika na mahusiano mema ya Tanzania na Mataifa mengine ambayo yamekuwa yakitoa fursa za ajira kwa raia wa kigeni.
Tanzania na Finland zimekubaliana kuendelea kushirikiana na kuimarisha ushirikiano wao kwenye Elimu ya kidigitali pamoja na ukuzaji wa vituo atamizi (Incubation Hubs) kwaajili ya kampuni changa zilizopo nchini Tanzania.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo ya Marais wa nchi hizo mbili, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Alexander Stubb, wakati wa mazungumzo yao mara baada ya Rais Stubb kuwasili nchini Tanzania leo Jumatano Mei 14, 2025 kwaajili ya ziara ya kikazi kufuatia mualiko wa Rais Samia.
"Vilevile ni dhamira yetu kuona namna tunavyoweza kushirikiana kukuza zaidi matumizi ya TEHAMA kwenye sekta muhimu za uzalishaji kuendana na mikakati yetu ya Kidigitali."- Amesema Rais Samia.
Mbele ya wanahabari mara baada ya mazungumzo yao, Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa majadiliano yao yameimarisha pia mahusiano katika sekta muhimu ikiwa pia ni pamoja na kusaidia katika uimarishaji wa huduma za serikali mtandao na usalama wa mtandao.
Katika mazungumzo yao, Rais Samia pia amemuahidi Rais Stubb kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Finland kwenye Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya Kimataifa katika kuhakikisha kuwa wanalinda amani na ustawi wa watu wa Mataifa hayo mawili yenye urafiki wa zaidi ya miaka sitini kwa hivi sasa.
Awali Rais Stubb amemueleza Rais Samia kuwa Finland kwasasa inafanya kazi na Mataifa mawili pekee barani Afrika ambayo ni Tanzania pamoja na Ethiopia, suala ambalo linadhihirisha mahusiano ya dhati miongoni mwa mataifa hayo mawili yaliyo rafiki.
Tanzania na Finland zimekubaliana kuendelea kushirikiana na kuimarisha ushirikiano wao kwenye Elimu ya kidigitali pamoja na ukuzaji wa vituo atamizi (Incubation Hubs) kwaajili ya kampuni changa zilizopo nchini Tanzania.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo ya Marais wa nchi hizo mbili, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Alexander Stubb, wakati wa mazungumzo yao mara baada ya Rais Stubb kuwasili nchini Tanzania leo Jumatano Mei 14, 2025 kwaajili ya ziara ya kikazi kufuatia mualiko wa Rais Samia.
"Vilevile ni dhamira yetu kuona namna tunavyoweza kushirikiana kukuza zaidi matumizi ya TEHAMA kwenye sekta muhimu za uzalishaji kuendana na mikakati yetu ya Kidigitali."- Amesema Rais Samia.
Mbele ya wanahabari mara baada ya mazungumzo yao, Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa majadiliano yao yameimarisha pia mahusiano katika sekta muhimu ikiwa pia ni pamoja na kusaidia katika uimarishaji wa huduma za serikali mtandao na usalama wa mtandao.
Katika mazungumzo yao, Rais Samia pia amemuahidi Rais Stubb kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Finland kwenye Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya Kimataifa katika kuhakikisha kuwa wanalinda amani na ustawi wa watu wa Mataifa hayo mawili yenye urafiki wa zaidi ya miaka sitini kwa hivi sasa.
Awali Rais Stubb amemueleza Rais Samia kuwa Finland kwasasa inafanya kazi na Mataifa mawili pekee barani Afrika ambayo ni Tanzania pamoja na Ethiopia, suala ambalo linadhihirisha mahusiano ya dhati miongoni mwa mataifa hayo mawili yaliyo rafiki.
Rais wa Jamhuri ya Finland Mhe. Alexander Stubb akikagua Gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Finland Mhe. Alexander Stubb wakati wimbo wa Taifa wa Tanzania na ule wa Finland ukiimbwa katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei, 2025.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeelezwa kutengua uteuzi wa viongozi wanane wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waliothibitishwa na Baraza Kuu la chama hicho mnamo Januari 22, 2025, kutokana na kutokuwepo kwa akidi halali ya kikao hicho. Kwa mujibu wa taarifa ya tovuti ya Mwananchi ya siku ya Jumanne, hatua hiyo imechukuliwa kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa na Lembrus Mchome, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, akipinga uhalali wa kikao hicho kwa madai kuwa akidi ya wajumbe haikufikiwa. Viongozi waliotenguliwa ni pamoja na John Mnyika – Katibu Mkuu, Amani Golugwa – Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Ally Ibrahim Juma – Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar). Wengine ni Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh, na Dk. Rugemeleza Nshala (Mwanasheria Mkuu wa chama) ambao ni Wajumbe wa Kamati Kuu Msajili ametoa maelekezo kwa CHADEMA kuitisha Baraza Kuu jipya lenye akidi stahiki, ili kufanikisha uteuzi upya wa viongozi hao kwa mujibu wa Katiba ya chama, Sheria ya Vyama vya Siasa, na kanuni zinazohusika. Katika mafunzo ya viongozi wa BAWACHA na BAVICHA Kanda ya Kusini mnamo Machi 25, 2025, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alieleza kuwa akidi ya kikao hicho ilikuwa sahihi, kwa kuwa kilihusiana na uteuzi wa kawaida si mabadiliko ya katiba wala uchaguzi. Mnyika alisema kikao hicho kilikuwa na zaidi ya asilimia 50 ya wajumbe, akisisitiza kuwa hiyo ilikuwa akidi ya kutosha kwa mujibu wa taratibu za ndani. Hata hivyo, Ofisi ya Msajili, baada ya kupitia malalamiko ya Mchome na majibu ya CHADEMA, imeafiki kwamba akidi haikufikiwa na hivyo uamuzi wa kikao hicho si halali. Kwa mujibu wa chanzo cha ndani ya CHADEMA kilichozungumza na tovuti hiyo, uamuzi wa msajili ni "taarifa mbaya sana kwa chama" na unaweka chama katika hatari ya kisheria iwapo hakitatekeleza maelekezo hayo. Chanzo hicho kimesema kuwa viongozi wengi kwa sasa wako mikoani wakitekeleza operesheni ya "No Reforms, No Election." Aidha, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CHADEMA, Brenda Rupia, ameeleza kusikia taarifa hizo, akisema bado anazifuatilia na chama kitatoa taarifa rasmi pindi zitakapothibitishwa. Kwa upande wake, Mchome amesema siku ya Jumatano, Mei 14, 2025, atazungumza na wanahabari kuhusu uamuzi wa Msajili juu ya malalamiko yake kwani hakukataa wala kukubali juu ya taarifa hiyo. Viongozi mbalimbali wa ofisi ya msajili akiwemo Msajili mwenyewe, Jaji Francis Mutungi na au Naibu Msajili, Sisty Nyahoza wametafutwa kuzungumzia suala hilo bila mafanikio. Jitihada za kuwatafuta bado zinaendelea.
Rais wa Burkina Faso Ibrahim Traoré Apokelewa Rasmi na Rais Vladimir Putin na Kushiriki Sherehe za Siku ya Ushindi Moscow
MOSCOW, Mei 9. Rais wa mpito wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, amepokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Urusi Vladimir Putin, alipowasili jijini Moscow kushiriki katika sherehe za maadhimisho ya miaka 80 ya Ushindi wa Umoja wa Kisovyeti dhidi ya Ujerumani ya Nazi katika Vita ya Pili ya Dunia.
Kupokelewa huko kulifanyika kwa heshima zote za kidiplomasia, Katika tukio hilo la kihistoria, Rais Traoré ameungana na viongozi wengine kutoka mataifa mbalimbali kushuhudia gwaride la kijeshi lililopambwa kwa maandamano ya vikosi vya Urusi, magari ya kivita, na maonyesho ya silaha za kisasa.
Tangu kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso mnamo Septemba 2022 yaliyomuweka madarakani Kapteni Ibrahim Traoré, uhusiano kati ya Burkina Faso na Urusi umeimarika kwa kasi. Serikali ya mpito imeelekeza siasa zake za kigeni kuelekea mashariki, ikitafuta ushirikiano wa karibu zaidi na Urusi katika nyanja za kijeshi, kiusalama, na maendeleo ya kiuchumi.
Urusi imekuwa ikitoa msaada wa kijeshi kwa Burkina Faso, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kijeshi na mafunzo kwa wanajeshi, ili kusaidia taifa hilo kupambana na makundi ya kigaidi yanayoshambulia eneo la Sahel. Aidha, kumekuwa na mikataba na mazungumzo kuhusu ushirikiano katika sekta za nishati, kilimo, na elimu.
Mwelekeo huu mpya umechukuliwa kama juhudi ya Burkina Faso kujiondoa kwenye utegemezi wa kihistoria kwa mataifa ya Magharibi, hasa Ufaransa, na kujenga ushirikiano wa kimkakati na Urusi kama mshirika mbadala.
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Msumbiji zimetiliana saini mkataba wa kubadilishana wafungwa baina ya nchi hizo mbili. Mkataba huo umetiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Maria Lucas na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Tanzania, Innocent Bashungwa.
Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na Serikali ya Msumbiji ya kushirikiana katika kukuza na kuendeleza utamaduni baina ya nchi hizo mbili.
Mkataba wa makubaliao hayo umesainiwa leo Mei 8, 2025 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), imeingia makubaliano na Serikali ya Msumbiji kupitia Redio ya nchi hiyo kuwa na Ushirikiano utakaowezesha nchi hizo kushirikiana katika upashanaji habari.
Mkataba wa makubaliano hayo umesainiwa leo Mei 8, 2025 Ikulu Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayub Rioba Chacha na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Redio Msumbiji, Abdul Naguibo Abdula
"Kwa niaba ya Serikali na Watanzania wote, nirejee tena pongezi zetu za dhati kwa Mheshimiwa Chapo kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji. Kwa hakika ushindi wake umepokelewa vizuri na Watanzania." - Rais Samia Suluhu na Rais wa Msumbiji wakizungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Msumbiji Mhe.Daniel Chapo amesema uhusiano imara wa kidiplomasia na kihistoria kati ya Tanzania na Msumbiji hauakisi ushirikiano na uhusiano wa kiuchumi uliopo kati ya mataifa hayo.
Kwa kutambua hilo, Rais Samia amewaambia wanahabari kusema kuwa mataifa hayo mawili yamekubaliana kushirikiana kutafuta mbinu za kurahisisha ufanyaji biashara kati ya wafanyabiashara wa nchi hizo mbili kwa lengo la kukuza uchumi.
Sambamba na hilo, amesema wamekubaliana kuwa na vituo vya pamoja katika mipaka ya mataifa hayo, ikiwa ni sehemu ya hatua ya kufanikisha kuimarisha kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo. "Tumekubaliana licha ya ujirani na uhusiano mzuri wa kihistoria tulionao, bado ushirikiano wa kiuchumi haujaenda sambamba na ushirikiano wa kidiplomasia," ameeleza Rais Samia.
Katika kufanikisha jambo hilo, amesema wamekubaliana kushirikiana kurahisisha mazingira ya biashara kuwafanya wafanyabiashara wawe huru pande zote na hivyo kukuza uchumi kwa kuwa na vituo vya pamoja katika mipaka ya mataifa hayo, kadhalika kuanzisha tume ya pamoja ya kiuchumi na itakayofuatilia makubaliano ya ushirikiano ili kukuza uchumi haraka kwa pande zote.
"Uhusiano wa kiuchumi unakuzwa na kuimarika kwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji na tumekubaliana kujenga miundombinu yetu ya mipakani inayounganisha nchi zetu," amesema.
Kuhusu fursa za uchumi wa buluu, amesema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya rasilimali. Kwa kutamba kuwa uchumi unategemea kilimo, amesema wamekubaliana kubadilishana uzoefu na kufanya tafiti za pamoja katika Kilimo hasa cha korosho.
Sambamba na hayo, amempongeza Rais Chapo kwa ushindi wake katika uchaguzi wa Oktoba mwaka jana nchini Msumbiji, pia amemshukuru kwa hatua ya kukubali mwaliko wa kutembelea Tanzania.
"Tanzania na Msumbiji ni ndugu wa damu ndio maana jamii za wamakonde, wamakua na wayao wanapatikana pande zote na haishangazi kuona tamaduni zinafanana," amesema.
Sekta ya Utangazaji Ni Nguzo Muhimu ya Maendeleo – Dkt. Jabiri Bakari
Dar es Salaam, Tanzania – Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari, amesisitiza kuwa sekta ya utangazaji ni muhimili muhimu katika kuendeleza jamii kwa nyanja zote; kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Akizungumza usiku huu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za Samia Kalamu Awards 2025, Dkt. Bakari alisema kuwa vyombo vya habari kama redio na televisheni vina nafasi ya kipekee katika kuwafikishia wananchi taarifa sahihi kuhusu masuala mbalimbali kama afya, elimu, siasa, mazingira na uchumi.
“Wananchi wanapopata taarifa sahihi, huongeza uelewa wao na hivyo kufanya maamuzi bora yanayowanufaisha wao binafsi na taifa kwa ujumla,” alieleza Dkt. Bakari.
Aidha, aliongeza kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuhifadhi, kukuza na kuendeleza utamaduni wa Taifa kwa kueneza mila na desturi, pamoja na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa mshikamano na kudumisha amani.
Tuzo za Samia Kalamu Awards zimetolewa kwa lengo la kutambua na kuhamasisha umahiri wa wanahabari katika kuandika habari zenye kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
RAIS SAMIA ATANGAZA ONGEZEKO LA MSHAHARA KWA ASILIMIA 35.1%, MPANGO SEKTA BINAFSI WAJA.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Mei Mosi, 2025 wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Singida, ametangaza kuongeza Kima cha chini ya mishahara kwa watumishi wa Umma kutoka Shilingi 370,000 kwa Mwezi hadi shilingi 500,000 sawa na Ongezeko la asilimia 35.1%.
"Mimi na wenzangu na baada ya kuangalia uchumi ulivyopanda na ukipanda kwasababu ya nguvu zenu wafanyakazi, ninayo furaha ya kuwatangazia kwamba katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, mwaka huu serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1%." Amesema Rais Samia.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wake, Rais Samia ameeleza kuwa mabadiliko hayo mapya yataanza kutumika rasmi mwezi Julai mwaka huu, akiahidi pia mabadiliko ya mishahara kwa watumishi wa ngazi nyinginezo.
Katika hatua nyingine pia Rais Samia ameeleza kuwa bodi ya Kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi inaendelea na tathmini yake ya kupitia mishahara ya sekta binafsi, akihimiza pia Wizara ya kazi pamoja na vyama vya wafanyakazi kufanya vikao na waajiri wa sekta binafsi ili kulipa mishahara kulingana na hali bora ya wafanyakazi inayohimizwa ili walau kuendana na mishahara ya kima cha chini kilichopo serikalini.
SERIKALI KUSHUGHULIKIA MAKATO YANAYOKATWA KWENYE POSHO NA MOTISHA ZA WATUMISHI WA UMMA
Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali yake itakaa ma Taasisi husika ili kushughulikia maombi yaliyowasilishwa kwake na Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi nchini, walioomba kufutwa kwa tozo mbalimbali zinazotozwa kwenye posho, nauli na motisha mbalimbali wanazopewa watumishi wa umma.
Akizungumza na wafanyakazi na Wananchi waliojitokeza kwa Wingi kwenye sherehe za siku ya wafanyakazi duniani zilizofanyika Kitaifa Mjini Singida katika viwanya vya Bombadia leo Mei Mosi, 2025, Rais Samia pia ameziagiza wizara zinazohusika na ajira kusimamia kwa ukaribu Mfumo wa ajira za muda mfupi kwenye sekta binafsi nchini kutokana na kulalamikiwa na vyama vya wafanyakazi kutofuata taratibu na staha za kazi kwa wafanyakazi mbalimbali, akisisitiza kuwa ajira za muda mfupi ni lazima ziwe na staha na zenye kuzingatia masharti na stahiki zote.
Rais Samia pia ameeleza kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa mchakato wa Bima ya afya kwa wote, akieleza kuwa kwasasa wanaandaa vitita vya mafao rahisi kwa wote na kusisisitiza kuwa wakati mchakato huo unasubiriwa, Wastaafu mbalimbali wanaweza kujiunga na mifumo ya CHF na NHIF ili kuendelea kupata stahiki mbalimbali.
RAIS SAMIA ATOA WITO WA KULINDA AMANI, AONYA VYAMA VYA WAFANYAKAZI KUTOCHOCHEA MACHAFUKO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi kuhakikisha wanadumisha amani na utulivu nchini, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa misingi hiyo muhimu.
Akizungumza Alhamisi Mei 1, 2025 kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Bombadia, mkoani Singida, Rais Samia alisema historia ya vyama vya wafanyakazi nchini ni ya kupigania uhuru, hivyo haviwezi sasa kutumiwa kama vyombo vya kuchafua nchi.
"Ili tuweze kujenga taifa letu ni lazima tulinde amani na utulivu nchini kwetu. Tusitoe fursa kwa vyama vya wafanyakazi kutumika kuichafua nchi yetu," amsema Rais Samia mbele ya maelfu ya wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Rais amesisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi wa vyama vya wafanyakazi kusimamia na kulinda misingi ya amani, akiwataka kutambua nafasi yao katika kulinda heshima ya uhuru uliopatikana kwa gharama kubwa.
"Historia ya vyama vya wafanyakazi ni vyama vilivyoleta vuguvugu la uhuru wa nchi hii. Sasa tusijibadilishe tukawa vyama vya kusaliti uhuru wetu tulioitafuta kwa nguvu kubwa," ameongeza.
Kauli hiyo ya Rais Samia imekuja katika kipindi ambacho maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 yanaendelea, ambapo wadau mbalimbali wamekuwa wakihamasisha utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Sheikh Aomba Dua ya Miaka Mitano Zaidi kwa Rais Samia Katika Sherehe za Mei Mosi
Katika kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 1 Mei 2025 mkoani Singida, Sheikh aliyealikwa kwa ajili ya kusoma dua ya ufunguzi alitumia nafasi hiyo kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, aongezewe miaka mitano mingine ya uongozi.
Sheikh huyo, ambaye hakutajwa jina lake mara moja kwenye taarifa za awali, aliomba dua hiyo mbele ya viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa vyama vya wafanyakazi, wageni waalikwa, na maelfu ya wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo.
Katika dua yake, alimsihi Mwenyezi Mungu ampe Rais Samia uhai, afya njema, hekima, na umri mrefu wa kuwatumikia Watanzania, huku akiweka wazi matumaini yake kuwa Rais huyo apate fursa ya kutumikia tena muhula mwingine wa miaka mitano.
Kauli hiyo ilizua hisia tofauti miongoni mwa baadhi ya washiriki, huku wengine wakichukulia kama ishara ya kuunga mkono utendaji wa Rais Samia, ambaye tangu aingie madarakani amekuwa akitekeleza mageuzi mbalimbali katika sekta za kiuchumi, kijamii, na kiutawala.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam kupitia kwa Kamanda wake Muliro Jumanne, limesema limemkamata Mtu mmoja kwa tuhuma za kumshambulia Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania Padri Charles Kitima jana. Taarifa ya Polisi imeeleza kuwa jana tarehe 30 April 2025 saa nne usiku maeneo ya Baraza la Maaskofu Kurasini Dar e salaam, ilipokelewa taarifa ya kujeruhiwa kwa Padri Kitima ambapo tangu saa tatu asubuhi Viongozi wa dini mbalimbali walikuwa katika kikao. Imeelezwa kuwa baada ya kikao kuisha saa moja jioni, Padri huyo alikwenda Kantini alikokaa hadi saa nne na robo usiku ambapo aliponyanyuka kwenda maliwatoni pembeni ya Kantini hiyo kushambuliwa kichwani na Watu wawili ambao walitumia kitu butu kumshambulia. Taarifa ya Polisi imeeleza kuwa Padri huyo aliwaishwa Hospitali na anaendelea vizuri kwa sasa ambapo tayari Mtu mmoja kati ya wawili hao amekamatwa na kutajwa kuwa Rauli Mahabi Haraja Mkazi wa Kurasini ambaye anashikiliwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo "uchunguzi wa kina unaendelea ili hatua kali na za haraka zichukuliwe kwa Wahusika"