Tanzania haihitaji hofu zaidi.
Inahitaji uponyaji.
Kwa sababu taifa lililojeruhiwa, mwishowe huanza kujijeruhi lenyewe.
Leo tunapaswa kusema ukweli
si kwa chuki,si kwa kisasi,bali kwa hofu ya kweli kuhusu mustakabali wa nchi yetu.
Kama Michael Jackson alivyowahi kusema:
“Tunapaswa kuponya dunia yetu iliyojeruhiwa. Machafuko, kukata tamaa, na uharibifu usio na maana tunaouona leo ni matokeo ya watu kujisikia wametengwa kutoka kwa wenzao na mazingira yao.”
Kauli hii kwa sasa
Inakuwa onyo hata kwetu sisi Watanzania, kama sehemu ya dunia
Wananchi wanapoanza kujisikia:
hawasikilizwi, wametengwa, wananyamazishwa, wanadhalilishwa,
au wanachukuliwa kama maadui kwa sababu tu wana mawazo tofauti.
umbali wa hatari huanza kujengwa kati ya wananchi na dola.
Na historia inatufundisha jambo moja la kuogopesha:
Mataifa mengi hayaanguki kwanza kwa sababu ya adui wa nje.
Huanzia kudhoofika ndani
wakati imani ya wananchi inapokufa.
Nchi haiwezi kujenga amani ya kudumu:
kama hofu inakuwa kubwa kuliko uhuru, kama utii unakuwa muhimu kuliko ukweli, kama taasisi zinaonekana kuwa za upande mmoja, au kama ukosoaji unatafsiriwa kama usaliti.
Kwa sababu jamii iliyojeruhiwa huzalisha wananchi walioumia.
Na wananchi walioumia mwishowe huzalisha:
hasira, mgawanyiko, msimamo mkali, kukata tamaa,au chuki ya kimya kimya.
Viongozi wanapaswa kuelewa:
si kila ukimya ni amani.
Wakati mwingine watu wananyamaza kwa sababu:
wamechoka,wanaogopa,au wamekata tamaa.
Na kukata tamaa ni hatari kwa taifa lolote.
Tanzania ilijengwa juu ya msingi imara ya : utu,umoja,mazungumzo,
uvumilivu,na hisia ya kuwa taifa ni la wote.
Julius Nyerere alielewa jambo kubwa sana,taifa haliishi kwa nguvu pekee (power)
linaishi pia kwa uhalali wa kimaadili.
Wananchi wakianza kuhisi kwamba:
haki inategemea upande wa kisiasa, ambao mtu yupo, taasisi si huru tena,
au demokrasia ipo kwenye maneno lakini si kwenye vitendo,
ule mkataba wa kihisia kati ya taifa na wananchi huanza kupasuka.
Kwa hiyo haya si mashambulizi.
Hili ni onyo.
Onyo kwamba:
siasa zinapokuwa za uhasama kupita kiasi,
mamlaka zinapoanza kuogopa ukosoaji,
wapinzani wanapoonekana maadui,
na wananchi wanapopoteza imani kwa mifumo ya taifa
taifa lenyewe huanza kujeruhiwa kihisia.
Na taifa lililojeruhiwa huwa taifa lisilo tulivu.
Hatuhitaji kulewa kisiasa zaidi.
Tunahitaji hekima.
Hatuhitaji viongozi wanaotaka kusifiwa tu.
Tunahitaji viongozi wenye uwezo wa kusikiliza ukweli usiofurahisha.
Kwa sababu uzalendo si ukimya.
Wakati mwingine uzalendo ni ujasiri wa kusema:
“Kuna jambo linaenda vibaya kabla hatujachelewa.”
Kama Tanzania inataka kubaki imara,
basi uponyaji lazima uwe sera ya taifa.
Uponyaji:
kati ya viongozi na wananchi,kati ya dola na upinzani,kati ya mamlaka na uwajibikaji,kati ya sheria na haki.
Kwa sababu hakuna taifa linaloweza kuishi milele kwa:
hofu, propaganda,au mgawanyiko wa kihisia.
Mwisho wa yote,
taifa huwa imara zaidi pale wananchi wake wanapoamini kwamba:
wao ni sehemu ya taifa,wanalindwa,
wanasikilizwa,na utu wao una thamani.
Mungu ailinde Tanzania isije kuwa nchi ambayo wananchi wanaogopana kuliko kuaminiana.
Na viongozi wetu wakumbuke:
historia haitawahukumu viongozi kwa barabara, madarasa , vituo vya afya walivyojenga pekee,
bali pia watahukumiwa kwa hali ya kihisia walizoliachia taifa.
Usisahau:
“Jamii iliyojeruhiwa huzaa watu waliojeruhiwa…
na watu waliojeruhiwa huongeza machafuko zaidi.”
Rev Petet simon Msigwa!
Iringa
Chaumma inavyosherehekea siku ya Wanawake Duniani leo 08 Machi,2026 Ubungo plazza ,Dar Es salaam. Ni mara ya kwanza Wanawake wa Chaumma kusherekea siku yao kwa kuwa pamoja kwenye Kongamano.
@HakiBalozi255 Utakubaliana nami kuwa katika utekelezaji wa athma yetu ya kudai mageuzi Kuna sehemu tulijiongoza vibaya pamoja na kwamba Nia ni Njema sana. Mwisho Sasa NRNE inatumika kama kinga ya CCM kupita bila upinzani kwani hata wale walioamua kupambana Bado wanazomewa na kukatishwa tamaa
Leo July 19,2025 kwenye Uzinduzi wa Ofisi ya CHAUMMA Kilimanjaro imeambatana na Zoezi la Uchukuaji wa Fomu Za Ugombea ubunge na Udiwani.
Miongoni mwa waliochukua fomu za kutia nia ya Ubunge ni pamoja na Patrick Assenga kwa jimbo Moshi Mjini, Grace Kiwelu-Jimbo la Vunjo, Jimbo la Moshi Vijiji- Michael Kilawila, Jimbo la Rombo-Andrea Oisso, Jimbo la Mwanga- Henry Kileo, Jimbo la Same Magharibi- Gervas Mgonja na Jimbo la Same Mashariki-Allan Mmanyi huku Jimbo la Siha na Hai likiwa bado halijapata wachukua fomu.
Aliyekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA Taifa Andrea Oisso, ambaye hapo awali alitangaza kujiondoa CHADEMA kutokana na kutokubaliana na msimamo wa chama hicho kuchukua mrengo wa kususia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa madai ya kutaka mageuzi kwanza, ameweka wazi kuwa tayari amepata jukwaa jingine la kisiasa atakalolitumia kuendeleza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Rombo.
Andrea Oisso amebainisha kuwa sasa ni mwanachama rasmi wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), na tayari amekabidhiwa kadi ya chama hicho na Naibu Katibu Mkuu wa CHAUMMA bara, Benson Kigaila. Amesisitiza kuwa hakuhama CHADEMA kwa lengo la kuwasaliti wenzake walioko katika mapambano ya mabadiliko, bali kwa nia ya kuhakikisha kuwa anaendelea kukabiliana na utawala wa CCM kupitia njia nyingine halali za kisiasa.
“Dhamira yangu ya kuwatetea wananchi wa Rombo haijawahi kuyumba. Nilitangaza mapema kuwa nitaendelea kupigania haki zao, na sasa nimepata jukwaa la kufanya hivyo. CCM Rombo haitapita bila kuwekewa upinzani wa kweli,” amesema Oisso.
Ameeleza kuwa nchi imeendelea kuwa maskini na mifumo yake kutokuaminika kwa sababu ya utawala wa muda mrefu wa CCM, na kwamba si sahihi kuisubiri CCM ilete mageuzi yenyewe huku wapinzani wakikaa pembeni. “Kuendelea kuwaachia eti hadi waje wenyewe na reforms ni kuwaongezea nguvu zaidi. Sisi tutasimama. Rombo tukiamua tunaweza,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Oisso ametoa rai kwa watu wote wanaoamini katika mabadiliko kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia CHAUMMA. Ameeleza kuwa mchakato wa kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi za Udiwani, Udiwani Viti Maalum na Ubunge umefunguliwa rasmi na chama hicho kuanzia tarehe 01 Julai 2025.
Kwa Mkoa wa Kilimanjaro, zoezi hilo linaratibiwa na Katibu wa CHAUMMA Mkoa, Bazil Lema ambaye pia ndiye Mratibu wa Uchaguzi wa Mkoa huo. Andrea Oisso amethibitisha kuwa naye atachukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea Ubunge wa Rombo muda si mrefu.
“Bila kujali kejeli na dhihaka za wachache walioamua kuisaidia CCM, mimi nitasimama kuhesabiwa. Katika hili, hayupo wa kunirudisha nyuma. Rombo ni yetu sote, na wakati wa kusimama kwa ajili ya haki na maendeleo ndio huu,” amesema kwa msisitizo.
Oisso amehitimisha kwa kutoa wito wa mshikamano, akisema kuwa Rombo ni ngome ya mageuzi, na itaendelea kuwa hivyo endapo watu wake watasalia na ujasiri wa kusimama kwa ajili ya mustakabali wa kizazi kijacho.