Oh! How we think it's done, then here comes a new tiding. Growing up is tough, we find wait on the list and here comes patience on the road, there comes listen around others, and boy! how love washes our eyes, we can't but be in the gym of 'forgiveness'.
Tabia zetu nyingi mbaya (chuki, kiburi, husda, visasi, roho mbaya, wivu kupindukia, mashindano) ni jitihada za nafsi kupambana na kumbukumbu ya upweke wa utotoni, hasira ya kukataliwa na hofu ya kuachwa na watu wetu wa karibu tuliowaamini utotoni—hasa wazazi, walimu na watoto wenzetu tuliocheza nao.
Unaweza kuwa na watu wanakupenda lakini huamini unaweza kupendwa hivi hivi na matokeo yake unajikuta ukiharibu kile kile unachokihitaji. Unakumbuka ulivyopambania upendo wa mzazi ukiwa mtoto kiasi kwamba huamini kuna mtu mwingine anaweza kukupokea hivyo ulivyo.
Tiba ni pamoja na kupata mtu (mwenzi, rafiki wa karibu, au hata mnasihi) atakayekusaidia kumsikiliza ‘mtoto’ ndani yako, ajisikie kukubalika bila masharti— akuruhusu kukosea, kuogopa, kuwa na hasira bila kukukataa. Mtu huyo, aghalabu, atakuwa na kazi ya kukuwekea mazingira ya kujisikia salama kuamini kuwa unaweza kupendwa bila kupambania upendo, atakufanya ujisikie kusikika, kueleweka, kuaminika, na hapo ndipo utakapoushinda upweke wa utotoni.
Usiombe binadamu apoteze uwezo wa kujisikia hatia. Ukishaacha kujisikia hatia unakuwa sawa na wanyama wengine wasio na dhamiri. Hatia, kimaumbile, inaturudisha kwenye wajibu wa kuutafakari mstari unaotenganisha mema na mabaya. Unapojisikia hatia maana yake dhamira yako inakushtaki kwa kufanya maamuzi unayojua si sahihi—mf. umemwuumiza mwezako, hujatenda haki nk—na huu ndio msingi wa uadilifu wa mwanadamu.
Hatia ni somo muhimu tunalolipata utotoni kupitia mahusiano yetu na wazazi. Kwa kawaida, hatupendi kuwakosea wazazi/walezi wetu. Tunawahitaji. Tunauhitaji upendo wao. Tunapokemewa kwa kukosea, kwa mfano, tunajisikia hatia. Tunajirudi. Hatupendi kupoteza uhusiano wetu na watu muhimu kwenye maisha yetu. Tunajifunza kujisikia aibu kwa matendo yetu yasiyopendeza. Hata hivyo, wapo wazazi huenda mbali na kutudhalilisha mbele za watu muhimu kama namna ya kutuonya. Hawa, kwa ukali wao, ukatili, hasira huenda walituchapa na kututukana tukajifunza hisia nyingine inayoitwa fedheha.
Unapofedheheka, aghalabu unaanza kuwa na wasiwasi na utu wako. Unapoteza kujiamini kwamba wewe ni mtu anayestahili heshima. Unaanza kujihoji namna watu wanavyokuona. Unaanza kujidharau. Unagundua hakuna kitu utafanya kikakubalika. Unapoteza matumaini ya kumridhisha mzazi. Unaanza kukosa kitu cha kupoteza. Mawili yanaweza kutokea. Kwanza, uwe mpweke asiyeamini ana lolote la kuchangia kwenye jamii ingawa unapotelea kwenye sonona. Pili, uwe jitu katili lisilo na dhamiri tena.
Hili la pili likitokea unakuwa sawa na watu walikosa ukaribu na wazazi/walezi wenye upendo uliowakumbusha haja ya kujisikia hatia. Hawa hawakupendwa, waliishi katika upweke na tangu utotoni hawakuwa na watu waliowapenda na kuwafanya wajikie wana kitu cha kupoteza. Hawa, aghalabu, huishia kuwa watu wazima wasiojisikia hatia wala fedheha. Hawa ni watu waliopoteza dira inayoamsha dhamiri. Hawa hugeuka kuwa watu wakatili wanaoweza kufanya uovu dhidi ya binadamu wenzako na hawajutii. Hawa, wakipata nafasi na madaraka, wanaweza kukuumiza na wakategemea uombe msamaha kwa kuwachokoza.
Ombwe lina tabia ya kumshughulisha mtu. Ukiwa na ombwe, mfano huna kitu kikubwa cha maana unachopambania zaidi ya sifa nyepesi nyepesi, unajiweka kwenye hatari ya kuteketeza muda na nguvu nyingi kwenye ubobezi wa mambo yasiyo na maana—majoring in minor things.
Kwa ngazi ya maisha binafsi mtu mzima na ombwe lako unaaga asubuhi unaenda kazini lakini huko uliko nguvu zote unazielekeza kwenye AOB —‘mambo mepesi yanayojitokeza.’ Ikitokea ukabahatika kuwa kiongozi wa taasisi ndio kabisa unakuwa mbobezi kwenye shughuli zinazowashughulisha watu na haziwasaidii.