SERGIO Ramos Garcia licha ya kwamba alizaliwa na kuanza maisha yake ya soka ndani ya Klabu ya Sevilla lakini ni moja ya wachezaji wanaoheshimika vilivyo Real Madrid.
.
Heshima ya Ramos Madrid inakuja kwa sababu ya kuiongoza katika mafanikio makubwa akiwa mchezaji wa kawaida na hata pale alipokuwa nahodha akipokea kitambaa kutoka kwa Iker Casillas mwaka 2015. Tangu wakati huo hadi msimu wa 2021/22 alipoondoka Madrid, Ramos alibeba mataji 12, yakiwemo matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ‘Uefa’
.
Mataji hayo yamemfanya Ramos kuwa moja ya manahodha wa Real Madrid waliobeba mataji mengi hadi alipoondoka na kuhamia Paris Saint-Geirman ya Ufaransa. Kwa hapa Bongo, tuna Sergio Ramos wetu na anapatikana mitaa ya Twiga na Jangwani ilipo klabu ya Yanga. Wawili hao kwa maana Ramos wa Ulaya na huyu wa Tanzania wote walihamia klabu ambazo zimewapa heshima kubeba mataji mengi.
.
Ramos wa Bongo ardhi ya Julius Nyerere ni Bakari Nondo Mwamnyeto, ni mmoja wa manahodha waliobeba mataji mengi tangu alipowasili kwa Wananchi Agosti Mosi mwaka 2020. Mwamnyeto alitua Yanga akitokea Coastal Union ya Tanga alikozaliwa na kazi kubwa aliyoifanya ndani ya kikosi hicho ndiyo iliwashawishi mabosi wa Yanga kuvunja benki na kuinasa saini yake na kumfanya kuwa beki mzawa aliyesajiliwa kwa kitita kikubwa zaidi kikitajwa kufikia milioni 200.
.
Beki huyo alikabidhiwa unahodha wa Yanga akichukua kitambaa kutoka kwa beki mwenzake, Mghana, Lamine Moro ambaye aliachwa na klabu hiyo. Tangu Mwamnyeto abebe kitambaa hicho cha unahodha wa Yanga hadi sasa amebeba mataji 11 ambayo yanamfanya kuwa miongoni mwa manahodha ambao wamechukua mataji mengi.