Unatamani kusoma. Ukishasoma ndio ‘unagundua’ kumbe elimu si muhimu kama ulivyofikiri. Unaanza kuamini elimu haikusaidii maana tayari unayo. Unasahau elimu hiyo hiyo ndiyo imekuwezesha kujifunza mengi ya ziada yanayolingana na mahitaji yako.
Unatamani kupata kazi. Unazunguka na bahasha miaka. Ukiipata unafurahi mwezi wa kwanza, wa pili, wa tatu unaanza kuiona ya kawaida. Unaidharau. Unaanza kutafuta kazi nyingine wanayoiacha wengine.
Unapigwa na upweke, unakutana na mtu unayemwona ndiye ‘dunia’ yako. Hulali. Hutulii. Unapambana kumpata. Ukishampata, na kwa jinsi mnavyopendana, unawashangaa wasioelewana na wapenzi wao. Mara, hamadi, unaanza kujisikia mpweke kwenye mapenzi uliyoyahangaikia. Unaanza kuvutiwa na wasiokupenda ambao nao wanawachosha wapenzi wao.
Haturidhiki. Tulichonacho hakina thamani. Tunatafuta tusichokuwa nacho. Maisha yanageuka kuwa safari ya kupambania tusivyonavyo na bado tunashangaa kwa nini hatuna furaha.