Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi mbalimbali kwenye Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, tarehe 05 Agosti, 2026.
Leo jijini Dar es Salaam nimeungana na viongozi wengine wa Afrika kufungua Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika, ambapo Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji. Jukwaa hilo, linaloadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, limekuwa sehemu muhimu ya kuunganisha mitaji, miradi na wataalamu ili kuharakisha maendeleo ya miundombinu barani Afrika.
Katika mkutano huo nimeeleza kuwa, Tanzania inashirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kuimarisha miundombinu, ikiwemo barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege. Hatua hii inachochea ukuaji endelevu wa uchumi kwa kupunguza gharama za usafirishaji, kukuza biashara, kuvutia uwekezaji, kutoa ajira na kuifanya nchi yetu kuwa kitovu cha usafirishaji.
Kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kimazingira duniani, nimesisitiza umuhimu wa Afrika kuimarisha miundombinu inayohimili mabadiliko hayo na kuunganisha nchi zetu ili kuendelea kukuza biashara, uwekezaji na uongezaji thamani wa rasilimali zetu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania ni Mhe. Chen Mingjian, Ikulu ya Tunguu, Zanzibar tarehe 28 Julai, 2026.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu Prof. Palamagamba A. Kabudi akitoa mada inayohusu Muungano na Mawasiliano; Msingi, Muundo na Umuhimu wake wakati wa ufunguzi wa Semina Elekezi kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu Umuhimu wa Mawasiliano Serikalini, tarehe 28 Julai, 2026, Ikulu ya Tunguu, Zanzibar.
Matukio mbalimbali katika Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, zilizofanyika kitaifa katika Uwanja wa Mashujaa, uliopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, tarehe 25 Julai, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, tarehe 16 Julai, 2026.
Ninakipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar kwa kufanya mazungumzo na kufikia maridhiano. Hii ni hatua muhimu inayozidi kuimarisha amani, umoja, utulivu na mshikamano miongoni mwa Watanzania. Maridhiano si ishara ya udhaifu bali ni alama ya ukomavu wa kisiasa unaoweka mbele maslahi ya Taifa badala ya maslahi ya vyama au ya mtu binafsi.
Wananchi hawahitaji vurugu wala mivutano ya kisiasa isiyoisha. Wanahitaji amani, usalama, huduma bora za kijamii, ukuaji wa fursa za kiuchumi na ajira. Ili kufanikisha hayo, serikali itaendelea kusimama imara katika kulinda usalama wa raia na mali zao, pamoja na kudumisha heshima na hadhi ya nchi yetu.
Kwa pamoja, tutafakari umuhimu wa maridhiano kama yanavyohimizwa pia katika vitabu vitakatifu:
Qur'ani Tukufu Sura Al-Hujurat 10: "Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu; basi patanisheni baina ya ndugu zenu na mcheni Mwenyezi Mungu, (msipuuze jambo la kupatanisha) ili mrehemewe."
Biblia Takatifu – Mathayo 5:9: "Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu."