Umewahi kuzungumza na mtu kitu cha kawaida, tena kwa nia njema, unashangaa hali inabadilika ghafla? Unajiuliza, nimekanyaga wapi? Watu wanauguza majeraha mengi ya kihisia. Unachokisema kinachokoza historia fulani inayomkumbusha mtu maumivu aliyopata kupitia. Mazungumzo ya kawaida ya kufahamiana yanatafsirika kama ‘unanichimba’, ‘unatafuta nini’ wakati maswali ya kawaida kabisa kwa mtu anayejiuguza yanasikika kama ‘huniamini,’ ‘unanisimanga’, ‘unanishambulia.’
Unapozungumza na mtu anayejiuguza, kila neno linapitishwa kwenye kidonda cha vita ngumu ya ‘mwenyewe kwa mwenyewe’ inayomkumbusha hofu za kuwahi kukataliwa, hasira za kuwahi kutokueleweka na hata kisasi kisichozungumzwa wazi wazi. Wewe unazungumza maneno lakini mwenzako anasikiliza ‘filamu’ ya maumivu anayojiuguza nayo. Wewe unatania lakini mwenzako anasikia kejeli, masimango, unyonge na dharau.
Watu wanacheka lakini wanajiuguza na mengi. Watu wamechangamka lakini wanauguza mengi. Jifunze kusikiliza zaidi kuliko kuzungumza. Uliza maswali yanayompa mtu nafasi ya kuzungumza mwenyewe. Usilazimishe kuelewa haraka kila kitu kwa mtu. Usichokielewa, huenda kimebeba kipande cha maisha yake anachotamani kukisahau. Kumbuka hata wewe kuna kitu unajiuguza nacho ndio maana unauliza usichotakiwa kuuliza, unazungumza usichotakiwa kuzungumza na unataka kuelewa usichotakiwa kukielewa.
“Ukizaliwa kwenye familia inayopendana na kuheshimiana mshukuru sana Mungu,” ananiambia Debora. “Sisi wengine tumezaliwa kwenye familia ambazo hata kuzungumza kitu kikaisha hamuwezi. Ukijaribu kuanzisha mazungumzo muhimu kurekebisha kitu kwa nia njema kabisa, anayetarajiwa kusikiliza mjadiliane ndio kwanza anajiandaa kujibu mapigo. Hasikilizi. Chochote unachosema anakitafsiri kama shambulio. Mazungumzo hayaishi vizuri.”
Debora anazungumzia kushindwa kuwasiliana kwa uwazi kama mfano wa tabia za familia mparaganyiko (dysfunctional families) ambazo aghalabu ni matokeo ya matatizo ya wazazi kitabia—mfano ulevi uliokithiri, uraibu wa aina mbalimbali na hata vilema vya haiba (personality disorders)—yanayohama kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine na hivyo kuchochea migogoro isiyoisha kwenye familia.
“Hizi familia zetu haziamini katika uwezo wa mtu kufanya maamuzi. Tangu unakua hupati nafasi ya kujifunza kuamua. Maisha yako yote yanakuwa chini ya mamlaka ya mtu anayeamua kwa niaba yako na ndiye anayefuatilia unachotakiwa kuamua maana anaamini anajua unatakiwa kuamua nini,” anasema Debora. Tabia hii ya kuingilia mno uhuru wa mtu binafsi kwa nje inaweza kubeba sura ya ukamilifu na utii usiohojiwa kwa mamlaka ya familia lakini inajenga hofu, hasira na chuki zisizosemwa wazi wazi.
“Fikiria kuna mtu anaamua usome nini na wala hahitaji kukusikiliza wala kukuelimisha. Hili wala halifanyiki kwa kuzungumza na kujaribu kuelewa mahitaji yako. Unafanya kupewa maagizo na kazi yako ni kutekeleza. Inachosha sana maana inakuwa kama mzazi anakutumia wewe kutimiza ndoto alizoshindwa kuziishi yeye. Inafikia hatua mbaya hata maamuzi binafsi ya ndoa huna. Kila kitu kiko controlled (kinaamuliwa) na mzazi.”
Debora ananiachia jambo linalofikirisha. Kwa nini mzazi ufikiri unaweza kudhibiti maamuzi ya mtoto kwa kiwango hiki? Je, malezi hasa ni nini? Unapoishi kwenye familia ya namna hii unafanyaje kulinda amani ya familia? Je, unapuuza utashi wako binafsi ili uwe mtii kwa mamlaka za familia? Je, ninwakati gani unachora mstari kuwa hili ni uamuzi wangu hata kama familia haiuelewi? Je, ni sahihi kuasi utamaduni wa sumu unaoshikilia familia mparaganyiko (dysfunctional family)?
“Mwezi huu ukiisha nitakuwa nimekamilisha mwaka sijazungumza kabisa na mtu yeyote wa familia yangu,” ananiambia Jonas, mtoto wa kiongozi mmoja wa dini hivi karibuni mjini Iringa. Jonas ni kijana wa miaka thelathini anayeonekana kuwa mchangamfu ingawa ni mtulivu kwa haiba.
Tunazungumza mengi kama sehemu ya maandalizi ya ndoa anayotarajia kuifunga mwakani. Namwuuliza kwa nini hasa hawasiliani na familia yake? Jonas anaonekana kukumbuka mengi. Nampa nafasi ya kujituliza kisha anaukunjua uso wake, “Nimechagua kuanza maisha mapya nje ya mzunguko wa sumu ya familia.”
Jambo hili linaweza kukushangaza ukilisikia kwa mtu. Simulizi la Jonas linastuka kidogo. Ukilisikia rahisi kumwona kama mtu mwenye matatizo. Hata nadharia nyingi za ushunuzi (psychology) zinakubaliana kuwa mtu timamu aghalabu ni matokeo ya uhusiano na familia yake mwenyewe na kwamba kuhusiana kwa karibu na familia ndio msingi wa utu wa mtu.
Katika jamii nyingi, mtu anayejitenga na familia yake anachukuliwa kuwa tatizo, “Unawezaje kuwatupa watu waliokuzaa?” Tunayo hadi misemo mingi inayosisitiza umuhimu wa familia, “Damu nzito kuliko maji,”
“Damu ya familia haimwagiki”,
“Mzazi ni Mungu wa pili duniani” na misemo mingine mingi inayotukumbusha kufungamana na familia.
Je, ni wakati wote tunalazimika kulinda uhusiano na familia? Vipi kama familia yako ni chanzo cha matatizo yanayokusumbua? Jonas ananikumbusha nadharia ya ‘uhuru wa nafsi’ kama alivyoieleza mshunuzi mtata, Carl Jung.
Ukifanya vizuri utajua hata kama hakuna mtu amekupongeza. Kuna ile unasikia kale kafuraha kanakoambatana na ka-ufahari kanakoleta changamko fulani hivi baada ya kufanya kazi nzuri. Unatazama kitu kizuri ulichofanya unajipongeza mwenyewe na wala hulazimiki hata kuonesha sana kile ulichofanya. Utoshelevu ndio huo sasa kwamba umefikia pahala unaweza kuridhika kuwa umefanya vizuri hata kama wengine hawatambui.
Ukishaanza kuona una ule msukumo usio wa kawaida wa kuonesha, kuonekana, kutambuliwa, kusifiwa, kupongezwa na inakuwa kama hujisikii utoshelevu mpaka watu waone ulichofanya, wasifie kwa vile unataka uzidi, uonekane bora kuliko wengine, hapo kuna shida ya ombwe. Ukishakuwa na ombwe, kwa kawaida, unaanza kuona kama vile haitoshi kufanya vizuri mpaka ushangiliwe.
Kusifiwa si vibaya. Shida ni pale unapotaka sana kukubalika, kuonekana na kusifiwa na huoni thamani ya unachokifanya mpaka watu waseme. Karen Horney, mshunuzi nguli wa haiba, anaita hali hii #NeuroticNeed —unakuwa unataka kitu sahihi (kusifiwa kwa mfano) kwa lengo la kushibisha ombwe la haiba. Utajikuta kila unachofanya ni kwa ajili ya watu. Shida inaanza pale ambapo hao unaokusukuma kufanya unachofanya hawaonekani kutambua, hawana habari na wala hawajali. Utaumia.
Kuna yule ‘wewe’ wa hadharani unayemtengeneza aonekane na kukubalika na watu—yule ‘wewe’ mkamilifu, asiye dhaifu, anayejua anachotaka, ‘wewe’ aliyejipata na kujitosheleza; ‘wewe’ msomi, mjuzi wa mambo, mwenye busara na maarifa; ‘wewe’ anayejituma, mwenye bidii ya kazi; ‘wewe’ mkarimu, mwenye upendo, usiye na matatizo na watu; ‘wewe’ mwenye utu na huruma na watu, ‘wewe’ mtetezi wa wanyonge, mpenda haki, asiyependa watu kuonewa, ‘wewe’ mcha Mungu, anayemtanguliza Mungu kwa kila jambo.
Halafu kuna yule ‘wewe’ wa faragha usiyependa afahamike sana na watu—‘wewe’ mbinafsi, mwenye husda, anayeweza kufanya chochote kupata anachotaka; ‘wewe’ anayeteseka na tamaa, asiyeweza kupenda, anayehangaika kupokea upendo na asiyeacha kugombana na watu wema; ‘wewe’ mnyonge, mlalamishi, mbabe, ‘wewe’ aliyekata tamaa; ‘wewe’ asiyejiamini, asiyejipenda, asiyejisamehe, anayejichukia na kutafuta huruma;
Tofauti kubwa kati ya ‘wewe’ wa faraghani na huyu ‘wewe’ unayetuletea hadharani ndiyo inayochangia matatizo yako mengi kitabia. Huna amani na uhuru kwa kuishi maisha yako kwa vile unajua fika kuwa ‘wewe’ unayetuletea hadharani hafanani hata kidogo na huyo wewe unayemjua sirini. Una hasira na kisasi na watu wema wasio na shida na wewe, unagombana na watu ambao kimsingi walipaswa kuwa rafiki zako, kwa vile watu hawa saa nyingine bila kujua wanamchokoza ‘wewe’ asiyependa afahamike na watu.
Ukitembelea hospitali unajifunza kumbe uhai na afya njema katika ujumla wake huo ndio msingi wa mengine yote. Ukishakuwa kwenye mazingira yanayotushia uhai wako, ukawa kwenye mazingira unayolazimika kupigania uzima wako, huwezi kuzungumzia chochote kinachoitwa maendeleo.
Kadhalika, ukitembelea magereza unajifunza kumbe uhuru ndio maendeleo halisi ya mwanadamu. Ukishakuwa kwenye mazingira ambayo huwezi kwenda mahali kufanya lolote na yupo mwenye mamlaka ya kukupangia ukutane na nani, uzungumze na nani, ratiba yako ya siku iende vipi huwezi kuzungumzia chochote kinachoitwa maendeleo.
Maendeleo, kwa hakika, ni hakikisho la uhai. Hatua ya kwanza ya mtu kujikwamua na umasikini ni haki yake ya kuishi. Maendeleo ni uhuru wa watu. Ukishaukosa uhuru wa kwenda unakotaka, ukaukosa uhuru wa kuwa binadamu mwenye hiyari kumaanisha akawepo mtu anayedhibiti fikra zako, maoni yako, maamuzi yako, unakuwa mtumwa na, kwa hakika, huwezi kusema wewe ni mtu mwenye maendeleo.
Mkutano wangu na waandishi wa habari niliokuwa nifanye katika Hotel ya Golden Tulip nimeuahirisha.
Nimesikiliza hotuba za Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu. Wameeleza vizuri kuhusu uvumi na upotoshaji uliokuwa ukifanyika juu yangu na misimamo juu ya chama chetu.
Nimedumu katika mapambano haya kwa zaidi ya miaka 22. Nimeenda lock-up zaidi ya mara 50. Nimezunguka nchi hii usiku na zaidi ya mara tatu. Nimewahi kuwa magerezani mara kadhaa, nimekoswa kuuawa zaidi ya mara tatu, na nimewahi kukimbia nchi.
Katika yote haya, nimekuwa nikitoa sadaka kubwa kwa ajili ya mapambano haya, ikiwemo ku-sacrifice familia yangu mara zote.
Kazi hii kwangu si ajira, si cheo, wala si njia ya kujitafutia maslahi. Ni huduma. Ni wito. Ni kama injili ninayoamini na kuitumikia.
Kwa hiyo, siwezi kuruhusu uvumi, upotoshaji au tafsiri za watu kuniondoa kwenye misingi ambayo nimeisimamia kwa zaidi ya miongo miwili.
Nitakuwa kwenye mapambano haya kwa imani, ujasiri na dhamira njema siku zote.
Dunia ina idadi kubwa ya watu wasio na shida na wewe, na wala hawana mpango wa kugombana na wewe, ikiwa utawahakikishia kuwa wewe ni wa kawaida, nyonge, huna mbele wala nyuma na mwenendo wa mambo unaonesha kuwa utaendelea kuwa chini.
Katika biblia, kwa mfano, tunasoma habari za Yusufu mwana wa Yakobo, kijana wa tofauti aliyesimulia ndoto zake zilizoonesha kuwa ana kitu kinachomtofautisha na ndugu zake. Ingawa Yusufu hakusimulia kwa nia ya kujionesha, matatizo yake na ndugu zake yalianzania hapo ndoto zake zilipowatia unyonge ndugu zake.
Kosa kubwa unaloweza kufanya na likakugombanisha na watu usiowatarajia ni kuonesha kuna kitu Mungu ameweka ndani yako kinachokutofautisha na wengi, na kwamba upo uwezekano wa kufanya yale ambayo wengi wanatamani kuyafanya lakini, kwa sababu mbalimbali, hawawezi kuyafanya.
Ikiwa hujajiandaa vizuri kupambana na chuki, saa nyingine kutoka kwa watu wa karibu, kuonekana ni mtu usiye na mbele wala nyuma inaweza kukuepusha na mengi. Ikiwa ni lazima simulizi la kazi unazofanya lisikike ukifanikiwa kuonesha kuwa huna mahali unaenda, uwezekano wa kujiepusha na mengi unakuwa mkubwa. Halaiki, kwa kawaida, haipendi kuona kuna mahali unasogea.
Kuna wakati nasaha, ushauri na lawama kwa mtu hazimsaidii kubadilika hata kidogo. Ukimruhusu kufedheheka, kudhalilika, kuaibika anafanya uamuzi sahihi na anabadilika bila kushauriwa.
Unaweza kuwa sahihi, unaongea jambo la kweli lakini usipojifunza namna ya kujieleza unaweza kuishia kueleweka vibaya, ukaumiza hisia za mwenzako na ukazalisha mgogoro usio wa lazima. Hapa nina mifano michache ya kuzungumza kwa namna inayopunguza migongano katika lugha:
✳️ Tafsiri, mara nyingi, ndizo zinazogombanisha watu. Ukitafsiri kilichofanyika, aghalabu unazusha ugomvi. “Umenikera” “Umenipuuza”, “Umeniumiza.”
Unaweza kusema hisia zako kuhusu jambo lililotokea bila kutanguliza tafsiri.
“Nimekasirika,” “Nimehuzunika,” “Nimeumia kusubiri muda mrefu” badala “Hujali muda wangu,” “Sijui umenionaje kuniweka muda wote.”
✳️ Ukikosa msamiati wa kusema hisia zako, badala ya kulaumu, bado unaweza kutafuta namna ya kusema hitaji lako kwa lugha chanya:
“Nilitamani sana tupate muda wa kuwa pamoja tuzungumze.”
“Nilitamani bidii yangu itambuliwe.”
Kumbuka muhimu ni hitaji hilo ulilonalo sio lawama na kumfanya mtu ajione mkosefu.
✳️ Unapozungumzia kosa alilofanya mwenzako, unaweza kukwepa kutumia lugha ya lawama, malalamiko na kumuwekea maneno madomoni. Ukisema ulichoona na kusikia bila lawama unakaribisha mahusiano badala ya ugomvi.
“Tulikubaliana turudi mapema tule pamoja. Jana umerudi saa 6 usiku.”
“Umezungumza na simu kwa dakika 40. Tulikubaliana tukutane hapa kwa mazungumzo.”
✳️ Katika mazingira ambayo mwenzako tayari anakulaumu, anakushambulia, kuliko kujitetea na kumgeuzia kibao bado, unaweza kufanya jitihada za kutambua hitaji lake. Huenda amekasirika na anahitaji tu uelewe kilichomkasirisha na mambo yanaisha.
“Unahitaji nirudi mapema nyumbani.”
“Hukupenda nilivyokujibu mbele za watu.”
Wakati mwingine hata kurudia kile tu anachokisema kwa maneno yako humfanya mtu aone unamuelewa na mapambano yanaishia hapo.
Lugha hii isiyotafuta ugomvi haikuhakikishii amani na mtu lakini angalau inakuwekea mazingira ya kutuma ujumbe kuwa una mtazamo chanya na mtu, si mgomvi, si mbabe, hujihesabii haki, humbebeshi mwenzako lawama na una staha kwa hisia za mwenzako.