Ilikuwa mwezi wa Agosti mwaka 2018 Tarehe 7 siku ya Jumanne nilipokutana kwa mara ya kwanza na Mwanahamisi Yusufu Sadikuli. Hii ilikuwa ni baada ya kupokea barua kutoka kwake akiwa bado ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Chanzige B, Kisarawe. Wakati huo, nilikuwa ndio kwanza nimepata uteuzi wangu wa kwanza wa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe katika Mkoa wa Pwani, nikiwa nimetoka kuapishwa Tarehe 3.
Kwenye barua yake aliomba nitembelee shule yao na kupokea changamoto zao. Kiukweli nilivutiwa sana na ujasiri wa huyu Binti kwa kumuandikia DC lakini zaidi wa kutaka fursa ya kwake na wanafunzi wenzake kujadiliana masuala ya ustawi wao pale shuleni. Niliitikia wito na nikafika shuleni kwao na kuwasikiliza. Kilikuwa ni kikao Kizuri. Nitumie fursa hii kumpongeza Mwalimu aliyehariri barua yake na kumtia moyo ailete ofisini kwangu. Wengine wangeweza kumzuia huyu mwanafunzi. Alifanikiwa kumaliza darasa la Saba na kufaulu kwa alama ya A na kuchaguliwa kwenda kusoma sekondari.
Wiki iliyopita huyu Binti wa Kisarawe, Pwani alifika ofisini kwangu, Korogwe. PS wetu ofisini alikuja na kunijulisha kuna binti kutoka Kisarawe amekuja kukusalimia, nikasema sawa. Alipo ingia ofisini sura yake ikanijia. Nikamuuliza umekuja kufanya nini akasema amekuja kusema asante. Kipindi kile mwaka 2018 nilimtia moyo na kumpa ujasiri wa kupambania elimu yake na kidato cha nne amefaulu kwa kupata division 1.10 na anapambana asome PCM ili awe mechanical engineer. Mara ya mwisho kumuona ilikuwa ni mwaka 2018 nimefurahi kumuona tena mwaka huu akiwa amepiga hatua kubwa kwenye safari yake kitaaluma.
Safari ya Mwanahamisi ni uthibitisho wa nguvu ya azimio na kuweka jitihada katika kile anachofanya. Hadithi yake ni mfano bora kwamba wasichana wadogo, wakiwa na nidhamu ya kujifunza na kujiendeleza, wanaweza kuvuka vikwazo na kutimiza ndoto zao maishani. Lakini pia tusiache kushukuru na kusema ASANTE kwa wote ambao wanakuwa na mchango kwenye safari yetu ya maisha, Tuwakumbuke!!!
Shukrani ya kimya haitumikii mtu yoyote!!!
Mh upewe maua yako sasa @jokateM tafsir nzur ya kiongoz ni kuwa miongoni mwa wananchi na kuweka mamlaka pembeni na kutumia Upendo/hekima n.k tendaji wako ni zaidi ya kimamlaka ni upendo : sikuwahi onahi popote wew ni shuja chaguo la Raisi wetu @SuluhuSamia@ikulumawasliano