Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amemtaja Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, kuwa msema kweli anayestahili kupongezwa badala ya kushambuliwa, kufuatia kauli yake ya kuwataka viongozi wa chama hicho kuachana na wanaharakati wa nje.
Wasira amesema hana ugomvi na Lema, akieleza kuwa amefurahishwa na uamuzi wake wa kuzungumza ukweli kuhusu mchango wa wanaharakati katika mabadiliko ya uongozi wa CHADEMA, akiwemo Freeman Mbowe, Tundu Lissu na John Heche.
Ametoa kauli hiyo Novemba 3, 2026, wakati akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Chamwino, mkoani Dodoma, ambako alikuwa akimnadi mgombea wa CCM, Dk Netho Ndilito.
“Sina ugomvi na Lema, kwanza alikuwa mbunge mwenzangu, lakini jana aliamua kusema ukweli kwamba wanaharakati walisaidia uchaguzi wa CHADEMA mwaka jana, wakamtoa Mbowe na kumuingiza Lissu na Heche, sasa wameanza kuingia mambo mengine,” amesema Wasira.
Amesema CCM haina ugomvi na CHADEMA, akisisitiza kuwa ushindani wa kisiasa unapaswa kujengwa katika hoja badala ya matusi na mashambulizi yasiyosaidia kujenga taifa. Ameongeza kuwa mazungumzo ya kisiasa yanapaswa kuendeshwa na wahusika bila kuingiliwa na watu wa nje.
Katika hatua nyingine, Wasira amemtaja Dk Ndilito kuwa mgombea mwenye uzoefu wa kiutendaji kutokana na nafasi mbalimbali alizowahi kushika katika halmashauri, Serikali na ndani ya CCM, akiwataka wananchi kumpigia kura ili aendeleze miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Deogratius Ndejembi, aliyeteuliwa kuwa Makamu wa Rais.
Kwa upande wake, Dk Ndilito ameahidi kukamilisha miradi yote iliyoanzishwa katika jimbo hilo, akitaja migogoro ya ardhi na madai ya baadhi ya watumishi wa umma kuwanyanyasa wananchi kuwa miongoni mwa mambo atakayoyapa kipaumbele endapo atachaguliwa kuwa mbunge.
VIDEO:
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ametoa ufafanuzi wa kisayansi kuhusu maana halisi ya El Niño na kutetea taarifa za wataalamu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), huku akifafanua ukweli kuhusu makadirio ya Shilingi bilioni 730 zilizotajwa kwa ajili ya utayari wa kukabiliana na majanga na athari za El Niño.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Msigwa ameeleza kuwa El Niño kimsingi ni ongezeko la joto linaloweza kuambatana na mvua za kupita kiasi au jua kali kulingana na eneo, huku akitaka wananchi kuacha kuwashambulia au kuwakosoa wataalamu wa hali ya hewa.
Msigwa amebainisha kuwa ingawa uhuru wa kujieleza na kukosoa upo, si vyema kwa watu wasio na utaalamu kupotosha umma au kumkosoa mtaalamu mbobezi wa sekta husika.
Kuhusu hofu na upotoshaji uliozuka kuhusiana na kiasi cha Shilingi bilioni 730, Msigwa amefafanua kuwa fedha hizo si taslimu zilizowekwa pembeni au kuliwa, bali ni makadirio ya gharama zitakazotumiwa na serikali pamoja na sekta binafsi katika kujiandaa na kujilinda dhidi ya majanga.