Mwakilishi wa Mkuu wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena ametoa wito kwa Vijana waliohitimu kidato cha sita mwaka 2026 kutoka shule zote Tanzania Bara na Visiwani kuhudhuria Mafunzo ya JKT kundi la lazima (Mujibu wa Sheria) kwa mwaka 2026.
SUMAJKT KUWALETA WATANZANIA DODOMA
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele amewataka Maafisa, Askari, Vijana na watumishi wa umma JKT, kuwaalika ndugu, jamaa na marafiki kushiriki SUMAJKT Marathon 2026, itakayofanyika Jijini Dodoma tarehe 6 Juni 2026.
UGENI
Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele leo Machi 25,2026 Ofisini kwake Makao Makuu ya JKT Chamwino Dodoma, amepokea ugeni wa Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Amani Tanzania Brigedia Jenerali George Itang'are
Rear Admiral Hassan awataka wataalam wa Uokoaji kufanya kazi kwa weledi
Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji Rear Admiral Ameir Hassan amewataka wataalam wa Zimamoto na Uokoaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutekeleza majukumu yao kwa weledi pindi majanga mbalimbali yanapotokea nchini.
Rear Admiral Hassan ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha wataalam wa Zimamoto na Uokoaji wa JWTZ kilichofanyika katika ukumbi wa Kikosi cha Usafirishaji Mwanza (MTC) tarehe 23 Machi 2026.
Amesisitiza kuwa Mafunzo,vifaa na utayari wa kukabiliana na majanga ni jambo muhimu katika kuhakikisha wanakuwa tayari wakati wote pindi majanga yanapotokea
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kukabiliana na Majanga Kanali Juma Katunge amesema kuwa Makao Makuu ya Jeshi yameandaa kikao hicho ili kuwajengea uwezo wataalam wake na kupata uelewa wa pamoja juu ya majukumu yao.
Wataalamu wa Zimamoto na Uokoaji Jeshini wamekua wakishiriki katika Operesheni za uokozi katika majanga ya asili na ajali mbalimbali kwa kusaidiana na Mamlaka nyingine za serikali.
Kikao kazi cha wataalam wa Zimamoto na uokoaji wa JWTZ kinafanyika kuanzia tarehe 23 hadi 26 Machi 2026.
Ziara Chuo cha Taifa cha Ulinzi Makao Makuu ya JKT
Washiriki wa Kozi kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichopo Kunduchi Jijini Dar es Salaam, wameanza ziara ya siku tatu ya mafunzo kwa vitendo katika vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Dodoma, ambapo leo Machi 9, 2026 wametembelea Makao Makuu ya JKT yaliyopo Chamwino, Dodoma.
Ziara hiyo ni sehemu ya kuimarisha uelewa wa washiriki kuhusu utekelezaji wa majukumu ya vyombo hivyo katika kulinda usalama wa Taifa.
Ziara hiyo inalenga kuwezesha ulinganifu kati ya mafunzo ya nadharia yanayotolewa darasani na hali halisi ya utekelezaji wa sera, mikakati na mipango ya Serikali inayohusu masuala ya ulinzi na usalama nchini.
Katika ziara hiyo, washiriki 72 kutoka mataifa 17, ikiwemo Tanzania, wanapata fursa ya kujifunza moja kwa moja namna taasisi mbalimbali za ulinzi na usalama zinavyotekeleza majukumu yake pamoja na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa sera za usalama.
Ziara hiyo inaongozwa na Mkufunzi Mwandamizi Elekezi Jeshi la Ardhini, Brigedia Jenerali Charles Ndiege akimwakilisha Mkuu wa Chuo hicho Meja Jenerali Wilbert Ibuge, akifuatana na wakufunzi waandamizi, maafisa wanadhimu pamoja na washiriki wa kozi ya 14 ya chuo hicho.
Mafunzo hayo kwa vitendo yanatarajiwa kuwajengea washiriki uwezo mpana wa kuchambua na kutathmini masuala ya ulinzi na usalama, ili waweze kutoa mchango madhubuti katika kuimarisha usalama wa Taifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi bendera Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda katika Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo Mkoani Dodoma tarehe 24 Februari, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Waziri wa Ulinzi na JKT Mhe. Rhimo Simeon Nyansaho, ufunguo mara baada ya kuzindua jengo la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo Mkoani Dodoma tarehe 24 Februari, 2026.
Jenerali Mkunda aweka jiwe la Msingi Ujenzi wa Kamandi ya Jeshi la Akiba
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda leo Februari 12, 2026 ameweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Jengo la Utawala katika Kamandi ya Jeshi la Akiba iliyopo Manyoni Mkoani Singida.
Akizungumza na Maafisa na Askari wa Kamandi hiyo, Jenerali Mkunda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuliwezesha JWTZ kwa kutoa rasilimali fedha pamoja na vifaa ili kuhakikisha kuwa Jeshi linatekeleza majukumu yake ya kiulinzi na usalama nchini.
Aidha amewataka wanakamandi ya Jeshi la Akiba kuhakikisha Ujenzi huo unaisha kwa wakati pamoja na kutunza miundombinu ya Jengo hilo pindi litakapoanza kutumika.
Pia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Mkunda amewashukuru wanakamandi hiyo kwa jitihada kubwa walizofanya kuhakikisha Ujenzi huo unaanza kwa wakati hadi kufikia hatua iliyopo na kuwasihi kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano na jamii inayowazunguka huku akisisitiza kutunza afya zao kwani wao ndiyo nguvukazi ya Taifa.
WAZIRI WA ULINZI NA JKT AZINDUA BODI MPYA YA USHAURI YA SUMAJKT
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt, Rhimo Nyansaho (Mb), Januari 14, 2026, jijini Dodoma, amezindua Bodi Mpya ya Ushauri ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT), itakayoongozwa na Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo, aliyeteuliwa hivi karibuni na Waziri wa Ulinzi na JKT.
Mhe. Dkt. Nyansaho amempongeza Mwenyekiti na wajumbe wapya kwa kuteuliwa katika Bodi ya Ushauri ya SUMAJKT na kusema kuwa, SUMAJKT limepiga hatua kubwa na nzuri katika miaka ya hivi karibuni katika Uzalishaji Mali kwa kutekeleza miradi mingi yenye tija kwa Taifa na kuleta maendeleo, ametoa rai kwa Bodi mpya aliyoizindua kushirikiana na Menejimenti kuyaendeleza mafanikio hayo.
Aidha, amewataka kuongeza ubunifu ili Uzalishaji na utendaji uimarike zaidi ndani ya Shirika hilo kwa kuendeleza mambo mazuri yaliyoanzishwa na Bodi iliyopita na kuweka mbele mikakati na ubunifu katika uwekezaji wa miradi mipya ili Shirika lipige hatua kubwa zaidi katika kukidhi madhumuni ya kuanzishwa kwake mwaka 1981. pasipo kusahau suala la Ulinzi na Usalama.
Aidha, amempongeza Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Meja Jenerali Mstaafu Farah Mohamed na wajumbe wa Bodi, kwa kujituma, ubunifu na kazi nzuri iliyoleta mafanikio kwa shirika hilo.
Uzinduzi huo pia umehudhuriwa na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Bodi hiyo, Meja Jenerali mstaafu Farah Mohamed, wajumbe wapya wa Bodi ya Ushauri, Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT, Brigedia Jenerali Petro Ngata, Mkuu wa Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, Wakurugenzi Makao Makuu ya SUMAJKT, Wakuu wa Miradi, Wakuu wa Makampuni na Wakuu wa Kanda za Ujenzi pamoja na Wakuu wa Shule zilizo chini ya Jeshi la Kujenga Taifa zinazosimamiwa na SUMAJKT.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda pamoja na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele, mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar, tarehe 06 Januari, 2026.
Waziri wa Ulinzi na JKT Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho amefanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya JKT Chamwino Dodoma Desemba 8, 2025, kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza na Maafisa, Askari, Vijana na Watumishi wa Umma.
Mhe. Dkt. Nyansaho amelipongeza JKT kwa kuendelea kutekeleza Majukumu yake ya Malezi ya Vijana, Uzalishaji Mali na Ulinzi, akaongeza kuwa Serikali kupitia Wizara anayoiongoza, itaendelea kuliwezesha Jeshi hilo ili liweze kuendelea kutekeleza majukumu hayo.
MHE. DKT. NYANSAHO ATEMBELEA MAKAO MAKUU YA JWTZ
Waziri wa Ulinzi na JKT, Mhe. Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho (Mb) tarehe 05 Desemba 2025, amefanya ziara ya Kikazi Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Msalato Dodoma, kwa lengo la kujitambulisha baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kushika wadhifa huo.
Mhe Dkt. Nyansaho alipokelewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, ambaye aliwaongoza Maafisa, Askari pamoja na watumishi wa umma kumlaki na kumkaribisha Makao Makuu ya Jeshi.
Akizungumza na Maafisa, Askari na Watumishi wa Umma waliohudhuria hafla hiyo, Mhe. Dkt. Nyansaho amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuliwezesha JWTZ ili liweze kutekeleza majukumu yake ya Ulinzi wa Taifa.
Mhe. Nyansaho amewahakikishia watendaji hao ushirikiano mkubwa ili JWTZ liweze kufikia malengo yanayokusudiwa.
Ziara ya Kikazi ya Waziri wa Ulinzi na JKT Makao Makuu ya Jeshi Msalato, ilihudhuriwa pia na Maafisa Jenerali, Maafisa Wakuu, Maafisa, Askari pamoja na Watumishi wa umma.