Ninaipongeza Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania (Twiga Stars), kwa kuanza vyema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 nchini Morocco kwa ushindi dhidi ya Timu ya Taifa ya Wanawake ya Afrika Kusini, (Banyana Banyana).
Ninaungana na Watanzania wote kuitakia kila la kheri Twiga Stars inapoendelea kupeperusha bendera ya Taifa letu katika michezo inayofuata. Endeleeni kupambana kwa moyo huo huo, mkionesha uzalendo, nidhamu na ari ya ushindani inayolitangaza vyema Taifa letu.
Usiku wa leo mkoani Dar es Salaam, nimeungana na viongozi na wananchi wenzangu kuadhimisha miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Maadhimisho haya yametupa fursa ya kuendelea kutambua na kujivunia mchango mkubwa wa TRA pamoja na walipakodi wote katika maendeleo ya Taifa letu.
Tunapotekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni muhimu kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani. Hili litafanikiwa wananchi wakilipa kodi kwa uaminifu, TRA ikikusanya kwa haki, na Serikali ikitumia mapato kwa uadilifu.
Sote tuendelee kukumbuka kuwa, kulipa kodi ni wajibu, ni uzalendo, ni heshima, na ni dhamana inayorudi kwa wananchi kupitia huduma na shughuli za maendeleo.
Julai 25 kila mwaka ni Siku ya Mashujaa; siku adhimu ya kuwakumbuka na kuwaenzi wote waliotoa maisha yao kupigania uhuru na kulinda amani ya nchi yetu. Kwa ujasiri, uzalendo na kujitolea kwao, walituachia msingi imara wa uhuru, amani, umoja na mshikamano tunaouenzi hadi leo.
Tunapowakumbuka mashujaa wetu, tuendelee kulinda tunu walizotuachia kwa kudumisha amani, umoja na kufanya kazi kwa bidii katika kujenga Tanzania yenye maendeleo na ustawi, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mungu Ibariki Tanzania.
𝗥𝗔𝗜𝗦 𝗦𝗔𝗠𝗜𝗔 𝗔𝗡𝗔𝗜𝗡𝗨𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗞𝗜𝗠𝗔𝗧𝗔𝗜𝗙𝗔.
🔷 Kutunukiwa Shahada ya Heshima ni utambuzi wa mchango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, elimu na maendeleo ya jamii.
🔷 Heshima hii inaendelea kuitangaza Tanzania katika jukwaa la dunia na kuonyesha kuongezeka kwa ushawishi wa Taifa katika masuala ya kimataifa chini ya uongozi wenye matokeo wa Rais Samia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.
Leo nimepata heshima ya kufunga Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi Namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi Namba 48 kwa Mwaka 2025/26 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) cha Jeshi la Magereza jijini Dar es Salaam, ambapo wanafunzi 657 wamehitimu.
Jeshi la Magereza lina nafasi muhimu katika mfumo wa haki jinai nchini. Hivyo, pamoja na kuwapongeza wahitimu, nimewasihi kuwa maarifa waliyoyapata yawe nyenzo ya mabadiliko ya kiutendaji, mathalan katika urekebishaji tabia za wafungwa, na uboreshaji taswira ya jeshi hilo, sawa sawa na mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na maelekezo ya Dira 2050.
Ili kuhakikisha wafungwa wanaoachiwa hawarudi magerezani, serikali itaweka utaratibu wa kuwapatia mitaji ili watumie ujuzi wanaoupata magerezani kujiendeleza. Aidha, nimelielekeza Jeshi la Magereza kuwa na mfumo wa TEHAMA utakaowezesha kuwafuatilia na kuwafanyia tathmini wafungwa walioachiwa, kujua walipo na shughuli wanazofanya.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi 2026), ambayo Kitaifa yamefanyika Mkoani Njombe, tarehe 01 Mei, 2026.
NJOMBE ➡️IRINGA
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiagana na watumishi wa serikali na chama katika Uwanja wa Ndege wa Iringa, mara baada ya kukamilika kwa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi yaliyofanyika mkoani Njombe.
Kheri ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Leo nimeungana na wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi mkoani Njombe katika maadhimisho ya siku hii kitaifa, ambayo mwaka huu imefungamanishwa na utekelezaji wa Dira ya 2050 unaoanza Julai 1. Hii ni hatua ya kimkakati inayolenga kuelekeza nguvu kazi ya Taifa katika kujenga uchumi shindani, jumuishi na endelevu.
Ninampongeza kila mfanyakazi kwani mafanikio tunayojivunia leo ni matokeo ya juhudi za pamoja katika sekta zote. Serikali yenu itaendelea kuimarisha fursa za ajira, kupanua fursa za kiuchumi, kuboresha mazingira na maslahi ya wafanyakazi, pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata kazi yenye staha, inayozingatia haki, usalama na ustawi.
Ili kufikia malengo hayo tunahitaji dhamira ya pamoja, kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi wa hali ya juu, huku tukidumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu.
Nchi yetu imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa kwanza barani Afrika wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Jumuiya ya Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) ambao leo nimeufungua jijini Dar es Salaam. Uamuzi huu unadhihirisha imani kubwa katika maendeleo yetu na utayari wetu katika kuimarisha zaidi huduma za afya, hususan huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.
Matokeo ya kazi kubwa tuliyofanya katika miaka mitano iliyopita katika huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi yanaonekana ambapo;-
1. Hospitali zinazofanya upasuaji wa kibingwa wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu zimeongezeka kutoka 2 hadi 7.
2. Madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu wameongezeka kutoka 12 hadi 37.
3. Tumeongeza kwa kiasi kikubwa vifaa muhimu kama MRI, CT-Scan na X-ray.
Uwekezaji huu umeifanya Tanzania kuwa moja ya nchi chache Afrika zenye uwezo mkubwa wa kufanya upasuaji huo, na sasa inahudumia wagonjwa kutoka nje ya nchi.
Ninashukuru Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania kwa tuzo mliyonipa, hakika, hii ni heshima yetu sote. Serikali yetu itaendelea kushirikiana na taasisi za kikanda na kimataifa kuimarisha huduma za afya kwa kuzifanya kuwa bora, nafuu na za uhakika ili kuokoa maisha ya wananchi na kurejesha tumaini kwa jamii.
RAIS SAMIA AAGIZA UWAZI MANUNUZI YA UMMA, ASISITIZA UWAJIBIKAJI
Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kuimarishwa kwa uwazi na uwajibikaji katika manunuzi ya umma, akielekeza taasisi zinazokiuka taratibu kutajwa hadharani na kuchukuliwa hatua.
Akizungumza tarehe 30 Machi, 2026, Ikulu Dar es Salaam, wakati wa kupokea Taarifa ya Mwaka ya Tathmini ya Utendaji wa Ununuzi wa Umma, Rais Samia amesema sehemu kubwa ya fedha za Serikali hutumika katika manunuzi ya umma, hivyo usimamizi madhubuti ni muhimu kulinda rasilimali za wananchi.
“Ripoti zijazo zitaje wazi taasisi zinazofanya vibaya na zinazofanya vizuri, ili kuongeza uwajibikaji na kuchukua hatua stahiki,” amesema Rais Samia.
Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha rasilimali za Serikali zinatumika kwa manufaa yaliyokusudiwa.
Asubuhi ya leo nimepata baraka ya kumuasili Grace Samia Suluhu. Grace ni mtoto mchanga aliyetelekezwa mjini Nzega, mkoa wa Tabora. Kila mtoto anayezaliwa ni baraka na hazina kwa jamii.
Tunao wajibu ndani ya Serikali na kila mwananchi kuhakikisha tunashiriki katika malezi, ulinzi, upendo na kesho ya watoto, kwani ndiyo kesho yetu na Taifa letu.
Karibuni Tanzania.
Karibuni Nyumbani.
Leo nimejumuika na Marais wa nchi na Wawakilishi wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, jijini Arusha.
Miaka 26 tangu kurejeshwa kwa umoja huu, umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha nguvu za nchi zetu kama ndugu, kuongeza sauti ya pamoja katika masuala mbalimbali, na kujenga mustakabali wenye mafanikio kwa wananchi wa Afrika Mashariki.