Kuna kizazi tunaendelea kukitengeneza cha watu wanaoteswa na upweke lakini wanaochoshwa na upendo. Kizazi cha watu wanaohitaji kupendwa lakini hawajui namna ya kupenda. Hiki ni kizazi kilichozaliwa na kizazi cha wazazi wanaonekana kuwa na mafanikio lakini wasio na muda wa kupenda —kupatikana kihisia, kuzungumza, kusikiliza, kuhusiana, kujali na kadhalika. Hiki ni kizazi kinachoziba ombwe la kutokupatikana kwa kutumia vitu.
Tunahonga watoto midoli wasiyoihitaji kufunika hatia ya kutokupatikana. Mtoto akilia, kwa mfano, tunampa kishikwambi atulie. Katuni inatumika kupotezea hitaji la mtoto kusikika na kuonekana. Tukishindwa kuzungumza na mtoto tunawashia runinga anyamaze. Tukikosa muda wa kulea tunalipia chekechea ya bweni.
Kwa ugumu na maumivu makubwa, mtoto anajifunza namna mpya ya kushughulikia mahitaji yake ya kihisia. Upweke, kupuuza hisia, kucheza na hisia za watu, ubinafsi, kukweza vitu na wenye vitu inakuwa sehemu ya mahusiano. Mtazamo huu wa maisha unaunda mwelekeo mpya wa mahusiano na watu ili kumudu uhaba mkubwa wa upendo—kupatikana kihisia, kuzungumza, kusikiliza, kuhusiana na kujali.
Matokeo yake, tukifikia umri wa mahusiano, tunachoshwa haraka uhusiano unaotudai tupende. Tunataka kupendwa lakini hatuelewi upendo maana yake nini. Tunataka kuaminiwa lakini tunamchoka haraka anayetuamini. Hatujazoea kuaminiwa. Tunataka mtu aoneshe kujali lakini tunakinai haraka kujali kukimaanisha muda kwa ajili yetu. Tunatamani kueleweka lakini tunatishwa na muunganiko wa hisia. Tumezoeshwa vitu kutumika kama mbadala wa kuhafahamiana vizuri, kuunganika kihisia na shauku ya kuwa karibu na mtu.
Tunalea kizazi ambacho ukimnyima mtu muda wako ukampa pesa anaamini unampenda, hata kama utamuondoa kabisa kwenye ratiba zako. Ukimpa mtu muda wako, usikivu, ukawekeza kwenye mahusiano, lakini usiwe na pesa mtu anaona unamchosha. Ukimnyima muunganiko wa hisia, ukampa uhakika wa ufundi wa ngono anachagua ngono hata akikosa uhakika wa mahusiano ya kudumu. Jitihada zozote za kudumisha mahusiano bila ngono inaonekana ni mzaha na ndoto za abunuwasi.
Hatutaki kuwekeza, tunataka kupita. Hatutaki kudumisha, tunataka kusisimuka. Hatutaki kufahamiana, tunataka kutumiana. Hatutaki kujipa muda, tunataka kilicho tayari. Hatutaki gharama, tunataka matokeo. Hatutaki kutafuta, tunataka vya kupewa. Hatutaki kusubiri, tunataka ghafla. Hatutaki uaminifu, tunataka uhuru. Hatutaki usisi, tunataka umimi. Hiki ndicho kizazi kinachoishi matokeo halisi ya utoto uliotekelezwa—deprived childhood.