"Dunia duara lakini usiombe ikuweke kati ikakuzunguka, au izunguke muelekeo tofauti na wako. Jitahidi uwezavyo uwe nje ya mduara na uzunguke nayo." ~Togolani Mavura.
"Tunamuomba Mungu atutazame na atuinue bila kujiuliza kabla ya kuomba kuinuliwa wewe umemuinua nani? Mungu huwainua zaidi wale wenye kuwainua wa chini yao ili wengine wainuke kupitia aliyowainua, kuliko kumuinua yule atakayeinuka pekeyake. Ndio maana mwenye nacho huongezewa."
"Sote tunazo ndani yetu mbegu za wema na ubaya, chuki na upendo, utu na unyama. Matokeo ya hulka zetu hutegemea tu mbegu ipi tunaistawisha." ~Togolani Mavura.
"Kadri wengi wanapokata tamaa na kuishia njiani, ndio fursa hupanuka zaidi kwa wale wachache wanaopiga moyo konde na kuendelea. Daima wenye kujaribu ni wengi lakini wenye kufanikiwa ni wachache. Mafanikio hayana budi kusindikizwa na kupambwa na msafara wa wanaofeli."
"Kwa kila mmoja unayemuinua, unainua kizazi. Kwa kila mtu unayemuangusha unaangusha uzao wake. Ukimbadilisha adui kwa wema umeokoa uzao wake." ~Togolani Mavura.