VIDEO:
Mwanamuziki na mfalme wa mashairi Tanzania, Selemani Msindi maarufu kama Afande Sele, ameeleza kuwa kitendo cha kukamatwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, kinaweza kuchochea hasira za wananchi, hasa katika kipindi hiki ambapo taifa lipo katika majonzi kutokana na masaibu yaliyotokea tangu Oktoba 29, 2025.
Afande Sele ameyasema hayo Novemba 5, 2025 wakati akizungumza na Jambo TV mkoani Morogoro, na kuongeza kuwa ni wakati sasa wa haki kutendeka, kwani haki ndiyo msingi wa amani.
Novemba 4, 2025, Wakili Hekimu Mwasipu, ambaye ni mmoja wa mawakili wa Heche, alithibitisha kuwa Heche alisafirishwa kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam, ambako anatarajiwa kufikishwa mahakamani kusomewa mashtaka yanayomkabili baada ya takribani wiki mbili za kuwa mikononi mwa Jeshi la Polisi.
Wakili huyo alitaja kosa la kwanza analotuhumiwa mteja wake kuwa ni kujihusisha na vitendo vya kigaidi kutoka Kimara mpaka Magomeni, na tuhuma ya pili inahusu kujihusisha na vitendo vya kigaidi maeneo ya Msewe na External.
VIDEO:
Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, James Mbatia amesema hali iliyojitokeza siku na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 nchini Tanzania, si suala la kisiasa pekee bali ni “maumivu ya wananchi walio wengi dhidi ya wachache”, kutokana na hali hiyo kugubikwa na maumivu, vifo- miongoni mwa mambo mengine.
Akizungumza na Jambo TV tarehe 5 Novemba 2025, Mbatia amesema hali hiyo haiwezi kufananishwa na migogoro ya kawaida ya kisiasa bali ni mwelekeo unaohitaji “fikra pana na pevu” ili kurejesha umoja wa kitaifa.
Amesema ni muhimu kila mwenye nafasi na sauti nchini kuzungumza wazi bila woga juu ya matukio hayo, akisisitiza kuwa hatua ya kwanza ya uponyaji wa taifa ni kurudisha utu kwa familia za waliopoteza maisha.
“Sasa tunajiuliza tufanye nini? Hatua ya kwanza ya maafa haya, kwenye maumivu haya, tupewe miili yetu, mashujaa wetu waliouawa ambao ni utamaduni kwenye utamaduni wetu, uungwana wetu wa kiimani na vinginevyo ili tuweze kuwasitiri vinginevyo ili tuweze kuwasitiri ndugu zetu, tukawazika kwa heshima mashujaa wetu bila kuendeleza ghadhabu zaidi kwakuwa mdharau mwiba mguu huota tende”, ameeleza.
Kauli ya Mbatia imekuja siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, kueleza kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria katika sehemu chache za nchi wakati wa uchaguzi, lakini vyombo vya usalama vilichukua hatua haraka, kitaalamu na kwa uthabiti kukabiliana na hali hiyo.
Aidha, katika hotuba yake ya kuapishwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alionesha masikitiko yake kutokana na kile alichokitanabaisha kama matukio ya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha na uharibifu wa mali za umma na za watu binafsi, hasa katika majiji na miji, vilivyojitokeza kipindi cha uchaguzi.
#TANZANIA:TULIANZA NA UHURU WA KUKUSANYIKA, KUISHI MAONI SASA TUMEINGIA UHURU WA KUABUDU.
ANAANDIKA ASKOFU BAGONZA
KAMA NI KWELI: Inaweza kumaanisha hivi..
Eti Kanisa Limefungwa au kufutiwa usajili. Kisa? Kiongozi wake kakosana na waliomsajili au kadaiwa kuhubiri kinyume na alivyotegemewa.
Kama ni kweli; tujifanye kuuliza? Kanisa ni mali ya mtu? Kama kakosea yeye, kwa nini kanisa lifungwe? Yaani mdomo utoe matusi halafu makalio ndiyo yachapwe kiboko?
Hakuna kanisa linalotuma mtu kuchochea, kutukana, kubaka, kuiba nk. Kama lipo, zipatikane miniti za kikao kilichoruhusu hayo. Kinyume na hayo ni kuingilia uhuru wa watu kuabudu. Uhuru wa kuabudu ni wa msingi sana maana unaruhusu hata kuabudu watawala. Tusiwachagulie watu ibada.
Bado siamini kama ni kweli kwa sababu zimetoka barua mbili: moja ina sahihi na nyingine haina sahihi.
Kama ni kweli kanisa limefungwa, maana yake yaweza kuwa hii;
1. Tangu sasa viongozi wote wa dini zote, watatakiwa kutoa nakala ya mahubiri yao kwa wakuu wa serikali siku mbili kabla ya ibada ili yahakikiwe.
2. Maimamu, mashehe, mapadre na wachungaji walio kwenye maeneo ya kata, wawasilishe mahubiri yao kwa Maafisa Watendaji wa Kata siku mbili kabla ya ibada.
3. Endapo Maafisa wa serikali watakosa muda wa kupitia na kuhariri mahubiri hayo, ibada ziahirishwe kusubiri uhariri huo.
4. Atakayehubiri bila kuhaririwa na akaenda kinyume, faini pekee haitoshi, kifungo kina unafuu bali kanisa/hekalu/msikiti utafungwa.
5. Maafisa wa serikali ngazi zote watatakiwa kwenda kozi ya kujifunza elimu ya dini na Teologia ili kufanya udhibiti huu kwa umakini.
6. Maafisa wote wa serikali itabidi wazikane dini zao ili wasije kuonea au kupendelea dini yoyote.
7. Upelekwe muswada bungeni haraka sana, tena kwa hati ya dharula, ili kubadili katiba na kutamka kuwa serikali yetu sasa ina dini rasmi isiyotamkika jina lake na dini nyingine zimefutwa na kubakiza hiyo dini ya serikali.
8. Viongozi hawataruhusiwa tena kuapa kwa misahafu ya dini zilizofutwa. Misahafu hiyo itakuwa imefikia ukomo wa matumizi maana inasababisha viongozi wa dini kufanya uchochezi.
9. Sikukuu za kidini zinafutwa rasmi na hakuna mapumziko siku hizo.
10. Mahusiano ya kibalozi na nchi zote zenye kutambua uwepo wa dini zilizofutwa au kufungiwa yanafungwa mara moja. Mabalozi wa nchi hizo walio nchini waondoke na mabalozi wa kwetu walio nchi hizo warejee nyumbani.
11. Tangu sasa ni marufuku kuomba sala ili kula chakula na ndoa zote zenye uhalali wa kidini hazitambuliki tena.
12. Wimbo wa Taifa uondoe neno Mungu kwa sababu Mungu huyo anaweza kuleta uchochezi wakati wowote.
Tulianza na uhuru wa kukusanyika, tukaja uhuru wa kuishi, tukaingia uhuru wa maoni, hatimaye tutakuwa tumeingia uhuru wa kuabudu. Imebaki nini? Uhuru wa kujinyonga?
I hope ninaota siyo kweli. Ni mitandao tu inazusha na kufanya uchochezi.