HABARI:
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Sigrada Mligo, amewataka wanawake kuwa na shughuli za kufanya zitakazowawezesha kujipatia kipato na kujikimu katika maisha.
Mligo amesema kuwa mwanamke mwenye shughuli na kipato ana nafasi kubwa ya kuchangia mahitaji ya familia, akisisitiza kuwa mchango huo pia huimarisha heshima na mahusiano ndani ya ndoa.
Ametoa kauli hiyo wakati akifunga Kongamano la Wanawake WAWATA lililofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Matembwe, Wilaya ya Njombe.
Amesema ni muhimu mwanamke kuwa bize na majukumu yenye tija ili aweze kujipatia fedha za kujikimu, akieleza kuwa mwanaume pia huheshimu mchango wa mwanamke katika familia.
HABARI:
Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, @AdoShaibu ameshiriki Ibada ya Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre ya Mhashamu Askofu Filbert Mhasi wa Jimbo Katoliki Tunduru-Masasi.
Ibada hiyo imefanyika katika viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Xavery, Tunduru, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 ya utumishi wa Askofu Mhasi katika daraja la Upadre.
HABARI:
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amefanya ziara ya kushtukiza leo Jumapili, Agosti 23, 2026, katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, kukagua hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alipowasili hospitalini hapo, Dkt. Mwigulu ametembelea wodi mbalimbali, zikiwemo Wodi ya Mama na Mtoto na Wodi ya Upasuaji, ambako amezungumza na wagonjwa pamoja na ndugu zao na kusikiliza maoni yao kuhusu huduma zinazotolewa hospitalini hapo na changamoto wanazokabiliana nazo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wanaopata huduma hospitalini hapo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kuboresha huduma za afya na mazingira ya utoaji wa huduma hospitalini hapo.
HABARI:
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuendelea kuliombea Taifa na kudumisha amani, akisema amani ni msingi unaowezesha wananchi, taasisi za dini na Taifa kwa ujumla kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.
Amesema dunia inaendelea kushuhudia mabadiliko na mitikisiko katika maeneo mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kumwomba Mungu ailinde Tanzania na kuendeleza amani ambayo imeiwezesha nchi kutekeleza shughuli zake kwa utulivu.
Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumapili, Agosti 23, 2026) aliposhiriki ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Usharika wa Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
“Tuendelee kuiombea nchi yetu. Leo hii tunaweza kufanya ibada kwa sababu nchi yetu ipo na amani. Tuna mipango mbalimbali kama nchi, katika ngazi ya familia, taasisi, Dayosisi na Kanisa, lakini hayo yote tunaweza kuyafanya kama nchi yetu ipo na amani,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kusonga mbele.
“Hauwezi ukataja maendeleo ya nchi yetu bila kutaja mchango wa Kanisa,” amesema.
Naye Katibu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Bw. Goodluck Nkini, alimshukuru Waziri Mkuu kwa kuchagua kuabudu katika Usharika wa Kijitonyama na kwa kuendelea kujumuika na waumini katika maeneo mbalimbali.
Ibada hiyo iliongozwa na Mchungaji Anna Kuyonga wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Kijitonyama.
Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Aggrey Mwanri; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila; Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule; Mbunge wa Same Magharibi, Dkt. David Mathayo; na Mbunge wa Makete, Festo Sanga.
HABARI:
Taharuki imeibuka katika Mtaa wa Njedengwa jijini Dodoma baada ya Katibu wa CCM wa tawi la Njedengwa, Maulid Juma, kudai nyumba yake imebomolewa bila kuzingatia utaratibu, licha ya kueleza kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa eneo hilo.
Maulid amesema mgogoro huo ulianza baada ya mtu mwingine kudai umiliki wa eneo alilonunuliwa mtoto wake na kuandikishwa, hali iliyowafanya pande hizo kufikishwa katika Baraza la Kata na baadaye ngazi ya uongozi wa mtaa kwa ajili ya kutafuta suluhu.
Amesema katika hatua nyingine, aliitwa pamoja na upande wa pili wa mgogoro huo katika kikao alichodai kuitishwa na Diwani wa Kata ya Makulu, Samson Mkopi, lakini katikati ya majadiliano Diwani na baadhi ya viongozi waliondoka huku wakimueleza asiondoke.
Kwa mujibu wa Maulid, muda mfupi baadaye alipigiwa simu na mkewe aliyemjulisha kuwa msafara uliokuwa umeongozwa na Diwani pamoja na kikosi cha ubomoaji ulikuwa ukibomoa nyumba yao.
Amesema tukio hilo linamsikitisha na kwamba linajenga taswira mbaya kwa CCM, akidai kuwa kitendo hicho ni uonevu na hujuma dhidi yake.
Kwa upande wake, Fridaus Matuliani, mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Njedengwa ambaye pia ni mke wa Diwani huyo, amelia kwa uchungu kufuatia tukio hilo na kuitaka haki yao irejeshwe haraka.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Njedengwa West, Daimu Haji, amekana kuhusika na ubomoaji huo, akisema Serikali ya mtaa haitambui kuhusu kilichotokea.
Tulipomtafuta Diwani wa Kata ya Makulu, Samson Mkopi, kwa njia ya simu, amewapa pole wananchi hao na kusema hana mamlaka ya kuvunja nyumba ya mwananchi wala hakuhusika kwa namna yoyote katika tukio hilo, akisema yeye pia alipata taarifa kuhusu tukio hilo kwa kusikia.
HABARI:
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche alipoingia na Kanuni za CCM kwenye mkutano Mkuu maalum wa Chadema wilaya ya Temeke, azungumzia namna CCM ilivyokiuka kanuni zao katika mchakato wa uteuzi wa wagombea.
HABARI:
Mbunge wa Tunduru Kaskazini, @AdoShaibu amesema amewasilisha Bungeni mapendekezo ya masuala mawili muhimu akitaka yapangiwe muda na kushughulikiwa katika Mkutano wa Nne wa Bunge unaotarajiwa kuanza Agosti 26, 2026.
Hoja ya kwanza inahusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya, ambapo Ado amesema amewasilisha hoja kwa mujibu wa Kanuni ya 64(1) ikisomwa pamoja na Kanuni ya 65(1) za Kanuni za Kudumu za Bunge.
Mbunge huyo anataka Bunge liazimie Serikali kuwasilisha ramani kamili ya mchakato wa Katiba Mpya, ikieleza hatua zitakazopitiwa, ratiba ya utekelezaji, muda wa kukamilisha mchakato pamoja na bajeti inayohitajika.
Ado amesema ramani hiyo inapaswa pia kuainisha mapitio ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kuundwa kwa Kamati ya Wataalam, matumizi ya maoni na kazi zilizofanyika katika mchakato uliopita, Mkutano wa Kitaifa wa Wadau, ushirikishwaji wa wananchi pamoja na Kura ya Maoni.
Hoja ya pili inahusu vijana 436 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walioshiriki katika ujenzi wa Ikulu ya Chamwino na miradi mingine ya kimkakati ya Serikali.
Ado amesema vijana hao wamewasilisha kwake ombi la kuifikisha hoja yao Bungeni, wakieleza kuwa baada ya kushiriki katika kazi hizo walipewa matarajio na ahadi ya kupatiwa ajira, lakini hadi sasa sehemu kubwa yao haijapata ajira wala kuwezeshwa kwa namna itakayowasaidia kujenga maisha yao.
Kupitia ombi hilo, Ado amesema vijana hao wanataka Bunge liishauri au kuitaka Serikali kuchunguza hali ya vijana wote 436, kutekeleza ahadi ya ajira kwa wale wanaokidhi vigezo na ambao bado hawajapata ajira, au kuweka utaratibu maalum wa kuwawezesha kiuchumi pale ajira ya moja kwa moja inaposhindikana.
Pia wameomba Serikali izingatie changamoto za maisha wanazokabiliana nazo baada ya kumaliza utumishi wao, pamoja na wale waliopata athari za kiafya kutokana na kazi nzito walizofanya.
Ado amesema kupitia hoja hizo mbili, anatarajia Uongozi wa Bunge utazipatia nafasi ili ziweze kushughulikiwa katika Mkutano wa Nne wa Bunge.
HABARI:
Wakili wa kujitegemea, Moses Basila, ametoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya hoja zinazoibuliwa baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kukutwa na kesi ya kujibu.
Basila amesema miongoni mwa hoja zinazojadiliwa ni uwezekano wa baadhi ya viongozi wa Serikali, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wastaafu, kuitwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo.
Akifafanua kuhusu suala hilo, Basila amesema sheria haimlazimishi Rais kufika mahakamani kutoa ushahidi, bali anaweza kupewa taarifa kuhusu hitaji la kutoa ushahidi na kisha akaamua mwenyewe hatua ya kuchukua.
Kauli hiyo inakuja wakati kesi ya Lissu ikiingia hatua nyingine baada ya Mahakama kumkuta ana kesi ya kujibu, huku mjadala ukiendelea kuhusu mashahidi ambao wanaweza kuitwa na upande wa utetezi.
HABARI:
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, amemtaka Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira, kueleza alikotoa kauli kwamba Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, hatasamehewa na kwamba kesi yake itaendelea.
Heche amesema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari, baada ya Lissu kukutwa na kesi ya kujibu.
Heche amehoji kauli ya Wassira, akitaka kufahamu iwapo Makamu huyo wa CCM alikuwa amewasiliana na majaji kabla ya kutoa kauli hiyo.
“Wasira alikuwa amewasiliana na hao majaji? Tunataka atuambie hayo maneno ameyatoa wapi.”
Heche amesema kauli hiyo inahitaji maelezo, hasa baada ya Wassira kusema Lissu hatasamehewa kama ilivyokuwa kwa Freeman Mbowe.
HABARI:
Kufuatia Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Mkoa wa Morogoro Barnabas Okola kwa mara kadhaa kutoa kauli za kumtuhumu Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara, John Heche
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Morogoro Jackson Malisa kwa niaba ya Baraza la Uongozi amemtaka Katibu huyo kuzingatia taratibu na Katiba ya Chama katika kuzungumza na vyombo vya habari, akisema maoni ambayo amekuwa akiyatoa ni binafsi na sio agizo la Baraza.
HABARI:
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imekataa kuendelea na mahojiano na Halmashauri ya Wilaya ya Same, ikisema haijaridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na maagizo iliyoyatoa kwa Halmashauri hiyo.
Kamati hiyo imefikia uamuzi huo leo baada ya kupitia na kuchambua Taarifa ya Hesabu zilizokaguliwa za Halmashauri ya Wilaya ya Same kwa miaka ya fedha 2023/2024 na 2024/2025.
Katika uchambuzi huo, Kamati imesema haijaridhishwa na utendaji wa Halmashauri hiyo chini ya Afisa Masuuli, ikieleza kuwa kumekuwa na uzembe na kukosekana kwa utayari wa kushughulikia hoja za CAG pamoja na maagizo ya Kamati.
Kamati imesema kati ya maagizo saba iliyoyatoa katika kikao cha Oktoba 27, 2024, ni maagizo mawili pekee, sawa na asilimia 28, yaliyotekelezwa kikamilifu.
Aidha, katika Hesabu za mwaka wa fedha 2024/2025, CAG alitoa hoja na mapendekezo 18, lakini Halmashauri imetekeleza hoja nne pekee, sawa na asilimia 22.
Kamati pia imebaini kuwa Halmashauri hiyo haijatekeleza kikamilifu hoja zilizotolewa na CAG katika miaka iliyopita, ambapo kati ya hoja tisa zilizotolewa, ni hoja tatu pekee zilizotekelezwa.
Kutokana na hali hiyo, LAAC imesema mwenendo huo ni dharau kwa Bunge pamoja na CAG, ambaye kwa mujibu wa Kamati ni “jicho la Bunge”.
“Kutokana na hali hii, Kamati haiwezi kuendelea na mahojiano na Halmashauri ya Same, na hivyo wakatekeleze hoja zote.”
Kamati imeitahadharisha Halmashauri ya Same kutekeleza hoja zote za CAG na maagizo ya Kamati, huku ikitoa onyo kwa Halmashauri nyingine nchini ambazo zimekuwa zikishindwa kutekeleza maagizo ya Kamati na hoja za CAG.
Taarifa hiyo imesomwa na Mwenyekiti wa LAAC na Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu Ado, kwa niaba ya Kamati hiyo.
HABARI:
Taharuki, simanzi na vilio vimetanda katika Mtaa wa Makulu jijini Dodoma baada ya nyumba ya familia ya Mzee Benedict Wilson, ambaye ni askari mstaafu, kubomolewa huku familia hiyo ikieleza kuwa imeachwa bila makazi.
Mama wa familia hiyo, Veronica Mwachali Bilingi, amesema familia hiyo imekuwa ikiishi katika eneo hilo tangu mwaka 1978 na kwamba awali walipopimiwa waliambiwa nyumba zao zilikuwa katika eneo linalopaswa kupisha barabara.
Kwa mujibu wa Veronica, katika mkutano uliofanyika wakati wa upimaji walipewa ahadi kuwa wangelipwa fidia kwa ajili ya kupisha eneo hilo, lakini fidia hiyo haikutolewa.
Badala yake, amesema nyumba yao iliwekewa alama ya X, huku familia ikiendelea kufuatilia hatma ya nyumba hiyo bila kupata majibu ya mwisho hadi ilipofikia hatua ya kubomolewa.
Hata hivyo, katika maelezo yake, Veronica ameibua madai mengine akisema familia hiyo imekuwa katika mgogoro na Diwani wa Kata ya Makulu tangu mtoto wake wa kiume alipoamua kuingia kwenye siasa za upinzani.
Amesema mtoto wake aligombea nafasi ya Udiwani wa Kata ya Makulu kupitia CHAUMMA baada ya kuhama CHADEMA.
Kwa upande wake, Peter Mwachali, ambaye ni mtoto wa familia hiyo, amesema wakati zoezi la ubomoaji likiendelea alijaribu kurekodi tukio hilo kwa kutumia simu yake, lakini alidai kuwa alizuiwa na watu waliokuwa eneo hilo.
Peter amedai kuwa katika tukio hilo alipigwa na simu yake ikavunjwa.
Wakati huo huo, tulipomtafuta kwa njia ya Simu Diwani wa Kata ya Makulu, Samson Mkopi, ambaye ametajwa na familia hiyo, alituomba tufike ofisini kwake siku ya kesho ili kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu madai hayo.
Hadi sasa, Jamii Voice inaendelea kufuatilia kwa undani madai ya familia hiyo.
MICHEZO:
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limefafanua msimamo wake kuhusu utekelezaji wa Katiba ya Klabu ya Simba iliyorekebishwa na kuidhinishwa na mamlaka husika, likisisitiza kuwa klabu hiyo inapaswa kutumia vyombo na taratibu zake halali katika kutekeleza maamuzi yaliyopitishwa na wanachama wake.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha, amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha Katiba ya klabu inatekelezwa na kufuatilia utekelezaji wa mambo yaliyopitishwa na wanachama, lakini haiwezi kufanya maamuzi kwa niaba ya Klabu ya Simba.
Marekebisho ya Katiba hiyo yalipitishwa katika Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Klabu ya Simba uliofanyika Novemba 30, 2025, na baadaye kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama na Vilabu vya Michezo kwa uchambuzi na kuidhinishwa kwa mujibu wa sheria na kanuni husika.
Kwa mujibu wa BMT, baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa kisheria, Msajili wa Vyama na Vilabu vya Michezo alikabidhi rasmi Katiba ya Simba iliyorekebishwa tarehe 18 Februari, 2026, ili ianze kutumika.
BMT imesema utekelezaji wa maamuzi yaliyomo katika Katiba hiyo haupaswi kufanywa na Serikali kwa niaba ya klabu, kwa kuwa maamuzi hayo yalifanywa na wanachama kupitia Mkutano Mkuu na baadaye kuidhinishwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Serikali imeeleza kuwa iko tayari kuipokea Klabu ya Simba kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusu masuala yoyote ya kiutawala yanayohitaji uelewa zaidi, kwa mujibu wa mamlaka na taratibu zilizowekwa kisheria.
Baraza hilo pia limetoa wito kwa Klabu ya Simba kutumia vyombo vyake halali na taratibu zilizowekwa katika Katiba yake ili kukamilisha utekelezaji wa marekebisho hayo, huku ikihakikisha masuala yoyote yanayohitaji ufafanuzi yanawasilishwa kwa mamlaka husika.
“Serikali itaendelea kutekeleza jukumu lake la kisheria la kuendeleza sekta ya michezo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, huku ikilenga kuhakikisha masuala ya maendeleo ya michezo yanazingatia utulivu, uwazi, uwajibikaji na maslahi ya wananchi na wapenda michezo,” imeeleza taarifa hiyo
HABARI:
Serikali kupitia Idara ya Huduma za Habari MAELEZO imesitisha leseni ya gazeti la Mwanahalisi kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Agosti 19, 2026, ikieleza kuwa gazeti hilo limekiuka masharti ya leseni yake na kanuni za uandishi wa habari.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara hiyo, uamuzi huo umechukuliwa baada ya gazeti hilo kuchapisha habari katika kurasa zake za 1, 2 na 3 za toleo namba 571 la Agosti 6–12, 2026, yenye kichwa “Nchimbi agoma kujiuzulu”, ambayo Serikali imesema haikuzingatia usahihi na mizania kabla ya kuchapishwa.
Maelezo imeeleza kuwa gazeti hilo lilishawahi kupewa onyo la maandishi Mei 8, 2026 baada ya makosa yaliyofanana kujitokeza katika toleo la Aprili 30 hadi Mei 6, 2026.
Baada ya kubaini ukiukwaji huo, Mkurugenzi wa Habari Maelezo aliipa Mwanahalisi fursa ya kusikilizwa kuhusu tuhuma hizo katika kikao kilichofanyika Dar es Salaam Agosti 7, 2026.
Katika majadiliano hayo, Maelezo ilieleza kuwa ufafanuzi uliotolewa na gazeti hilo haukuondoa haja ya kuchukuliwa hatua, ikiwemo suala la kuzingatia misingi ya taaluma ya uandishi wa habari, hususan usahihi na umakini katika kuripoti habari.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa katika majadiliano hayo zilibainika dosari nyingine za kiuandishi, ikiwemo kukosekana kwa usahihi na umakini katika baadhi ya habari zilizochapishwa.
Maelezo pia imeeleza kuwa baadhi ya habari zilikuwa na madai yaliyohitaji uthibitisho zaidi, huku nyingine zikihusisha watu katika tuhuma bila kuonyesha ushahidi wa kutosha wa madai hayo.
Kwa mujibu wa Idara hiyo, gazeti hilo pia lilikuwa limepewa fursa nyingine ya siku tatu kuwasilisha maelezo ya ufafanuzi, lakini baada ya majadiliano hayo Mkurugenzi wa Habari Maelezo aliona makosa yaliyobainika yanastahili kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Hatua hiyo imefanya Mwanahalisi kusitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo kwa kipindi cha miezi sita.
#Soma zaidi kupitia kurasa rasmi za Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.