Unaweza kufurahia kile ulichonacho na hatua unazopiga bila kuwabeza waliokutangulia. Kesho ni fumbo. Usione watu wanaongea kwa tahadhari. Maisha yamewahekimisha.
@cc@bwaya
Usipoweza kuijali familia yako mwenyewe ngumu sana kujali mtu mwingine. Usinielewe vibaya. Sijasema haiwezekani. Nimesema ngumu sana.
Sasa usikurupuke, “mbona nanywesha sana jamaa zangu pombe?” Tofautisha kujali na kumfanyia hisani mtu unayetaka akufanikishie jambo lako.
Ukiwa mwema kwa watu wanaojua upande wako wa pili vizuri, wewe ni mtu mwema. Utu wa mtu unaanza kwa watu wa nyumbani kwake.
“Ustaarabu wa jamii haupimwi kwa vile inavyowatendea raia wake wema na wenye mchango mkubwa katika jamii bali namna inavyowatendea wahalifu [na wapinzani wa maendeleo.]”
—Fyodor Dostoyevsky
Ukisoma maandikio ya Maslow mwenyewe unaona anapozungumzia utoshelevu (self-actualization) ni ile hatua ya juu kabisa ya mwanadamu kujitambua, kujikubali na kuachilia kile alichonacho kwa ajili ya wengine. Maslow anafikiri huwezi kupata utoshelevu bila kuvuka mtazamo finyu wa maisha unaomfanya afikiri anaishi kujitumikia na kuwatumikisha wengine. Utoshelevu, kwa maana hiyo, unaanzia pale unapovuka kiambaza cha kuwa mtumwa wa mahitaji yako mwenyewe—ubinafsi.
Hiki ni kiwango cha juu kabisa cha uwepo wa mtu hapa duniani. Unakuwa umejitambua, umejua ndani yake una nini cha kuwapa watu wengine bila kuwatumia kufanikisha malengo yake. Unakuwa kama umevua gamba la kufikiri umezaliwa kutafuta hela, madaraka, mali na vitu vingine vinavyokupa nguvu ya kuwatesa wengine. Unaanza kuyaona maisha kwa jicho pana la uanajamii. Hufanyi wema kupata sifa (esteem) na kujikusanyia mamlaka yanayokusaidia kuwadhibiti wengine (power and control) bali kutafuta ustawi wa utu (humanity) katika upana wake.
Hayo sasa ndio yanaitwa mafanikio. Unaliishi kusudi, ambalo kwa asili yake ni kuwapa watu kile ulichonacho na hicho ndicho kinachokupa utoshelevu. Huna cha kukutosha na bado unaweza kutumia kidogo ulicho nacho kumpatia mwenzako. Hatua hiyo haifikiwi kwa kujikusanyia vitu maana, kwa hakika, inaanza na badiliko la ndani yako. Usipobadilika nafsi yako, hakuna kitu utapata kikakuletea ule utoshelevu (utulivu) wa nafsi.
Unaweza kuwalea watoto wakawa na huo utoshelevu usiotegemea vitu. Unawafanya wajisikie salama, wajisikie hawana haja ya kuupambania upendo wako kama mzazi. Unawafanya wajikisie huru kuuishi uhalisia wao bila hofu ya kukosolewa, kuhukumiwa na kukataliwa. Hili linawezekana kwa kujenga mahusiano na watoto. Kuwasikiliza. Kuwakubali vile walivyo kutambua utu wao hata pale unapowarekebisha na kuwaongoza kuwa watu bora zaidi. Ukifanya hivyo, unawapunguzia kazi ya kutumia maisha yao yote wakipambana na tishio la usalama wao, njaa ya mahusiano, njaa ya kutambuliwa, njaa ya kuwamiliki wengine, hali itakayowafanya wawe watumwa wa mahitaji yao kwa sehemu kubwa ya maisha yao.
Utoshelevu wa mtu (contentment) huanza utotoni wakati ambao huna chochote kinachowavutia watu kwako. Wakati ukiwa mtoto uchi, bila elimu, mali, umaarufu, huo ndio wakati wa kujenga misingi ya utoshelevu utakaoamua kiwango cha utulivu na ustahimilivu wako kwa safari nzima ya maisha. Shughuli inaanza na namna familia inavyokupokea, inavyokufanya usijisikie kusikika, kuonekana, kueleweka bila kukufanya ujione hutoshi.
Utoshelevu wetu unaletwa na thamani tunayoiona ndani yetu hata tusipoambiwa na mtu kuwa tuna thamani. Utoshelevu ni kazi inayoanzia ndani ya mtu na sio matokeo yanayoletwa na kinachotokea nje ya mtu. Naomba urudie setensi hiyo. Utoshelevu ni matokeo ya kujiona unatosha hata kama ulivyonavyo visipokuwepo na unavyovitaka visipopatikana. Utoshelevu ni ile furaha na amani unayokuwa nayo kabla hujakutana na yeyote mwingine.
Hali hii, kwa kiasi kikubwa, inategemea mazingira ya kimalezi uliyokutana nayo miaka ya mwanzo ya maisha yako. Ikiwa bahati mbaya uliwekewa mazingira ya kupambania mahitaji yako ya msingi yanayokujenga ujione mtu, ikiwa muda wote ilibidi ulie, ugombane kusikika na kueleweka, utoto wako ulisongwa na upweke wa kutokueleweka, kuonekana na kusikika, ni vigumu mno baadae ukawa mtu mwenye utoshelevu wa ndani hata ungepata vingi.
Ukikosa hiyo thamani ndani yako, kishunuzi utajielekeza kwenye vitu ili kujihakikishia heshima. Unaweza kufikiri, kwa mfano, nikifaulu basi watu wataniheshimu. Unafaulu unakuwa wa kwanza darasani lakini unakuja kugundua wala haikupi huo umuhimu ulioufikiri ungeupata. Unasoma shahada ya kwanza ile ngumu ngumu ukifikiri watu watakuheshimu. Unamaliza wanakuuliza ulisoma chuo gani. Unagundua shahada pekee haitoshi bali jina la chuo kilichokutunuku shahada yako. Unasoma shahada ya uzamivu ukifikiri sasa watu watakuelewa. Wasiopenda amani wanakuja kukuuliza,
“Mbona tafiti zako unachapisha kwenye majarida ya kitapeli (predatory)?”
“Mbona maandiko yako hayana jipya?”
“Mbona hunukuliwi?”
“Mbona huna miradi inayofanana na uzamivu?”
Unavurugwa maana sasa kile ulichofikiri kinakuja na utoshelevu hakikuhakikishii heshima uliyofikiri ungeipata ukiwa nacho. Unielewe. Hoja hapa sio usisome. Hoja ni tatizo la kusoma kama nyenzo ya kukupa utoshelevu.
Mwingine anatafuta kuongeza thamani yake kwa pesa. Unafikiri ukiwa na mali basi watu watakunyenyekea. Unagundua wapo wengi wanakuzidi na wewe wala huonekani kwenye mazungumzo ya mafanikio. Unaanza kupambana si kuwa na mali bali uwazidi wenzako wote angalau na wewe uonekane. Unaanzisha mradi wa kujitengenezea himaya na umaarufu. Unachokuja kugundua, baadae ukishafanikiwa, ni kuwa wengi wanakufuata kupata ulichonacho. Unaanza kuhisi badala ya kuwatumia watu, wewe ndiye unayetumika. Ule utoshelevu uliofikiri unakuja na mali huupati. Unajisikia ombwe. Unakuwa mwenye mali na power lakini ndani kwa ndani ni mnyonge.
Kufikiri wingi wa vitu huja na heshima ni kujitengenezea mazingira ya kutokuridhika daima. Kufikiri heshima inayotoka nje ndiyo inayokuhakikishia thamani na utulivu wa ndani ni kujitengenezea mazingira ya kuwa mnyonge wa kudumu. Kwa nini? Hukuanza kushughulikia unyonge wa ndani yako kwanza kabla ya kupata hivi vingine.
Habari njema ni kwamba, wakati wowote, katika hatua yoyote ya maisha yako, unaweza kuchukua hatua ya kujenga ile thamani yako isiyotegemea elimu uliyonayo, mali uliyonayo, madaraka uliyonayo na umaarufu ulionao. Ukishaanza kuridhika na wewe, ukajifurahia bila kutegemea kibandiko chochote kile cha kijamii, nakuhakikishia hivi vingine vyote —pesa, elimu, madaraka, umaarufu—havitakusumbua. Utavipata na kuvikosa lakini ndani hako utakuwa na utoshelevu.
Ukiondoa elimu, ulikosoma, taaluma ulizosomea, kazi, mahali unakofanya kazi, mali, mamlaka na cheo ulichonacho, watu uliojitambulisha nao, unabaki na nini kinachopambanua vizuri utambulisho wako na kukupa utoshelevu? Wewe ni nani ukiacha vibandiko hivi?
Ukiweza kujisikia mtu wa thamani, mtu wa maana, mwenye furaha, mwenye utulivu na amani, bila kujishikiza mno na hivi vibandiko tunavyojipachika baada ya kuzaliwa, wewe kwa hakika ni mtu ukiyekutana na wewe, unayemfahamu ‘wewe’, unayeheshimiana na wewe, unayejitambua, uliyefanikiwa na kwa hakika, utakuwa mtu mwenye utulivu unaokupa utoshelevu katika maisha.
Ukiupata utulivu huo, mshunuzi Abraham H. Maslow anakuita ‘self-actualized’ hata kama huna chochote kinachoonekana. Katika utulivu huo unakuwa mtu mwanana, asiye na mashindano, asiyejitanguliza yeye na maslahi yake, asiyeteseka kujikweza aonekane, na hivyo unakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuipa dunia kile ulichopaswa kuipa. Carl Rogers angesema hapo unakuwa unaliishi kusudi lako na hayo ndio maisha yenye utoshelevu (fully-functioning person).
Hivi ni kwa nini unaweza kuwa na madaraka, elimu kubwa, vitu vingi na utajiri mwingi na bado hujisikii kuridhika? Kwa nini watu wanaweza kukutazama kwa macho ya nje kama mtu ‘anayejitosheleza kwa kila kitu’ lakini ndani ni mtu mwenye ombwe la kutaka usichonacho? Utoshelevu katika maisha —contentment—unakujaje? Je, masikini nisiyejua nitakula nini baadae naweza kuwa na utoshelevu unaonisukuma kuwafikiria na wengine wasio na chakula kama mimi? Wengi wetu tunafikiri ili niweze kumfikiria mwenzangu, niwaze ustawi wa mwenzangu, lazima kwanza 'nijitosheleze' kwanza mahitaji yangu. Je, hili ni kweli? Hapa nakupa mtazamo wa kishunuzi.
Ingawa kimaumbile upo ukweli kuwa mwanadamu ana mahitaji yake ya msingi yanayomsukuma kujitanguliza na kujipigania kwanza, lakini ukimtazama kama sehemu ya kundi, unaona mwanadamu ni kiumbe ambaye ustawi na usalama wake unategemea pakubwa namna anavyoshirikiana na wengine. Ustawi wetu kama kundi hautegemei namna tunavyoshibisha ubinafsi wetu bali uwezo wa kufikiria mahitaji ya wengine. Hili linaanza tangu tunapozaliwa. Usalama wetu wa kisaikolojia unategemea namna tulivyo karibu na mama, familia, watoto wenzetu na baadae jamii inayotuzunguka.
Ushirikiano na watu wanaotuzunguka ni hitaji la kimaumbile na halina uhusiano wa moja kwa moja na wingi wa vitu vinavyokidhi mahitaji yetu binafsi. Abraham H. Maslow, mshunuzi wa utoshelevu, alifikiri kuna mahitaji ya msingi ni muhimu yapatikane ili mtu aweze kupanda ngazi katika safari ya kuushinda ubinafsi. Maslow alifikiri mwanadamu anakabiliana na bounding vingi vinavyomlazimisha kujifikiria mwenyewe kwanza—kimoja wapo ni uhakika wa mahitaji ya kila siku ambayo ukiyakosa wachumi wanakuita maskini. Mfano ni chakula. Kuna ukweli kuwa ni vigumu mwenye njaa kufikiria njaa ya mwenzake. Njaa itamkumbusha kujipambania. Hata hivyo, kama sehemu ya kundi, kuna ukweli unaweza usiwe na vingi na bado macho yako yakafunguka kuona uhitaji wa mwingine.
Kinachokusukuma kuona uhitaji wa mwenzako ni nini? Kushiba chakula kwanza? Hapana. Mshunuzi Harry Harlow alikuja kugundua baadae kuwa ni ile shibe ya nafsi inayokufanya ujisikie salama, ujione ni sehemu ya mnyororo wa mahusiano na watu wengine, unayewajibika na ustawi wa mwenzako. Ukilikosa hili, unakuwa kama mtu anayeishi kwenye umasikini wa kutisha unaokufanya muda wote uwaze namna ya kuwazidi wenzako na kupata zaidi na zaidi na zaidi na kwa hakika hutofika mahali ukajisikia kuridhiki na chochote ulichonacho kama hakikupi mamlaka (power and control) vya kutosha. Unakuwa na maradhi ya nafsi mufilisi isiyoweza kutulia wala kuridhika. Unakuwa mtu mwenye kila kitu lakini unataka zaidi. Huwezi kuwa hivi na ukasema umefanikiwa— ‘self actualized.’
Tunagombanishwa na tafsiri za mapenzi. Unachoamini ni mapenzi kwa mwenzako kinaweza kuwa kitu kingine na kikachokoza matatizo. Kuna mtu mapenzi ni kukumbushwa furaha ya utotoni. Mwingine mapenzi ni kusahaulishwa huzuni ya utotoni. Kuna mtu humpenda mpenzi anayefukia hasira zake za migogoro ya utotoni. Mwingine humpenda anayemhakikishia usalama aloukosa utotoni.
Mwingine humpenda anayeziba ombwe la uhuru. Kwake kumfuatilia, kuingilia faragha yake ni wivu sio mapenzi. Mwingine mapenzi ni kupata mtu wa kutosha kuziba ombwe la kukosa mamlaka na sauti ya kumuelekeza. Unachokiona ni ‘utumwa’ na kukosa faragha kwako hayo ndio mapenzi na unapompa uhuru maana yake hujali.
Mwingine ukimfanya asikike na aeleweke anaona unamthamini. Kazoea ukaribu, kueleweka na mazungumzo ya wazi yasiyoacha makisio. Usiposema wazi unataka nini anakuona ‘toxic’. Mwingine ukimfanya asikike na aeleweke anakuchoka. Kwake mapenzi ni drama za kuviziana. Hasemi anachotaka. Anakulaumu kwa asichosema. Ukimpenda basi ujifunze kujua anataka nini bila kuambiwa. Usipojua asichokuambia humpendi.
Migogoro yetu mingi ni kutumia tafsiri zetu binafsi kwa wenzetu. Tunafikiri tunachokitaka sisi ndicho wanachokitaka wenzetu. Mapenzi, kwa hakika, ni kuelewa na kuiheshimu tafsiri ya mapenzi kwa mwenzako. Tunapofanya hivyo, mapenzi yanakuwa fursa ya kujifunza mengi yanayotibu makovu tulowahi kupitia.
Unaachana na mpenzi anayekutesa, una-move on kukutana na mwingine kama huyo na kumzidi hatimaye unatulia kwa ‘konki’ anayekuumiza kwa ustadi zaidi kuliko waliopita na huwezi kumwacha kirahisi.
Kuna muda mapenzi ni safari ya kutafuta watu wanaotufanania au kuyafanania matatizo yetu. Tunawapenda wenye kitu kinachotusaidia kusahau ombwe linalotusumbua na kisha tunatulia kwa wanaosumbuliwa na kile kile tulichokizoea.
Mahusiano yanayokua polepole,
Mahusiano yasiyoanza na ‘mlipuko’ wa mapenzi,
Mahusiano yasiyoharakisha ngono,
Huwa na uwezekano mkubwa wa kudumu.
Wapenzi wanaojipa muda kufahamiana,
Wapenzi wasioharakisha ‘kuaminiana’,
Wana uwezekano mkubwa wa kuoana, kuridhika na kudumu zaidi katika ndoa.
Haraka haraka, tafiti zinasema, huleta kuteleza.
Haraka haraka hunyima umakini,
Haraka haraka kuleta kizaa zaa.
Ukiweza kutofautisha hisia za ngono na mapenzi uwezekano wa mahusiano unayoyaanzisha kudumu unakuwa mkubwa. Hisia za ngono, tamaa, ni msukumo wa kimwili unaowachochea wanyama kuzaliana. Nzi, pamoja na udogo wake anazo hisia hizi—sexual instincts—ingawa hana mapenzi.
Hisia za ngono (tamaa) zikiwa kipaumbele chako, vigumu kuwekeza kwenye mahusiano yanayokutanisha fikra na kuruhusu mikinzano ya mawazo kujenga utambulisho wa pamoja—intimacy. Ukaribu wako na mtu, aghalabu, utalenga kukutanisha miili kuliko fikra, imani na mambo yanayowatambulisha (identities). Utavutiwa na mwonekano, utamtamani, ukifanikiwa kukidhi tamaa za mwili hisia hizo zitapoa. Usipozimudu hisia hizi, kama ilivyo kwa nzi, unaweza kucheza na wengi kwa mpigo—maana huwapendi.
Mapenzi, tofauti na hisia za ngono, ndizo zinatutofautisha na wanyama wengine. Ukimpenda mtu unahamia kwenye fikra, imani na misimamo yenu. Upendo unakuchochea kuweka mazingira ya kumwamini, kumfanya kuwa sehemu ya faragha yako, na hivyo unampandisha ngazi ya kumruhusu kukufahamu, kuyafahamu matumaini yako, kuzijua aibu zako. Upendo unakuchochea kujitoa ili kumheshimu, kumstahi na kumfanya kuwa sehemu ya maisha yako.
Ukaribu wa kiwango hiki ndio unaochochea muunganiko wa utambulisho wenu (identity) ili kuufanya kuwa mmoja. Huo ndio upendo unaodumu, kwa mujibu wa mshunuzi Sternberg. Ingawa uwezo huu anao mwanadamu, ukishakosa upendo wa mzazi utotoni, inaweza kukuwia vigumu mno kumpenda mtu mwingine au hata kumruhusu mtu mwingine akupende kwa kiwango hiki. Katika mazingira kama haya, watu wengi huishia kwenye hisia za ngono, na uwezekano wa ajali nyingi za mahusiano unakuwa mkubwa zaidi.
Tunawafahamu wale watu wema ambao kuomba msamaha ni kama sehemu ya maisha yao. Hawaoni haya kukubali wamekosea na hawapati utulivu mpaka myatengeneze. Pia wapo wale wenzao ambao Ingawa inaweza kuwasumbua kukiri makosa lakini huona bora wavumilie fedheha ya kuonekana wamekosea kuliko kuupoteza uhusiano.
Halafu kuna wewe hapo ambaye kuliko kumsikiliza mtu anayelalamikia tabia zako na kuomba msamaha bora urafiki ufe. Huamini kabisa kuwa binadamu mwenzio anastahili kuombwa msamaha hata kama kweli unajua umekosea. Tena mtu asipoangalia anaweza kuishia kuomba msamaha kwa kukuambia ulimkosea. Happy Valentine kwako :)
Hatia ni nguzo muhimu ya malezi yanayokuza mtu mwenye utu na dhamiri hai, muhimu yasiwepo mazingira ya mtoto kufedheheka. Hatia, kwa kawaida, haifanyi kazi penye upweke, penye tishio la usalama, na uhaba wa uhusiano wa mtoto na mzazi/mlezi.
Usiombe binadamu apoteze uwezo wa kujisikia hatia. Ukishaacha kujisikia hatia unakuwa sawa na wanyama wengine wasio na dhamiri. Hatia, kimaumbile, inaturudisha kwenye wajibu wa kuutafakari mstari unaotenganisha mema na mabaya. Unapojisikia hatia maana yake dhamira yako inakushtaki kwa kufanya maamuzi unayojua si sahihi—mf. umemwuumiza mwezako, hujatenda haki nk—na huu ndio msingi wa uadilifu wa mwanadamu.
Hatia ni somo muhimu tunalolipata utotoni kupitia mahusiano yetu na wazazi. Kwa kawaida, hatupendi kuwakosea wazazi/walezi wetu. Tunawahitaji. Tunauhitaji upendo wao. Tunapokemewa kwa kukosea, kwa mfano, tunajisikia hatia. Tunajirudi. Hatupendi kupoteza uhusiano wetu na watu muhimu kwenye maisha yetu. Tunajifunza kujisikia aibu kwa matendo yetu yasiyopendeza. Hata hivyo, wapo wazazi huenda mbali na kutudhalilisha mbele za watu muhimu kama namna ya kutuonya. Hawa, kwa ukali wao, ukatili, hasira huenda walituchapa na kututukana tukajifunza hisia nyingine inayoitwa fedheha.
Unapofedheheka, aghalabu unaanza kuwa na wasiwasi na utu wako. Unapoteza kujiamini kwamba wewe ni mtu anayestahili heshima. Unaanza kujihoji namna watu wanavyokuona. Unaanza kujidharau. Unagundua hakuna kitu utafanya kikakubalika. Unapoteza matumaini ya kumridhisha mzazi. Unaanza kukosa kitu cha kupoteza. Mawili yanaweza kutokea. Kwanza, uwe mpweke asiyeamini ana lolote la kuchangia kwenye jamii ingawa unapotelea kwenye sonona. Pili, uwe jitu katili lisilo na dhamiri tena.
Hili la pili likitokea unakuwa sawa na watu walikosa ukaribu na wazazi/walezi wenye upendo uliowakumbusha haja ya kujisikia hatia. Hawa hawakupendwa, waliishi katika upweke na tangu utotoni hawakuwa na watu waliowapenda na kuwafanya wajikie wana kitu cha kupoteza. Hawa, aghalabu, huishia kuwa watu wazima wasiojisikia hatia wala fedheha. Hawa ni watu waliopoteza dira inayoamsha dhamiri. Hawa hugeuka kuwa watu wakatili wanaoweza kufanya uovu dhidi ya binadamu wenzako na hawajutii. Hawa, wakipata nafasi na madaraka, wanaweza kukuumiza na wakategemea uombe msamaha kwa kuwachokoza.
Utu uzima unakuja na mengi. Kuna shinikizo la kazi. Kuna kupambana na ndoto. Kuna vita ngumu za kuongeza kipato. Kuna mipango kutetereka. Kuna kuishiwa. Kuna muda na familia. Kuna migogoro isiyosemwa. Kuna kujitafakari kunakohitaji kujitenga. Kuna kupumzika. Mtu wako wa karibu kutokupatikana haimaanishi hakujali.
Utu uzima pia hubadilisha mazungumzo. Kila unachokisema kinamkumbusha mtu historia fulani. Maumivu alo’wahi kupitia. Usaliti alo’wahi kukutana nao. Kuna imani zisizobadilika. Kuna tabia mtu anapambana nazo bila mafanikio. Kuna ndoto kubwa na mipango isiyotimia. Kuna hatia. Ombwe. Unyonge. Mtu kuamua kukuweka pembeni haimaanishi hakupendi.
Kijana unayefanya kazi kwa mazoea, usiyeona haja ya kujifunza mambo mapya, unayeamini unajua kuliko wanaokutangulia, huna nidhamu ya kazi, unachelewa kazini, unaondoka muda unaotaka wewe, huheshimu makataa (deadlines);
…kumbuka kuna wakati utafika wenzako wa umri wako na elimu kama yako wataaminiwa kwa majukumu makubwa zaidi wakati huo wewe ukipambana na ‘roho’ ya kukataliwa na kulalamikia kila mtu ukiamini hakupendi na hawakutakii mema.
Walter Mischel, mshunuzi maarufu aliyepata kuwa pia mwalimu wa Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani anaweza kuwa na mawili matatu kwako unapotafakari namna utakavyoanza safari yako ya kumamilisha malengo yako kwa mwaka 2026.
Miaka ya 1970, Walter Mischel alifanya utafiti unaoendelea kuthibitika duniani kote kuonesha kuwa subira —uwezo wa kudhibiti mihemuko (tamaa ya macho, hisia) ndio siri kutimiza małengo. Unaweza kujifunza zaidi kwa kupitia Marshmallow experiment, au delayed gratification mtandaoni.
Mischel aliwatumia watoto wa miaka minne, wengi wakiwa watoto wa walimu wa chuo hicho. Kawagawia kijikeki kinachoitwa Marshmallow, hapa kwetu ingekuwa labda pipi kijiti au chochote mtoto anakipenda. Mischel anawapa agizo rahisi, “Naondoka kidogo. Ukiweza kusubiri nikarudi ukawa hujaila nikaikuta, basi nitakupa ya keki ya pili.”
Marshmallow ya pili ilikusudiwa kuwa ‘zawadi ya ushindi’ kwa maana ya kuutambua uvumilivu wa mtoto. Hata hivyo, ikiwa mtoto angeila, haidhuru, lakini mtoto asingepata zawadi ya keki (marshmallow) ya pili. Mischel anaondoka baada ya kuhakikisha mtoto ameelewa maelezo hayo, anarudi baada ya dakika kumi na tano.
Ukisema, “mwanaume anapenda kuheshimiwa na hakai kwenye nyumba isiyo na amani,” unakuwa na maana gani? Kwamba mwanamke anapenda kudharauliwa na haoni shida kuishi kwenye nyumba yenye vurugu?
Kwa nini tusiseme binadamu anapenda mahusiano yenye amani na kuheshimiana? Kwa nini tunapenda kutia jinsia kwenye sifa ambazo kila binadamu timamu anazihitaji?
“Mwanaume anapenda mtu msikivu”
“Mwanaume anataka mtu muelewa”
“Wanaume hatupendi kufuatiliwa fuatiliwa”
Tunahitaji heshima. Wote.
Tunahitaji amani. Wote.
Tunahitaji kueleweka. Wote.
Fikiria vizuri kabla hujatia jinsia.
Katika eneo la ujifunzaji, 2025 umenikutanisha na maarifa mengi kupitia waandishi mahiri. Ingawa nimesoma vitabu vingi (30+) kupitia Club mbalimbali za usomaji (Tusome na Uongozi Dodoma), hivi 12 vimenigusa zaidi kitaaluma, kiutendaji na kiuelewa.
Ukisoma ninachokiandika, mara kwa mara humu, unaweza kupata muhtasari wa maudhui ya vitabu hivi kwa lugha yangu ya kishunuzi. Hata hivyo, kwa faida ya msomaji anayetafuta kitabu kizuri kwa mwaka tunaouanza, nitapitia kimoja baada ya kingine.
Shukrani sana kwa @UONGOZI kwa vitabu vingi nilivyoazima, kuvisoma na kuvijadili na wenzangu kupitia mijadala ya Dar es salaam na Dodoma.