Leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya Matawi mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa. Dominika hii ina sura mbili - furaha na huzuni. Sura ya furaha tunaionja katika sehemu ya kwanza ya ibada ya siku hii tunapoadhimisha namna Yesu alivyoingia Yerusalemu kwa shangwe, siku sita kabla ya Pasaka.
Kristo Yesu ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu; ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Kuingia kwa Kristo Yesu mjini Yerusalemu kunaonesha ujio wa Ufalme wa Mungu: Wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anakumbusha kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo.Maandamano haya sio ya kuiga au kurudia mambo ya kihistoria yaliyopita tu, bali ni ishara ya nje ya sisi kukiri na kuungama waziwazi kuwa Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa ajili yetu ni Mfalme wetu.
Sehemu ya pili ya Ibada ya Dominika ya Matawi ni kukumbuka mateso ya Yesu Kristo yanayotuingiza katika Jumaa Kuu la kuadhimisha fumbo la ukombozi wetu, mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, yaani Pasaka. Katika sehemu hii Kanisa linaweka mbele yetu mateso makali aliyoyapata Kristo Yesu na kutueleza mapato yake โ ushindi dhidi ya dhambi na mauti unaodhihirishwa na utukufu wa ufufuko wake.Kwa hiyo liturujia ya adhimisho hili imejaa mwanga wa Pasaka. Nasi tukiweka matumaini Yetu kwa Kristo Yesu, tukayaishi mafundisho yake, tutashinda na kustahilishwa kuurithi uzima wa milele.
Ikumbukwe kuwa siku ya Dominika ya Matawi Injili inasomwa pasipo mishumaa wala chetezo na bila utangulizi wala ishara ya msalaba. Nayo husomwa na shemasi baada ya kuomba na kupokea baraka ya Padre. Na kama hakuna shemasi husomwa na Padre. Lakini ili kuipamba liturujia hii, Injili husomwa na walei kwa kuimba, ili kuweze kuwa na uwakilishi wa wahusika katika simulizi hili. Lakini sehemu ya Kristo lazima isomwe au kuimbwa na Padre. Simulizi hili linatuambia kuwa Yesu alikamatwa akiwa bustanini Gethsemane akisali. Naye bila ubishi alikubali kukamatwa, akahukumiwa, na kuanza safari ya ukombozi kuelekea Golgota kusulubiwa. Safari hii ilikuwa na mateso makali sana: alibebeshwa msalaba mzito, alifanyiwa dhihaka, alipigwa mijeledi, akavuliwa nguo, akatemewa mate, akatukanwa, akasulubiwa msalabani, na hatimaye akafa, kwa sababu ya dhambi zetu na kuonekana kuwa mtu aliyelaaniwa na Mungu. Lakini kwa kifo chake kilivyokuwa cha pekee, dunia ilitetemeka, jua lilififia, kukawa giza juu ya nchi, pazia la hekalu likapasuka mara mbili. Naye alipochomwa ubavu kwa mkuki, vilitoka damu na maji, ndizo chemichemi za Sakramenti za Kanisa. Nao walioshuhudia walisadiki uaguzi wa manabii na kusema, โhakika huyu alikuwa mwana wa Mungu.โ
Tuige mfano wa Kristo Yesu, Bwana, Mwalimu na Mkombozi wetu aliyepambana na kumshinda shetani si kwa upanga na vitisho bali kwa uvumilivu, unyenyekevu, upole na utii wake kwa Mungu Baba. Yuda alimsaliti Yesu kwa busu, alama na ishara ya upendo, Petro naye alimkana mara tatu, nao Mitume wengine, walimkimbia. Sisi nasi tunafanya mambo haya haya, tunamsaliti, tunamkana na kumkimbia Yesu Kristo, kila tunapoionea aibu Injili, tunaporudi nyuma kiimani na kukosa matumaini kwake kwa sababu ya magonjwa na matatizo ya kimaisha hata kutafuta suluhu katika dhambi.Jogoo amekwisha kuwika mara ya tatu, tunaalikwa kujirudi, tujiweke chini ya Msalaba wa Kristo, kwani hatuna tumaini lingine, japo kwao wanaopotea Msalaba ni kikwazo na upuuzi, kwetu sisi ni nguvu ya Mungu, alama na bendera ya ushindi, kama tukiutazama kwa imani na moyo wa toba.
Basi katika Juma Kuu linalofunguliwa na Dominika ya Matawi, tuombe neema ya kuwa wasikivu na watii, tujipatanishe na Mungu ili tuweze kuifurahia Pasaka, ufufuko wa Bwana, na baada ya maisha ya hapa duniani, tukastahilishwe kufurahi naye Mbinguni.
Tumsifu Yesu Kristu. ๐