Waziri wa Afya Ummy Mwalimu (@ummymwalimu) amepiga marufuku Vituo Binafsi kuwaondoa wodini Wagonjwa ambao ni Wanachama wa NHIF mara baada ya saa 48 kupita toka kutolewa kwa taarifa ya vituo hivyo.
Ummy amesema kufanya hivyo ni kuvunja sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalamu wa afya shirikishi Sura ya 152 inayowataka Madaktari kutositisha huduma kwa Wagonjwa ambao tayari wanawahudumia na wale Wagonjwa wa dharura.
Ummy amesema hayo Mkoani Lindi leo huku akisisitiza kuwa Wizara ya imepokea kwa masikitiko makubwa namna ambavyo baadhi ya Watoa huduma wameamua kusitisha huduma licha ya kupewa fursa ya kuwasilisha maoni na ushauri wao pamoja na ushirikishwaji mkubwa uliofanyika katika mchakato mzima wa maboresho ya Kitita cha Mafao cha NHIF cha mwaka 2023 ambapo imetoa rai kwa Hospitali zote zilizositisha kutoa huduma ziendelee kuwahudumia Wanachama hao.
Kauli hii ya Waziri Ummy inakuja kufuatia hali inayoendelea kwa sasa kati ya NHIF na Chama cha Wamiliki wa Vituo Binafsi vya huduma za Afya (APHFTA) ambayo imepelekea APHTA kutoa tamko la kutoridhia Kitita cha Mafao kilichofanyiwa mapitio na hivyo kuazimia kusitisha huduma kwa Wanachama wa NHIF, ambapo Hospitali za Kairuki, Regency, Hospitali za TMJ, Hospitali za Apollo na Hospitali zote za Agha Khan Nchini zimetangaza kusitisha huduma hizo kuanzia leo.
#MillardAyoUPDATES