@MadiniTanzania Jambo jema,ila ingependeza yakakusanywa maoni kutoka kwa wachimbaji kwa sababu wao ndo wahuska wakuu na wanaelewa changamoto
mfano Pesa ya kufanya drilling,Vifaa vya kusagia mawe,na vitendea kazi Bora ...
Hv vyote huwezi vipata bila kuwahsisha hawa watu
STAMICO KUENDELEZA LESENI ZA UCHIMBAJI DHAHABU KIGOSI
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lipo katika hatua nzuri ya kuendeleza leseni nane linazozimiliki katika Hifadhi ya Pori la Kigosi Mkoani Geita ambalo hivi karibuni limeruhusiwa kufanya shughuli za uchimbaji wa madini.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO,Dkt.Venance Mwasse alipotembelea eneo hilo leo tarehe 4 Aprili, 2025.
Katika kikao kifupi kilichofanyika leo,Dkt Mwasse alibainisha kwamba STAMICO itaendelea kutekeleza jukumu lake la ulezi na uwezeshaji kwa wachimbaji wadogo.
Hata hivyo, alitoa angalizo kwa wachimbaji wadogo kutovamia leseni za Shirika zilizopo eneo hilo kwani kwa kufanya hivyo kutafifisha juhudi za kuwahudumia.
Aliongeza pia kuwa Shirika lina mpango wa kupeleka mtambo mdogo wa uchorongaji eneo la Kigosi ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kwenye shughuli za utafiti kwa gharama nafuu.
Katika ziara hiyo,Dkt Mwasse aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Mbogwe, Mha. Jeremiah Hango, Afisa Tawala Wilaya ya Bukombe, Bw. Limbe Charles Ndaki na Mwakilishi Mhifadhi Mkuu Pori la Kigosi, Bw. Peter Edson Kibona.
Kwa upande wa STAMICO,aliambatana na Mjiolojia Mkuu wa Shirika Bw.Alex Rutagwelela pamoja na Mhandisi Uchenjuaji Bw Tiberio Kaduma.
Pia alitembelea na kujionea shughuli za uchimbaji mdogo zinazofanywa na kampuni ya NGM ambayo katika ziara hiyo iliwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Bw Emmanuel Gungu.
Aidha, Dkt. Mwasse alibainisha kwamba ili kuwawezesha zaidi wachimbaji wadogo, Shirika lipo tayari kuwapa taarifa za utafiti wa maeneo ambayo kwa sasa wanayamilki kihalali ndani ya hifadhi hiyo ambayo hapo awali yalikua chini ya umiliki wa STAMICO.
Katika hatua nyingine, Dkt Mwasse alitoa wito kwa wachimbaji wadogo kujikita kufanya uchimbaji salama ndani ya maeneo au vitalu vyao walivyogawiwa na Tume ya Madini hivi karibuni na kuacha kufanya uvamizi katika maeneo yenye leseni za STAMICO.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Mbogwe alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO kwa ziara hiyo na kumuahidi kumpa ushirikiano katika kuhakikisha leseni zinazosimamiwa na Shirika zinakuwa salama muda wote.
Aidha, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mbogwe pamoja na Ofisi inayosimamia pori la Kigosi ziliahidi kutoa ushirikiano kwa Shirika katika kusimamia miradi iliyomo katika pori hilo.
Dkt Mwasse pia alitembelea mtambo wa kuchenjua na kuchakata dhahabu unaomilikiwa na Kampuni ya NGM uliopo Ushirombo Mkoani Geita.