NAZUNGUMZA KAMA MZAZI MWENYE WATOTO WA KIKE NA KIUME.
Hii haki ya kumuua binadamu mwenzako kwa sababu ya mapenzi unaitoa wapi aisee??
Yani nilee binti yangu mpaka amekuwa mtu mzima, nimgharamie kuja Chuo Kikuu, kisha wewe ukutane naye tu na kuanzisha mahusiano yanayokupa haki ya kumchoma visu na kumuua??
Ni sababu gani ya kimapenzi ambayo unahisi ni nzito kiasi cha kukupa haki ya kuondoa uhai wa binti yangu?
Kuna namna jamii yetu inapaswa kufunda upya vijana wa kiume.
Mara nyingi haya matukio ya mwanaume kuuwa mwanamke kwa sababu za mapenzi ni matokeo ya entitlement tuliyomjengea mtoto wa kiume.
Tumewajengea watoto wa kiume dhana mbaya sana inayowafanya waamini wana haki ya kumfanya mwanamke chochote.
Na hili linaanza mapema kabisa pale ambapo kijana anamfanyia binti ukatili wa wazi kabisa huku jamii ikimpuuzia na hata kumchochea kwa hoja kwamba “huyu ni mumeo, unapaswa kumheshimu.”
Chukulia kwa mfano cheating. Cheating imegeuzwa kuwa dhambi kubwa ajabu kwa mwanamke lakini wakati huo huo ni haki kwa mwanaume.
Kamwe hausikii jamii ikimzungumzia mwanaume malaya, hata kama ana wanawake 100. Ila mwanamke akifanya hivyo hata na mwanaume mwingine mmoja tu, tayari inageuka kuwa dhambi ya milenia.
Sio ajabu kabisa kukuta mwanaume anayecheat na wanawake kibao ndio huyo huyo anayempiga na kumsulubisha mwanamke kwa hoja kwamba “ana tabia za kimalaya; hatulii; hajiheshimu.”
Mwanaume huyu huyu anayecheat anaweza kabisa kumuua huyu binti kwa kucheat na jamii ikamtetea kwa hoja kwamba “alishindwa kudhibiti hasira.”
Hasira nayo imekuwa ni haki ya mwanaume lakini sio haki kwa mwanamke.
Mwanamke anafanyiwa ukatilia wa ajabu lakini analazimishwa na jamii kuvumilia na kunyamaza.
Hata akimfumania mumewe right hand, ataambiwa “wanaume wameumbwa hivyo; wana tamaa. Unapaswa kuvumilia.”
Hii sio sawa hata kidogo.
Mwanamke naye ni binadamu; ana haki za kuishi na kufurahia maisha yake kama ilivyo kwa mwanaume.
Ana haki ya kuwa huru kufanya maamuzi yake ya kimapenzi na kingono kama ilivyo kwa mwanaume.
Ukiona tabia za mwanamke haziendani na matarajio yako, ni kiasi cha kuachana naye tu na kutafuta mwingine.
Kama jamii tunapaswa sio tu kukemea bali pia kuhakikisha wanaotekeleza haya wanakutana na consequences.
Tufundishe vijana wetu wa kiume tangu wanapokuwa wadogo kuwa mwanamke sio mali yake wala subject wake.
Tuwafundishe kuwa mwanaume hana haki yoyote juu ya maisha ya mwanamke kiasi cha kuamua kumnyanyasa na hata kumuua.
Tuwafundishe pia kuwa hoja “hasira” kuwa ni hoja ya kipumbavu na kikatili. Ni hoja ambayo mara nyingi tumekuwa tukiitumia kuhalalisha ukatili dhidi ya wanawake.
Tuwafundishe pia kuwa hoja ya “nimemgharamia” ni hoja ya kikatili na kipumbavu.
Hakuna kiasi cha fedha kinachoweza kukupa uhalali wa kumiliki na hata kuondoa uhai wa binadamu mwingine; kutweza utu wa binadamu mwingine.
Mabinti zetu wana haki ya kuishi; wana haki ya kupursue ndoto zao pasipo kuwa na hofu kwamba siku moja mwanaume fulani aliyetamani tako au sura yake atammiliki kama mali yake na hatimaye kuja kuondoa uhai wake.
Mwisho, ifike mahali matukio ya kikatili kama haya yaadhibiwe kwa uzito wa kutosha ili yatume ujumbe sahihi kwa wengine.
Jaribu kutafakari tu namna mzazi wa huyu binti anavyopokea hii taarifa.