Grand Imam of Masjid Ma'amur, Chairman of Mwinyi Baraka Islamic Foundation @MwinyiBaraka, Member of Scholarly Committe - BAKWATA, Theological Director @halaaltz
Asili ya dini nzima ni tabia njema. Allah, Subhannahu, ameuhusisha uvumilivu kuwa ni miongoni mwa sifa zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghfira na mwenye lutfu na kwahivyo anapendelea waja wake kujipamba na tabia ya uvumilivu na kusamehe wengine.
“Kivuli kilichonyooka hakitarajiwi kutoka kwenye kijiti kilichopinda. Hivyo basi usikimbilie kivuli; bali nyoosha kijiti.” Hekima ya ki-Sufi, nukuu toka kwa Sheikh Ahmed Saad al-Azhari.
Kadiri mja anavyozidi kumdhukuru Mwenyezi Mungu kwa dhikri, ndivyo moyo wake unavyozidi kuwa msafi, na kadiri moyo unavyokuwa msafi, mawazo machafu huanza kuondoka moyoni mwake hata yakatoweka kabisa. Al-Allamma Muhammad Alauddin Siddiqui.
Tunapokumbwa na mitihani na matatizo, tunapaswa kuwa na mioyo yenye subira na ndimi zenye kushukuru. Hata ikawa matendo yetu maovu katika maisha hubadilishwa kuwa mema, na kile kinachodhaniwa kuwa ni dhiki kuwa neema.
Hakika, kutabasamu ni kipawa chenye kuinua hali yako na hali za wengine. Katika dini yetu hii (Uislamu), kutabasamu kunahimizwa. Jaribu kutabasamu kadri uwezavyo, uso wa Mtume ﷺ muda wote ulipambwa na tabasamu na hakuwa na fikra hasi hata alipokuwa amejawa wasiwasi na huzuni.
Mtu ajinufaishe na muda wake maadamu ana afya njema na ahifadhi mtaji wake ambao ni uhai wake, wakati wake na pumzi yake, akiupoteza kwa udadisi, pumbao na kughafilika, anaupoteza na kuutupa; basi kadiri awezavyo, anapaswa kuutumia muda wake vizuri na kutojali ni msiba mkuu.
Kamwe usiwe mwenye kuwasimbulia watu wema auliowatendea bali kuwa mwenye kushukuru wema watu waliokutendea; Ni vyema ukawa msahaulifu wa mema unayowatendea watu lakini kamwe usiwe msahaulifu wa mema wanayokutendea watu; Ni bora ukamsahau uliyemsaidia kuliko kumsahau aliyekusaidia
Ametongoa mmoja wa wema:
“Ye ni mpenzi wangu,” amenadi Mwingi wa Rehema;
Kimbilio la nyoyo za maashiki, Nawe ndiye nafsi halisi ya nafsi;
Mpewa, mwenye milki;
Muhammad Mtengwa, nuru yako inayoangaza ndiyo dhati ya nafsi yangu.
Mwenyezi Mungu akubarikini ninyi, nasi na Waislamu wote katika Idi hii, na Mwenyezi Mungu atutakabalie amali zetu tulizotenda mchana na usiku wa Ramadhani na usiku wetu huu, usiku wa tuzo. Hakika malipo ya Mola wako Mlezi ni makubwa kwa uweza wake, na zawadi Zake ni vivyo hivyo.
Ibn Rajab – Mwenyezi Mungu amrehemu – amesema: “Yatakikana mja aihitimishe Ramadhani kwa istighfari.” Na Umar bin ́Abd al-‘Aziz – Mwenyezi Mungu amrehemu – aliandika barua akiwaamuru watawala na wakazi wa majimbo waihitimishe Qur’ani kwa kuomba msamaha na kutoa Zakaatul-Fitri.
#TafakuriYaLeo Kadiri mja anavyozidi kufanya Dhikr ya Mwenyezi Mungu, ndivyo moyo wake unavyozidi kuwa msafi, na kadiri moyo unavyokuwa msafi, mawazo machafu haraka huanza kuondoka (moyoni) hata kufikia yote kutoweka.
#TafakuriYaIjumaa Dunia hii ni kama nyoka - nyororo ukigusana naye, lakini sumu yake ni hatari (yenye kuangamiza). Kijana mjinga humkimbilia, (ilhali) mtu mzima mwenye hekima huwa na tahadhari naye.
Imam Al-Ghazali (Mwenyezi Mungu amrehemu): “Laylatul-Qadr ni kama mgeni mtukufu, jiandae kumpokea kwa kuusafisha moyo wako, kuondosha vilengelenge vyenye kuuhangaisha, na kuzidisha taqwa juu ya Mwenyezi Mungu.
Chanzo: Ihyaa’ ‘Uloom al-Deen, Abu Hamid al-Ghazali, Juz. 1, uk. 234.
Kasema Imam Al-Shafi‘i (Mwenyezi Mungu amrehemu): “Ili kuitambua Laylatul-Qadr, ongeza ibada yako katika masiku 10 ya mwisho hali unajikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu, kwani Yeye huwaruzuku (hiyo) wanaoitafuta kwa ikhlasi.”
Al-Umm, Imam Al-Shafi‘i, Juz. 2, uk. 231.
Ibn al-Qayyim al-Jawziyyah (Mwenyezi Mungu amrehemu) amesema: “Kama mja hayuko tayari kujikurubisha/kujinyenyekeza kwa Mwenyezi Mungu kwenye Laylatul-Qadr, hata akiushuhudia (Usiku wa Cheo), hukosa baraka zake.”
Chanzo: Madaarij al-Saalikeen, Ibn al-Qayyim, Juz. 1, uk. 504.