MAKAMU WA RAIS AZINDUA KAMPENI YA MITI KITAIFA, MISITU YATAJWA NGUZO YA UCHUMI
Na Mwandishi Wetu, Lindi
MAKAMU wa Rais, Mhe Emmanuel Nchimbi, amezindua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya Upandaji Miti Kitaifa 2026, akionya kuwa kasi ya upotevu wa misitu nchini imefikia hekta 460,400 kwa mwaka na kuwataka Watanzania kuchukua hatua za haraka kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa uchumi na mazingira.
Akizungumza leo Machi 19, 2026 katika Uwanja wa Ilulu, Lindi, Nchimbi alisema misitu si tu chanzo cha maisha bali ni mhimili wa uchumi endelevu, akibainisha kuwa sekta hiyo inachangia asilimia 3.5 ya pato la taifa, na kufikia hadi asilimia 20 inapojumuishwa thamani ya huduma za mifumo ikolojia zisizo na bei ya soko.
“Leo tunazindua kampeni ya upandaji miti kitaifa ili kuongeza uhamasishaji wa wananchi kupanda na kutunza miti. Hatuwezi kuendelea kuvumilia upotevu huu wa misitu,” alisema.
Alifafanua kuwa Tanzania ina takribani hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 55 ya eneo lote la nchi kavu, lakini sehemu kubwa inakabiliwa na vitisho vya shughuli za binadamu zikiwemo uvamizi, uchomaji moto, ufugaji holela na matumizi makubwa ya kuni na mkaa.
Katika hotuba yake, Makamu wa Rais alisisitiza kuwa kampeni hiyo ni utekelezaji wa moja kwa moja wa maono ya Samia Suluhu Hassan kupitia ajenda ya “Tanzania ya Kijani”, akitaja kuwa zaidi ya miti milioni 113 tayari imepandwa tangu mwaka 2023.
Alitoa maagizo kwa viongozi wa mikoa na halmashauri nchini kuhakikisha wanatekeleza mikakati madhubuti ya upandaji miti kwa kuzingatia ekolojia ya maeneo husika, huku akisisitiza elimu kwa jamii na usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji.
Makamu wa Rais pia aliielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kuimarisha tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto za wakulima wa miti na kubaini aina sahihi za miti kwa kila eneo.
Aidha, aliagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuongeza uzalishaji wa miche ya miti na kuimarisha vitalu nchini ili kuhakikisha upatikanaji wa miche bora kwa wananchi.